Waziri Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa akizungumza na wananchi, wakati wa futari ya pamoja na watoto
yatima kutoka kwenye vituo sita vya kulea watoto yatima vya jijini Dar
es Salaam, iliyofanyika katika viwanja vya Karimjee Mei 26.2019. (Picha
na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watoto yatima, kwenye
futari ya pamoja na watoto yatima kutoka kwenye vituo sita vya kulea
watoto yatima vya jijini Dar es Salaam, iliyofanyika katika viwanja vya
Karimjee Mei 26.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa akisalimiana na Mkurugenzi wa Chocolate Princess na mwandaaji
wa kipindi cha televisheni maarufu cha The Mboni Talk Show, Bi. Mboni
Masimba, wakati wa futari ya pamoja na watoto yatima kutoka kwenye
vituo sita vya kulea watoto yatima vya jijini Dar es Salaam,
iliyofanyika katika viwanja vya Karimjee Mei 26.2019. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu).
.......................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewaonya baadhi ya wamiliki na waendeshaji wa makao ya watoto
wasiofuata taratibu za usajili wa watoto, wanaowatumia watoto kama
mitaji au kwa maslahi binafsi na wanaoendesha makao hayo kwa minajili ya
kidini na kikabila.
Amewataka pia wamiliki hao waache
mara moja kuwalea watoto hao katika maadili yasiyofaa na yasiyo ya
Kitanzania na kwamba maofisa ustawi wa jamii wahusike moja kwa moja
katika usajili wa mtoto ili kuhakikisha kuwa ni watoto wanaostahili tu
kuwekwa kwenye makao ndiyo wanasajiliwa.
Alikuwa akizungumza jana usiku
(Jumapili, Mei 26, 2019) kwenye Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es
Salaam alikokuwa mgeni wa heshima wakati wa futari ya pamoja na watoto
yatima kutoka kwenye vituo sita vya kulea watoto yatima vya jijini humo.
“Nitoe rai kwamba watu mmoja
mmoja, taasisi na makao wazingatie baadhi ya taratibu za msingi za
uendeshaji wa makao kama vile mtoto kukuzwa katika mazingira ya familia,
kuzingatia misingi ya kitaifa badala ya misingi ya tamaduni za kigeni.
“Mtoto kukuzwa kwa kuzingatia
maslahi bora ya mtoto; kuzingatia umuhimu wa kuwa na mwendelezo katika
dini ya mtoto na utamuduni wake; kutotenganisha watoto na ndugu na
kuhakikisha watoto wote wanapata huduma stahiki, kulindwa dhidi ya
vitendo vya ukatili na unyanyasaji; na kutunzwa na kuendelezwa hadi
kufikia kimo cha utimilifu wao,” alisema.
Waziri Mkuu alitumia hadhara hiyo
pia kutoa maelekezo mahsusi kwa waendeshaji wa makao pamoja na
wasimamizi wa sheria na taratibu za uendeshaji wa makao ya watoto
yatima.
“Afisa Ustawi wa Jamii katika
eneo yanakoanzishwa makao, ahusike moja kwa moja katika usajili wa mtoto
ili kuhakikisha kuwa ni watoto wanaostahili tu kuwekwa kwenye makao
ndio wanasajiliwa.
“Taasisi na makao zihakikishe
kuwa kila mtoto anawekewa mpango maalumu wa kuondoka kwenye makao na
namna ya kumuunganisha mtoto huyo na familia yake.
“Wamiliki wa taasisi na makao,
waruhusuni maafisa ustawi wa jamii na maafisa wengine wa Serikali
wafanye ukaguzi kwa mujibu wa sheria na wekeni utaratibu wa kuandaa
taarifa za kila mwezi za watoto na taarifa ya mwaka wa fedha,” alisema
Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu pia alionya dhidi ya
wale “wanaowabadili watoto dini kinyume cha sheria; wanaofanya vitendo
vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto; wasiowaruhusu watendaji wa
Serikali kufanya ufuatiliaji na usimamizi; wasioandaa mpango wa
kuwaunganisha watoto na familia zao na hivyo, kusababisha watoto kukaa
kwa muda mrefu kwenye makao na wale wote wanaondesha makao bila kuwa na
leseni ya uendeshaji.”
Alisema Serikali haitowafumbia
macho watu wa namna hiyo, na mara tu watakapogundulika kuanzisha au
kuendesha makao bila kufuata taratibu, hatua kali za kisheria
zitachukuliwa dhidi yao.
Alisema tangu mwaka 2016 hadi
sasa, kuna jumla ya watoto 24,067 wanaolelewa katika makao
yaliyosajiliwa nchini yakiwemo makao 140 yanayoendeshwa na kumilikiwa na
watu au taasisi binafsi. Kati yao wavulana ni 11,925 na wasichana ni
12,142.
Alisema Serikali kupitia Wizara
ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaratibu upatikanaji
wa huduma za msingi kwenye makao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Baadhi ya huduma hizo ni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa Bima ya Afya
kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi. “Hadi sasa, watoto 900
kutoka Dar es Salaam, Mbeya, Kilimanjaro na Arusha wamepatiwa kadi hizo
na zoezi hilo linaendelea,” alisema.
Waziri Mkuu alisema Serikali
itaendelea kusimamia na kufuatilia kwa karibu uendeshaji wa makao ya
watoto sambamba na kutoa elimu kuhusu malezi, makuzi, haki, ulinzi na
usalama wa mtoto kwa mujibu wa sheria zinazosimamia haki na ustawi wa
mtoto.
Mapema, akielezea azma ya kuandaa
futari hiyo, Mkurugenzi wa Chocolate Princess na mwandaaji wa kipindi
cha televisheni maarufu cha The Mboni Talk Show, Bi. Mboni Masimba
alisema jumla ya watoto yatima 325 walikuwa wamealikwa kushiriki futari
hiyo.
Watoto hao wanatoka vituo vya
Ijango Zaida Orphanage Centre kilichopo Sinza, Alzama Orphanage Centre
(Mbagala), Ashura Foundation (Vingunguti), Madina Orphanage Centre
(Tandale), Hiyari Orphanage Centre (Mbagala) na Hisani Orphanage Centre
(Mwasonga).
Futari hiyo iliandaliwa na Mboni
Masimba kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Asure Yetim Vafki,
United Bank of Africa (UBA), Junaco, Mo Dewji Foundation, Lake Oil,
ASAS, AZAM, Uncle K Catering, Zurii, Simply Special Decor na State Oil
na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwamo Balozi wa Uturuki nchini, Bw.
Ali Davutoğlu, Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Taifa, Sheikh Issa Othman,
masheikh, maimamu wa misikiti na viongozi wa taasisi zinazojihusisha na
malezi ya watoto yatima.
No comments:
Post a Comment