*****************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemsimamisha kazi Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Same, Mussa Msangi kwa
kosa la kumdanganya kuhusu mradi wa maji aliouzindua leo katika kata ya
Hedaru.
Amechukua uamuzi huo leo jioni
(Ijumaa, Julai 19, 2019) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa
Hedaru mara baada ya kuzindua mradi wa maji wa Lengeni-Hedaru, wilayani
Same.
Waziri Mkuu alibaini kuwepo
kwa tatizo wananchi walipoanza kuzomea wakati zikitolewa salaam za
utambulisho kwa viongozi alioambatana nao. Kabla hajahutubia, aliamua
kumuita Mhandisi huyo aelezee ukweli wa madai ya wananchi kwamba maji
yametoka leo kutokana na ujio wake.
“Eleza ni kwa nini
nilipofungua maji, hayakuwa na presha ya kutosha na wewe umesema
upatikanaji wa maji umefikia zaidi ya asilimia 80?”
Alipoulizwa kwa mwezi
wanakusanya kiasi gani cha fedha kutokana na mauzo ya maji hayo,
Mhandisi Msangi alijibu kwa mwaka uliopita walikusanya sh. milioni saba
tu.
“Haiwezekani kama maji
yanatoka, wenye KAMATI wapate shilingi milioni saba. Ni ama maji
hayatoki au wanakusanya hela na wanazila.”
Alipoambiwa aelezee utendaji
wa mradi huo wa maji na kama alikuwa akiufuatilia, alishindwa kutoa
maelezo kamili, akidai kuwa leo maji yanatoka kidogo kwa sababu kuna
hali ya mawingu. “Mbona kule ndani ulisema zile betri zinasaidia kuvuta
maji na kubalance upatikanaji wa maji wakati hakuna jua la kutosha?”
alihoji Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu aliamua kumuita
mwenyekiti wa Jumuiya ya watumiaji maji au Kiongozi mwingine yeyote aje
atoe maelezo, lakini wote hawakuwepo kwenye mkutano huo. Ndipo akachukua
uamuzi wa kuzivunja jumuiya hizo.
“Jumuiya zote za
maji nazivunja kuanzia leo, na wahusika wote watafutwe na Jeshi la
Polisi. Haiwezekani nipewe kazi ya kuzindua mradi ambao hauna maji,”
alisema Waziri Mkuu.
“Katibu Tawala wa Mkoa lete
wakaguzi wa mahesabu kwenye huu mradi, pia leta Mhandisi mwingine
asimamie huu mradi. Huyu arudishwe kwa Waziri wake,” alisema.
Waziri Mkuu pia alimwagiza Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Awesu abaki Hedaru na afuatilie utendaji wa mradi huo kisha ampe taarifa.
Wakati akimaliza kutoa maagizo
hayo, Katibu wa Jumuiya ya watumiaji maji Hedaru-Masasi (HEWAUA), Bw.
Francis Kazen Kiondo aliletwa akiwa chini ya ulinzi wa polisi, lakini
Waziri Mkuu alielekeza apelekwe kituoni akatoe maelezo.
Taarifa zilizothibitishwa
zimebainisha kuwa Kata ya Hedaru inazo Jumuiya tatu za watumiaji maji
ambao ni Hedaru-Masasi, Lung wana na Mradi wa Kati. Wakazi wa Hedaru
wanakadiriwa kufikia 20,000.
Ilibainika kwamba wiki
iliyopita, Mwenyekiti wa Hedaru-Masasi, Bw. Clement Ngoka aliamua
kujiuzulu nafasi hiyo kwa sababu ya upinzani aliokuwa akipata kwa
viongozi wenzake ambao pia wanadaiwa kuwaunganishia maji baadhi ya watu
hadi majumbani kwao na fedha zilizolipwa hazijulikani zilipoenda.
Awamu ya pili ya mradi wa maji
alioenda kuuzindua Waziri Mkuu, inahusisha ujenzi wa chanzo cha maji
katika korongo la mto Rangeni ambao ulikamilika Desemba 2018. Chanzo
hicho cha mtiririko, kilitarajiwa kuzalisha lita 750,000 kwa siku ili
kusaidia maji yanayozalishwa kwenye visima ambayo yana ujazo wa lita
7,500 kwa saa.
No comments:
Post a Comment