WATOTO WA KIKE MSIKUBALI KUDANGANYWA – WAZIRI MKUU
*Awaonya vijana, wazee wanaotaka kuwaoa, asema miaka 30 jela ni yao
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka
watoto wa kike wasikubali kudanganywa na wanaume na badala yake
wakazanie masomo hadi wahitimu elimu ya juu.
“Wasichana wote mliopo hapa, mwanaume
yeyote akikufuatafuata mwambie usinusumbue; mwambie niache nisome. Kamwe
msikubali kudanganyika, someni hadi mmalize Chuo Kikuu,” alisema.
Ametoa wito huo kwa nyakati tofauti
wakati akizungumza na wakazi wa wilaya za Same na Mwanga akiwa kwenye
ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za maendeleo mkoani Kilimanjaro.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa na ziara ya
siku nne mkoani humo, amewaonya vijana na wazee ambao wana tabia ya
kuweka mahusiano ya kimapenzi na watoto wa kike kwamba waache mara moja
la sivyo wataishia jela.
“Wanaume msisahau kwamba mtoto wa mwenzio
ni wako. Nataka niwakumbushe kuwa ukimuona mtoto wa kike, muache. Huyo
ni moto wa kuotea mbali. Ukimchumbia, ukimuoa, au kumpa mimba mtoto wa
kike, ujue kuwa miaka 30 jela ni yako.”
“Serikali ya awamu ya tano, imeamua
kuwekeza kwa mtoto wa kike, kwa hiyo tunataka watoto wa kike wakianza
shule ya awali, wasome shule ya msingi, waende sekondari hadi wamalize
Chuo Kikuu,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment