MAKAMU WA PILI WA RAIS AFUNGUA TAMASHA 24 LA UTAMADUNI WA MZANZIBARI
Na Mwashungi Tahir,Maelezo
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Idi aliwataka vijana kuacha kuvutika na desturi za kigeni kwa
kuacha mila zao kwani kunaweza kusababishia ukiukwaji wa maadili kwa
Taifa la Wazanzibar.
Wito huo aliutoa huko katika Uwanja wa
Kumbu Kumbuwa Mapinduzi Square wakati alipokuwa akifungua Tamasha la
24 la Utamaduni wa Mzanzibar na kuwataka vijana waendeleze silka ,
tamaduni na mila za Kizanzibar ili jamii isipotee.
Alisema Vijana hawafuati mfumo halisi wa
maisha uliowakuza na hatimaye wamekuwa wahanga wa kuiga, kukumbatia na
kufuata tamaduni ambazo kimfumo haziendani na mazingira pamoja na
mfumo mzima wa maisha ya Wazanzibar.
Hivyo alisema wakati umewadia kuacha
utamaduni wa kigeni na kila siku tujivunie mambo ya Wazanzibar na kuwa
na mikakati mbali mbali itayosaidia kutoa elimu juu ya umuhimu wa kuenzi
kulinda na kuendeleza utamaduni wa Zanzibar.
Pia alieleza kwamba tukiendelea
kuadhimisha tamasha hili jamii ina wajibu wa kujiuliza na kupata jibu la
pamoja kwa kiasi kipi matamasha haya yananandaliwa katika visiwa vya
Unguja na Pemba na kuweza kubeba dhima na kusaidia ukuzaji na
uendelezaji wa mfumo wa utamaduni na sanaa katika jamii ya Zanzibar.
Vile vile alikemea matendo maovu ambayo
yanakosa uadilifu na kusababisha kuzaa chuki , mifarakano, visasi baina
ya familia na kuhatarisha mshikamano wa kijamii ambao husababisha
uvunjifu na amani, kutia aibu Taifa na watu wake .
Aliiomba jamii kuiunga mkono juhudi
zinazochukuliwa na Serikali katika vitendo vua udhalilishaji kwa kuacha
muhali au kuoneana haya jamii ijitokeze kutoa ushahidi katika vyombo vya
sheria hatimae sheria ichukuwe mkondo wake tukishirikiana kwa pamoja
tunaweza na kuondosha madawa ya kulevya ili tupate vijana walio bora
katika nguvu kazi.
“naomba vijana wajiepushe na madawa ya
kulevya ili Taifa lipate vijana walio imara na kupatikana Taifa lililo
bora”,alisema Balozi Seif.
Nae Waziri wa Vijana , Utamaduni, Sanaa
na Michezo Ali Abeid Karume alisema Tamasha la Mzanzibar tutalienzi kwa
lengo la kukuza mila silka na utamaduni ili jamii waweze kujua mambo ya
visiwa hivi na kizazi kiendelee kujua mambo ya nchi yao yakiwemo mambo
ya asili .
Alisema tamasha hili mwaka ujao
linatimiza miaka 25 ambalo litakuwa linaingia robo karne hivyo amewataka
wananchi kutarajia tamasha kuwa kubwa zaidi .
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub
Mohamed Mahmoud alitoa rai kwa Wizara ya Vijana , Utamaduni , Sanaa na
Michezo kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ianze
mitaala ili watoto waanze wakiwa wadogo kufundishwa mambo ya utamaduni
ili usipoitee.
Alisema dhamira kubwa ya tamasha hili ni kutunza utamaduni , utu mila na silka za kizanzibar .
Kauli mbiu ya tamasha hili ni”Utamaduni ni Ngao na ustawi wa jamii yetu” .
No comments:
Post a Comment