Rais Magufuli, Wafanyabiashara Wajadili Fursa na Changamoto za Biashara Nchini
Adelina JohnBosco, MAELEZO Dodoma
Rais John Pombe Magufuli amekutana na
wawakilishi wa wafanyabiashara nchini leo Ikulu Jijini Dar es salaam ili
kujadili changamoto zinazowakabili wafanyabiashara na jinsi ya
kuzitatua kwa ajili ya kukuza uchumi kupitia sekta binafsi nchini.
Licha ya jitihada zinazoendelea kuleta
uboreshaji katika sekta ya biashara, Rais ametaja uwepo wa changamoto
mbalimbali kwa pande wa Serikali na wafanyabiashara wenyewe ambazo
zimekuwa ni kikwazo katika kufanya biashara nchini.
Rais Magufuli amebainisha vikwazo
vinavyosababishwa na wafanyabiashara kuwa ni pamoja na ukwepaji kodi
unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara na vitendo vya rushwa kuwa ni
miongoni mwa changamoto zinazozuia uboreshaji wa sekta ya biashara
nchini.
Amesema kuna kampuni 17,446 zinakwepa
kodi kwa njia ya mauzo hewa ya biashara za ndani na nje, manunuzi hewa
kutoka makampuni hewa na kuagiza kampuni hizo kuchunguzwa zaidi na
zikithibitika kukwepa kodi zitalazimika kulipa kodi hiyo katika kipindi
cha siku 30 kuanzia sasa.
”Baadhi yenu sio waaminifu mnakwepa kodi,
mnatoa rushwa na wengine mmekuwa mkifanya kazi za udalali hasa kwenye
biashara ya sukari, mafuta ya kula na korosho” ameeleza Rais Magufuli
Changamoto nyingine kutoka kwa
wafanyabiashara ni kuhujumu uchumi kwa kutokuwa wawazi katika mahesabu
yao kwa kuwasilisha vielelezo tofauti vya taarifa ya fedha zinazopelekwa
benki na TRA.
Aidha, amewaonya wafanyabiashara
wanaobadilisha matumizi ya viwanda yaliyokusudiwa awali wakati
yakisajiliwa na kuanzisha biashara nyingine pasipo kufuata utaratibu.
Upande wa Serikali, Rais Magufuli
amebainisha changamoto mbalimbali ambazo ni kikwazo kwa biashara nchini
kuwa ni pamoja na wingi wa taasisi za udhibiti kama vile TRA, OSHA, TBS,
TFDA, Ofisi ya Mkemia Mkuuu, Tume ya Ushindani, EWURA, na SUMATRA
ambazo husababisha mwingiliano kimajukumu na kutoza tozo mbalimbali
zinazofanana hivyo kudhoofisha ukuaji wa biashara nchini.
Ametaja vitendo vya rushwa kwa baadhi ya
watumishi wachache wa Serikali wasio waadilifu kuwa ni miongoni mwa
changamoto inayorudisha nyuma jitihada za wafanyabiashara hasa maeneo ya
vizuizi barabarani, bandarini, na TRA.
Katika kuhakikisha changamoto hizi
zinatatuliwa, Rais amebainisha mikakati ya Serikali iliyoweka ikiwa ni
pamoja na kuandaa kitabu cha mwomgozo na kwamba mapendekezo mbalimbali
yameanza kutekelezwa kwa lengo la kuboresha mazingira ya biasha nchini.
”Sasa Brela inatumia utaratibu mpya wa
kusajili biashara kwa njia ya mtandao, kufuta baadhi ya ada na tozo
zilizokuwa zikitozwa na taasisi za OSHA na Zima moto kabla ya kuanzisha
biashara,” amesisitiza Rais Magufuli.
Aidha amezitaka mamlaka husika katika
Serikali kuweka mikakati thabiti ya kuwaendeleza wafanyabiashara wadogo
na wakati kama ilivyofanyika kwa wafanyabiashara wakubwa.
”Wafanyabiashara wadogo na wakati ndiyo
kitovu cha kukuza uchumi katika nchi, hivyo nashauri waendelezwe kama
ambavyo tumeshaanza kwa kutoa vitambulisho kwa wajasiriamali wadogo
nchini”, alisisitiza Rsi Magufuli.
Kwa upande mwingine, Rais amezionya
taasisi za kifedha kutokana na kuwa na mitaji midogo huku zikiweka
masharti magumu na kutoza riba kubwa ikiwemo kuendesha shughuli zake
zaidi mijini kuliko vijijini.
”Serikali kupitia Benki Kuu imekuwa
ikikopa fedha nyingi kwenye taasisi za kimataifa ikiwemo benki ya dunia
kwa ajili ya kutoa dhamana na kuwakopesha wajasiriamali wa hapa nchini,
lakini sina hakika kama fedha hizo zinawafikia walengwa,” amehoji Rais
Magufuli.
Rais amewaonya mawakala wa Shirika la
Viwango Tanzania (TBS) nje ya nchi wanaowasababishia hasara
wafanyabiashara kwa kuidhinisha bidhaa ambazo zinagundulika kuwa hazina
viwango zinapokaguliwa baada ya kuingizwa nchini.
Aidha ameziagiza mamlaka husika kuangalia
uwezekeno wa kuunganisha baadhi ya mifuko inayosimamia sekta ya
biashara ili kuiimarisha na kupunguza gharama za uendeshaji huku
akizitaka mamlaka zinazosimamia sekta ya biashara ikiwemo wizara, idara,
wakala wa Serikali kuhakikisha changamoto hizo zinafanyiwa kazi mara
moja ifikapo mwezi Julai mwaka huu, kwa kuzingatia mapendekezo yote
yaliyomo katika kitabu cha mwongozo (Blue Print).
Hata hivyo, rais ametoa pongezi kwa wafanyabiashara halali wanaofuata taratibu elekezi ikiwemo kulipa kodi kwa wakati.
Mkutano huu ni mwendelezo wa mikutano
inayofanywa na Rais kwa kuyahusisha makundi mbalimbali ikiwemo viongozi
wa dini, wachimbaji wa madini, wazee na watendaji Serikalini lengo
likiwa ni kujadiliana na kuweka mikakati itakayosaidia kukua kwa uchumi
kwa maslahi ya Taifa.
No comments:
Post a Comment