Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala, akizungumza katika uzinduzi wa Ilala ya Kijani.
Makamu Mwenyekiti wa UVCCM, Tabia Mwita akiwa ameshika zawadi ya picha ya Rais Dk. John Magufuli.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dar es
Salaam, Mussa Kilakala, akiendesha mnada wa keki ambayo ilinunuliwa kwa
Sh milioni 1.8 Kulia ni mgeni rasmi Makamu Mwenyekiti wa UVCCM, Tabia
Mwita.
************
NA MWANDISHI WETU
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umesema kuwa
sasa unajipanga kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kwa kuhakikisha
unampatia kura za heshima Rais Dk. John Magufuli.
Pamoja na hali hayo, UVCCM imesema ni vema chama kikatoa fursa
kwa vijana kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kama njia ya kumuenzi
Rais Magufuli ambaye ameamua kuwaamini katika nafasi mbalimbali za
uongozi serikalini.
Akizungumza Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Ilala ya Kijani,
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala, amesema wao
kama vijana kwa sasa wanatembea kifua mbele kutokana na kazi kubwa
inayofanywa na Rais Magufuli pamoja na wasaidizi wake, wakiwamo Makamu
wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na mawaziri.
Kilakala amesema viongozi hao wamekuwa wakijenga heshima kwa
nchi na chama kwa kuhakikisha wanasimamia falsafa na misingi ya CCM kwa
kuimarisha mshikamano kwa Watanzania.
“Ndugu Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa (Tabia Mwita), sisi
vijana wa Dar es Salaam tunatembea kifua mbele kwani Rais Magufuli
amekiheshimisha chama na taifa letu kwa ujumla na mwaka 2020 tutampatia
kura za heshima.
“Lakini pia kama kiongozi wa nchi (Rais Magufuli), ameweza
kuwaamini vijana basi na uchaguzi wa mwaka huu tunakiomba chama kitoe
tamko la kutokata majina ya wagombea vijana ambao muda wote wamekuwa
wakikijenga chama kwa kuimba ‘hiyena hiyena’ na sasa nao waweze kuingia
katika uongozi wa Serikali za Mitaa, udiwani na hata ubunge,” amesema
Kilakala.
Mgeni rasmi katika mkutano huo wa ndani, Makamu Mwenyekiti wa
UVCCM, Tabia Mwita, amesema kuwa ili kijana aweze kutimiza wajibu wake,
ni lazima ahahakikishe anajiandikisha na kuwa na kitambulisho cha
kupigia kura.
Tabia alisema hatua hiyo itahakikisha ushindi mnono wa CCM kwa
kushinda viti vya mitaa, vijiji na vitongoji pamoja na Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2020.
Amesema agizo la CCM ni kuhakikisha inashinda nafasi zote za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na Serikali Kuu.
“Kama kuna mtendaji yeyote atakayekwamisha uandikishaji kwenye
Daftari la Kudumu la Wapigakura toeni taarifa haraka ili tumpe taarifa
Mwenyekiti wa CCM Rais John Magufuli,” amesema Tabia.
Pia ametoa onyo kwa mataifa yanayojaribu kuisemea demokrasia ya
nchi na kuwataka watatue matatizo yanayowakabili badala ya kushughulika
na Tanzania.
Pia aliwataka viongozi wa chama hicho kushirikiana na kuepuka migogoro ya ndani inayokigawa chama hicho kipindi cha uchaguzi.
“Tuacheni tabia za kubomoana wenyewe kwa wenyewe, tunahitaji
ushirikiano na muelekezane kwa utaratibu uliowekwa na chama,” amesema
Tabia.
Mwenyekiti wa UVCCM, Wilaya ya Ilala, Amani Pazi, amesema
wamefanya uchunguzi na kubaini kwamba asilimia 80 ya wapigakura ni
vijana, hivyo ili kuweza kushinda uchaguzi wagombea vijana wapewe
kipaumbele zaidi.
Katika mkutano huo, wanachama 200 walijiunga na CCM akiwamo
aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) upande wa
Vyuo Vikuu, Jackson Nzinza.
No comments:
Post a Comment