Waziri wa Maliasili na Utalii
Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla akimkabidhi Bendera ya Taifa kiongozi wa
timu ya waendesha baiskeli 28, Bw. Paul Pulson wakati wa kuwaaga
waendesha baiskeli hao kutoka nchi mbalimbali kupitia kampeni ya Geita
Gold Mining Kilimanjaro Challenge 2019 yenye lengo la kuendeleza
mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi na kuchangisha kwa ajili ya watoto
yatima na wanaoishi na VVU, leo mkoani Kilimanjaro.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.
Dkt. Hamisi Kigwangalla akimkabidhi Bendera ya Taifa kiongozi wa timu
ya wapanda mlima Kilimanjaro 32 Bw. Moses Rusasa wakati wa kuwaaga
wapanda mlima hao kutoka nchi mbalimbali kupitia kampeni ya Geita Gold
Mining Kilimanjaro Challenge 2019 yenye lengo la kuendeleza mapambano
dhidi ya VVU na Ukimwi, leo mkoani Kilimanjaro.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.
Dkt. Hamisi Kigwangalla akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa
Mkoa wa Kilimanjaro wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe.
Anna Mgwira wakati wa kuwaaga waendesha baiskeli na wapanda mlima na
waendesha baiskeli 60 wanaoshiriki kampeni ya Geita Gold Mining
Kilimanjaro Challenge 2019 yenye lengo la kuendeleza mapambano dhidi ya
VVU na Ukimwi, leo mkoani Kilimanjaro.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.
Hamisi Kigwangalla akiwa katika picha ya pamoja na waendesha baiskeli
wanaopanda mlima Kilimanjaro kupitia kampeni ya Geita Gold Mining
Kilimanjaro Challenge 2019 yenye lengo la kuendeleza mapambano dhidi ya
VVU na Ukimwi, leo kwenye lango la Machame wilayani Hai , Kilimanjaro
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.
Hamisi Kigwangalla akiwaongoza wapanda mlima Kilimanjaro 32 walioanza
safari ya kupanda mlima Kilimanjaro kwa siku 7 kupitia kampeni ya Geita
Gold Mining Kilimanjaro Challenge 2019. Kampeni hiyo ina lengo la
kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi, leo mkoani Kilimanjaro.
Waendesha baiskeli wakijiandaa
kupanda mlima Kilimanjaro kuelekea kilele cha Uhuru kiupitia Kampeni ya
Geita Gold Mining Kilimanjaro Challenge mwaka 2019 yenye lengo la
kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi, leo mkoani Kilimanjaro.
***************************
WMU – Arusha
15/6/2019.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.
Hamisi Kigwangalla amepongeza juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali
kutangaza utalii na uanzishwaji wa kampeni zinazohamasisha mapambano
dhidi ya VVU na Ukimwi kupitia vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini.
Dkt. Kigwangalla ametoa pongezi
hizo leo mkoani Kilimanjaro wakati wa hafla fupi ya kuwaaga Wapanda
mlima 32 na Waendesha Baskeli 28 kutoka nchi mbalimbali walioshiriki
kupanda mlima Kilimanjaro kupitia Kampeni ya Geita Gold Mining Kilimanjaro Challenge 2019 inayolenga kukusanya fedha za kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi na kuwasaidia watoto yatima.
Amesema kampeni hiyo itawawezesha
wapanda mlima hao kufika kilele cha Mlima Kilimanjaro (Uhuru Peak) na
waendesha Baiskeli kuzunguka mlima Kilimanjaro takribani Kilometa 500
ikiwa ni sehemu ya kushiriki katika changamoto ya kuunga mkono juhudi za
Serikali katika mwitikio dhidi ya VVU na Ukimwi.
“Ugonjwa wa UKIMWI umeendelea kuwa
suala la kipaumbele kwa Serikali, athari zake zinagusa sekta zote
ikiwemo wizara ninayoiongoza ya Maliasili na Utalii, bila shaka sote
tumeona jitihada mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa kupambana na janga
hili” Amesisitiza Dkt. Kigwangalla
Amesema kuwa pamoja na takwimu
kuonesha kupungua kwa maambukizo mapya bado jitihada zaidi zinahitajika
ili kuutokomeza ugonjwa huo akifafanua kwamba kila mwananchi ni lazima
awe macho kuhakikisha anashiriki kutokomeza ongezeko la maambukizo
mapya.
Aidha, amefafanua kuwa programu
hiyo imetoa mchango mkubwa katika kuongeza idadi ya watalii
wanaotembelea Mlima Kilimanjaro wakati na baada ya msimu wa Kill
Challenge kumalizika kwani wageni kutoka ndani nan je ya Tanzania
huwataarifu wenzao pindi wanaporudi makwao ili waweze kuja kupanda mlima
Kilimanjaro.
“Huu ni uthibitisho tosha kwamba
programu hii siyo tu inachangia kudhibiti Ukimwi bali pia inachangia
kukuza uchumi wa nchi yetu kupitia mapato ya utalii ya Mlima
Kilimanjaro” Amesema.
Dkt. Kigwangalla ameipongeza
kampuni ya GGL na wawekezaji wote ambao wamekua wakijitoa kuchangia
ustawi wa jamii ya watanzania akitoa wito kwa makampuni mengine
kuendelea kujitolea kuchangia program hiyo pamoja na Mfuko wa hisani wa
UKIMWI ulioanzishwa na Serikali wa AIDS Trust Fund (ATF).
Amesema hatua ya GGL kushirikiana
na Serikali kupitia TACAIDS ni ya kupigiwa mfano na kwamba inaonesha
namna sekta binafsi hususani wafanyabiashara wanavyoendelea kujitokeza
kuchangia mwaka hadi mwaka.
Ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa program hiyo takribani shilingi bilioni 13 za Kitanzania zimekusanywa kupitia jitihada hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
TACAIDS, Dk. Leonard Maboko amewapongeza wadau wote kwa kuendelea
kuchangia kwenye Mfuko wa kupambana na Ukimwi.
Amesema kuwa mujibu wa takwimu
zilizopo TACAIDS ugonjwa wa UKIMWI bado ni tatizo nchini kutokana na
kuwepo kwa maambukizi mapya ya watu 200 kila siku.
Amesema kazi kubwa inayofanywa na
TACAIDS kwa sasa ni kuendeleza kampeni ya kuzuia maambukizi yasitokee
ili kuendana na makubaliano ya umoja wa Mataifa ya kufikia maambukizo 0
ifikapo mwaka 2030.
“ Bado tunayo kazi kubwa sana ya
kuzuia maambukizi haya, watu 200 kwa siku kuambukizwa VVU ni wengi,
tunaendelea kujitahidi na kufanya kazi kubwa ya kuelimisha wananchi na
kama ingekua ni ajali ingekua ni watu 200 wanaumia kila siku,
tunazungumza hizi takwimu kujikumbusha kwamba Ukimwi bado upo”
Amesisitiza Dkt. Maboko.
Ameeleza kuwa kiwango cha
maambukizi hayo kinazidi kuongezeka miongoni mwa vijana wenye umri kati
ya miaka 15 hadi 24 akifafanua kwamba kwamba kati ya watu 200
waliopata maambukizi , watu 80 ni vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24.
“ Kwa ujumla maambukizi mapya
yanazidi kushuka isipokuwa kwa vijana yanazidi kupanda juu, sisi kama
Tume kwa kushirikiana na wadau tunaliona na tunaendelea kulifanyia kazi
kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kunusuru kizazi cha vijana
ambao ndilo tegemeo la Taifa na viongozi wa baadae” Amesisitiza Dk.
Maboko.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Masuala ya UKIMWI Mhe. Oscar Mukasa amesema kuwa kazi yao kama
Kamati ni kushirikiana na wadau wote katika masuala ya Sera, Sheria na
usimamizi na kufafanua kuwa mfuko wa Ukimwi tangu kuanzishwa kwake
umekuwa na changamoto ya kupata fedha akiupongeza Mgodi wa Dhahabu wa
Geita (GGM) kwa kuendelea kuchangia fedha katika mfuko huo.
Amesema Bunge itaendelea kuishauri
Serikali kwa lengo la kupata vyanzo vingine vya mapato vya uhakika ili
Serikali iweze kushirikiana na wadau wa ndani wa Sekta binafsi kwa lengo
la kujitegemea.
Amesema tukio hilo la wapanda
mlima kuchangisha fedha linapeleka ujumbe kwa jamii kwamba kazi ya
kupambana na UKIMWI bado ni kubwa na endelevu hivyo jamii yote inapswa
kushiriki kikamilifu.
No comments:
Post a Comment