Saturday, July 20, 2019

KUNAMBI ATUNUKIWA CHETI NA SHIRIKA LA MACHINGA NCHINI

Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi akizungumza na viongozi wa Shirika la Umoja wa Machinga Tanzania walipomtembelea Ofisini kwake ambapo pia walimpatia cheti cha shukrani kwa mchango wake kwa Machinga

 Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Shirika la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA) walipomtembelea ofisini kwake n kumkabidhi Cheti cha Shukrani kwa kutambua mchango wake kwa machinga

………………

Na.Alex Sonna,Dodoma

SHIRIKA la umoja wa Machinga Tanzania limetakiwa kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Mafuguli kutaka Machinga wafanye shughuli zao pasipo kusumbuliwa na mamlaka nyingine.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alipokuwa akiongea na kamati tendaji ya Shirika la Umoja wa Machinga Tanzania walipomtembelea ofisini kwake kumkabidhi cheti cha shukrani leo.

Kunambi alisema “ndugu zangu, tunawajibu wa kumsaidia mhe Rais kama wadau. Mhe Rais amefanya jitihada kubwa katika kuhakikisha machinga wa nchi hii wanafanya shughuli zao katika mazingira mazuri.

Tumeona utaratibu wake wa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo. Vitambulisho hivi vimekuwa msaada mkubwa kwa wafanyabiashara wadogo” alisema Kunambi.

Katika kuhakikisha Machinga wanafanya kazi zao vizuri, Mkurugenzi huyo alisema kuwa Jiji la Dodoma linataka kufanya Machinga wa kisasa. Machinga wanaofanya kazi zao vizuri kwa kuzingatia taratibu.

Aidha, aliwataka kufanya shughuli zao na kukua kimtaji. “Lazima tuwe na mpango wa kufanya mabadiliko kutoka Machinga kwenda kuwa wafanyabiashara. Hata Mbuyu ulianza kama mchicha” alisema Kunambi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirika la Umoja wa Machinga Tanzania, Ernest Masanja alisema kuwa umoja huo umeamua kumpatia cheti hicho kumshukuru Mkurugeni wa Jiji la Dodoma kutokana na ushirikiano ambao amekuwa akiutoa kwa Machinga katika kutekeleza majukumu yao.

Jiji la Dodoma ni miongoni mwa Halmashauri ambazo zimemaliza kuuza vitambulisho vyote walivyopewa kwa ajili ya kuwauzia wafanyabiashara wadogo.

Vitambulisho 15,173 vya wajasiliamali vimeshauzwa kwa wafanyabiashara kwa bei ya shilingi 20,000 kwa kila kimoja.

Rais John Magufuli aliamua kutoa vitambulisho na kuagiza mamlaka zinazohusika kuwa vitambulisho hivyo ni maalumu kwa wafanyabiashara ambao mtaji wao hauzidi Shilingi milioni nne (4) ili viwasaidie kuzitambulisha biashara zao.

Aidha, aliagiza kuwa wafanyabiashara watakaogawiwa vitambulisho hivyo wasisumbuliwe na mtu yeyote wakati wa kufanya shughuli zao.

Lengo ni kuwafanya wafanyabiashara wadogo kutambuliwa rasmi na kutobughudhiwa wanapofanya biashara zao za halali

No comments:

Post a Comment