Serikali yakabidhi Mfumo wa Usimamizi wa Mashauri Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Clement
Mashamba, akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari( hawapo pichani)
kabla ya kukabidhiwa Mfumo wa Usimamazi wa Mashauri uliotengenezwa na
Wakala ya Serikali Mtandao (e GA), Makabidhiano ambayo yalifanyika leo
Ijuma, Juni 7,2019 Jijini Dar es Salaam, Kulia ni Mkurugenzi wa Ubora
na Udhibiti Mashauri kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na kushoto
ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma za TEHAMA wa Wakala ya Serikali
Mtandao, Injinia Benedict Ndomba.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Clement
Mashamba(Kulia), akipokea rasmi Mfumo wa Usimamazi wa Mashauri kutoka
kwa Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma za TEHAMA wa Wakala ya Serikali
Mtandao, Injinia Benedict Ndomba(Kushoto) Makabidhiano hayo yalifanyika
leo Ijuma, Juni 7,2019 Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma za
TEHAMA wa Wakala ya Serikali Mtandao, Injinia Benedict Ndomba (wa kwanza
kushoto) akitoa maelezo kuhusu ufanyaji kazi wa Mfumo wa Usimamazi wa
Mashauri uliotengenezwa na Wakala ya Serikali Mtandao (e GA) mbele ya
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Clement Mashamba( wa pili kushoto) katika
makabidhiano ya Mfumo huo mapema Leo Jijini Dar es Salaam.
Mfumo wa Usimamazi wa Mashauri uliokabidhiwa na Wakala ya Serikali Mtandao mapema leo kama unavyoonekana kwenye Picha.
(Picha na MAELEZO).
……………………..
Na.Paschal Dotto-MAELEZO.
Serikali Kupitia Wakala ya Mtandao (e GA)
imekabidhi rasmi Mfumo wa Taarifa wa Usimamizi Mashauri, kwa Ofisi ya
Wakili Mkuu wa Serikali ili kuiwezesha Ofisi hiyo Kutekeleza majukumu
yake kwa ufanisi Mkubwa.
Akizungumza ya Waandishi wa Habari katika
makabidhiano kati ya Wakala ya Serikali ya Mtandao na Ofisi ya Wakili
Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi Wa Usimamizi wa Huduma za TEHAMA wa Wakala
ya Serikali, Injinia, Benedict Ndomba, amesema kuwa Ofisi yake inatumia
wataalam wake wa TEHAMA kutengeneza mifumo inayorahisisha kufanya kazi
katika Taasisi mbalimbali nchini.
Injinia Ndomba, alisema kuwa serikali ya
Awamu ya Tano inalo kusudi kubwa la kutekeleza ahadi zake kama utoaji
huduma nzuri kwa wananchi ikiwemo hiyo ya utengenezaji mifumo ya huduma
kwa ajili ya kero za wananchi.
“Serikali hii ya Awamu ya Tano, ina
hazina kubwa ya wataalam wa TEHAMA, ambapo kielelezo kimojawapo ni kuwa
mfumo huu umebuniwa, umesanifiwa na kutengenezwa na Watumishi wa Umma na
tumekubaliana na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuwa Mfumo huu
utekelezwe kwa awamu mbili ili kuweza kukidhi mahitaji ya wadau wote”,
Injinia Ndomba alisema.
Katika awamu ya Kwanza ya Utengenezaji
Mfumo huo, Ndomba alisema wametengeneza Moduli itakayoisaidia Ofisi ya
Wakili Mkuu wa Serikali kutekeleza majukumu yao hasa ya ndani kwenye
masuala ya Usimamizi Mashauri, ambapo pia itakuwa ni nyenzo muhimu wa
utekelezaji majukumu kwa haraka.
Naye, Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt.
Clement Mashamba ameipongeza Wakala ya Mtandao wa Serikali (e GA) kwa
kutengeneza mfumo huo kwa mahitaji ya ofisi ya Wakili wa Serikali na
kudai kuwa watakuwa wanatekeleza majukumu kwa haraka na kwa ufanisi
zaidi katika kutatua kero za wananchi.
“Ofisi yangu itaendelea kushirikiana na
Wakala ya Serikali ya Mtandao ili kuhakikisha awamu zote za utengenezaji
wa mfumo huu zinatekelezwa kwa wakati na kwa ubora unaostahili, lakini
pia Ofisi yangu inatambua Mchango huu mkubwa kwa kazi zetu ya kisheria,”
Dkt. Mashamba.
Aidha Dkt. Mashamba alisema kuwa mfumo
huo utakuwa ni muhimu katika kutatua kero za wananchi, hususani
Usimamizi wa majalada ya Mashauri; Usajili wa Mashauri; Upangaji wa
Mashauri yanayoshughulikiwa; Ufutiliaji wa Maendeleo ya Mashauri; Huduma
zingine ni Usimamizi wa Ratiba ya Mashauri; Utoaji wa Taarifa; Uhakiki
wa Mwenendo wa Mashauri na Uhamishaji wa Taarifa na Takwimu.
Dkt. Mashamba alieleza kuwa mfumo huo una
umuhimu mkubwa kwani unaweza kutumiwa na idara mbalimbali za Serikali
na unapatikana mahali pamoja kwa hiyo ni mfumo ambao Ofisi ya Wakili
Mkuu wa Serikali itaweza kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
No comments:
Post a Comment