NITAMTUMA WAZIRI MHAGAMA AJE MAKANYA – WAZIRI MKUU
*Ni katika mashamba ya mkonge, apokea kilio cha wafanyakazi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
atamtuma Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia
Sera, Uratibu, Kazi, Ajira na wenye Ulemavu, Bi. Jenista Mhagama aende
Makanya, wilayani Same, kwenye mashamba ya mkonge akatatue kero za
wafanyakazi.
“Nitamleta Waziri wa Nchi anayesimamia
masuala ya kazi, aje afuatilie kero za wafanyakazi hapa Makanya, manake
watumishi wameweka malalamiko yao kwenye mabango na mimi nimeona
wanaoendesha mitambo hawana gloves, wengine wamevaa kandambili badala ya mabuti, kofia za usalama nimeambiwa ziko 20 tu…” alisema Waziri Mkuu.
Ametoa ahadi hiyo jana (Ijumaa, Julai 19,
2019) wakati akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha kuchakata katani
kilichopo kwenye shamba la mkonge la Hasani, kata ya Makanya, wilayani
Same, Kilimanjaro, mara baada ya kukagua uzalishaji kwenye kiwanda
hicho.
Alifikia uamuzi huo baada ya kusoma
mabango yaliyokuwa yakitoa ujumbe juu ya hali mbaya kiwandani zikiwemo
malipo ya sh. 3,800 kwa siku; mikataba mibovu ya kazi; wafanyakazi
kutothaminiwa wanapougua na kutoridhika na mawakala wawili ambao ni
UNIQUE na UPANI waliowekwa kusimamia uendeshaji wa shamba hilo. UNIQUE
inasimamia wakata mkonge na UPANI inasimamia kazi ya upandaji na upanuzi
wa mashamba.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alimweleza Meneja
wa Mashamba ya METL likiwemo la Hasani, Bw. Ndekiwa Nyari kwamba uamuzi
wa kuweka mawakala unawapunguzia wenye kampuni mzigo wa usimamizi
kwenye mashamba lakini unaipa hasara kampuni yao.
“Kwa sasa unashughulika na watu watatu au
wanne ambao ni mawakala wakati watu wote wanaokuzalishia wako hapa. Ni
vema ungeajiri hao watu wanne, ukawasimamia kwa karibu na unaweza kuwapa
motisha wakifanya vizuri au kuwafukuza wakiharibu. Lakini kwa sasa hawa
mawakala huna mamlaka hayo, sababu ulishaweka mkataba nao,” alisema.
“Ni bora uwe na idara mbili za upandaji
na uvunaji, kisha uweke wasimamizi watatu au wanne ambao watawajibika
kwako moja kwa moja. Hii system uliyotumia ina walakini hasa
kwenye maslahi ya wafanyakazi. Unawalipa fedha lakini haifiki yote kwa
wafanyakazi,” alisema na kuamsha shangwe miongoni mwa wafanyakazi hao.
Wakati huohuo, Waziri
Mkuu alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa Makanya wajipange na
kutafuta maeneo ya ekari tatu hadi nne ili nao waanze kulima mkonge
ambao alisema watakuwa wanauuza kwenye kiwanda hicho.
“Niwasihi wananchi wa hapa na vijiji
jirani ingieni kwenye kilimo cha mkonge kwa sababu kina soko ndani na
nje ya nchi. Tafuteni maeneo ya ekari tatu au nne anzisheni kilimo cha
mkonge sasa. Zao hili lipo kwenye mazao ya nyongeza ya mkakati ambayo ni
chikichi na mkonge.”
“Na uzuri wake unalima mara moja tu,
halafu kila mwaka unakuwa unavuna tu. Viongozi wa Serikali ya Kijiji
simamieni jambo hili,” alisisitiza.
Mazao mengine ya mkakati ambayo Serikali
ya awamu ya tano ilianza kuyatilia mkazo ili kuimarisha uzalishaji wake,
upatikanaji wa pembejeo na masoko ni pamba, chai, tumbaku, kahawa na
korosho.
Mapema, akitoa taarifa
juu ya uzalishaji kwenye kiwanda hicho, Bw. Nyari alisema shamba lote
lina ukubwa wa ekari 2,453 na kwamba uzalishaji umekuwa ukiongezeka
kidogo kidogo ambapo mwaka 2014 walizalisha tani za mkonge 713 na hadi
kufikia mwka 2018 walifikisha tani 890 za mkonge. “Mwaka huu tunatarajia
kufikisha tani 1,080 kwa sababu eneo lililopandwa mkonge limeongezeka,”
alisema.
Alisema moja ya changamoto inayowasumbua
ni tabia ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba yenye mkonge
mchanga hali ambayo alisema inaua miche hiyo michanga.
Aliitaja changamoto nyigine kuwa ni
ukosefu wa maji ya uhakika, hali ambayo inawafanya washindwe kuzalisha
singa za katani ambazo ni safi.
Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake
mkoani Kilimanjaro kwa kutembelea wilaya ya Mwanga ambako atazungumza na
watumishi na kisha ataenda kijiji cha Kirya, Nyumba ya Mungu kukagua
mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe.
No comments:
Post a Comment