Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Ngailonga
Hasunga (Mb) akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya
Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2019/2020 Bungeni Jijini Dodoma, leo tarehe 17 Mei
2019. (Picha Zote Na Mathias Canal,
Wizara ya Kilimo)
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe na Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Kilimo Prof Siza Tumbo wakifatilia hotuba ya Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Ngailonga Hasunga (Mb) kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2019/2020 Bungeni Jijini Dodoma, leo tarehe 17 Mei 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Ngailonga Hasunga (Mb) akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2019/2020 Bungeni Jijini Dodoma, leo tarehe 17 Mei 2019.
1.0
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa
Spika,
naomba kutoa hoja kwamba, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo na Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji, Bunge lako Tukufu sasa lipokee na
kujadili taarifa ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa
mwaka wa fedha 2018/2019. Aidha, ninaliomba
Bunge lako Tukufu lipitishe Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara na
Taasisi zake kwa mwaka wa Fedha 2019/2020.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote
ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufikia siku ya leo tukiwa wazima
wa afya njema na kuendelea kuijalia nchi yetu amani na mshikamano na kujadili
bajeti hii inayolenga kusukuma mbele kasi ya maendeleo ya Sekta ya Kilimo na wakulima
kwa ujumla wao.
3. Mheshimiwa
Spika,
napenda kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuniteua kuwa Waziri wa Kilimo. Pia, niwashukuru
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais na Mheshimiwa Kassim Majaliwa
Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu kwa kazi kubwa wanayofanya kusukuma maendeleo ya
nchi hii, ikiwemo Sekta ya Kilimo. Napenda kuwaahidi kwamba nitafanya kazi ya
kuongoza Wizara ya Kilimo kwa uaminifu, juhudi na maarifa ili kuhakikisha kuwa
rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya maendeleo ya kilimo zinawafikia walengwa
ili kuongeza tija na kuinua kipato chao.
4. Mheshimiwa
Spika, nitumie fursa hii kumpongeza Waziri Mkuu, Mhe.
Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) kwa hotuba yake ambayo iligusa maeneo mengi ikiwemo Sekta
ya Kilimo. Aidha, nimpongeze tena Mhe. Waziri Mkuu kwa kuendelea kuwa mstari wa
mbele kuhamasisha na kusimamia kilimo pamoja na maendeleo ya Vyama vya Ushirika.
5. Mheshimiwa
Spika, napenda
kukupongeza wewe na Naibu Spika Mhe. Dkt. Tulia Ackson Mwansasu (Mb.) pamoja na
Wenyeviti wa Bunge kwa jinsi mnavyoliongoza Bunge kwa umahiri mkubwa.
Aidha, nitumie nafasi hii kuwapongeza Wabunge
wote kwa umahiri wao mkubwa katika mijadala inayoendelea katika Bunge hili la
Bajeti.
6. Mheshimiwa
Spika, nitumie fursa
hii pia kuwapongeza na kuwashukuru wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Kilimo Mifugo na Maji chini ya Uenyekiti wa Mhe. Mahmoud Mgimwa, Mbunge wa
Mufindi Kaskazini na Makamu Mwenyekiti Mhe. Dkt. Christine G. Ishengoma (Mb). Kamati
ilipata fursa ya kukutana na Wizara na kutembelea baadhi ya maeneo kuona
utekelezaji wa kazi za kilimo na kushauri namna ya kuimarisha utekelezaji wa
majukumu ya Wizara, Bodi na Taasisi zake. Naomba kulihakikishia Bunge lako
Tukufu kwamba, ushauri wao umezingatiwa na tutaendelea kushirikiana na Kamati
ili kuleta mageuzi ya kilimo nchini.
2.0
MWELEKEO WA SEKTA YA KILIMO
7. Mheshimiwa
Spika,
Serikali imepanga kubadilisha kilimo kutoka kuwa cha kujikimu na kuwa kilimo
cha kibiashara kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Aidha,
Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo umesisitizia mapinduzi ya viwanda na umeitambua
Sekta ya Kilimo kuwa mhimili imara kwa ajili ya upatikanaji wa malighafi za
viwanda. Miongozo hiyo ya Kitaifa,
pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 na Sera ya Kilimo ya mwaka
2013, inatekelezwa na Wizara kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo
Awamu ya Pili (ASDP II) ambayo inalenga kuleta mageuzi katika Sekta ya Kilimo.
Aidha, kwa kutambua umuhimu wa kuongeza mitaji, teknolojia na ubunifu, Sekta
Binafsi inashirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wa ASDP II.
8. Mheshimiwa
Spika, ASDP
II iliyozinduliwa rasmi tarehe 4 Juni, 2018 na Mheshimiwa Dkt. John Joseph
Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inalenga kubadilisha
maisha ya mkulima kwa kufanya mageuzi makubwa kwenye kilimo kwa kuzingatia
mazao ya kipaumbele kulingana na ikolojia za kilimo.
3.0
MCHANGO WA KILIMO KATIKA UCHUMI
9.
Mheshimiwa Spika, kilimo ni sekta kubwa na muhimu kwa maendeleo
kutokana na mchango wake katika uchumi. Katika mwaka 2017, sekta hiyo imetoa ajira
kwa Watanzania kwa asilimia 65.5, ikichangia takriban asilimia 28.7 ya Pato la
Taifa ambapo sekta ndogo ya mazao ilichangia asilimia 16.58. Vilevile, Sekta ya Kilimo inachangia asilimia
65 ya malighafi za viwanda. Takwimu zinaonesha kuwa katika robo ya kwanza ya
mwaka 2018, ukuaji wa Sekta ya Kilimo ulifikia asilimia 7.1. Ukuaji huo ulichangiwa
na jitihada za Serikali za kuhakikisha upatikanaji na matumizi ya pembejeo bora, hali nzuri ya mvua na
uboreshaji wa miundombinu ya uzalishaji.
3.1 Upatikanaji wa Chakula
10. Mheshimiwa
Spika,
upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2018/2019
ulifikia tani milioni 16.89 zikiwemo tani milioni 9.53 za mazao ya nafaka na
tani milioni 7.35 za mazao yasiyo nafaka. Kiwango hicho cha uzalishaji
kimeiwezesha nchi kujitosheleza kwa mahitaji yake ya chakula ya tani milioni
13.56 na hivyo kuwa na ziada ya tani milioni 3.32 za chakula kwa kiwango cha
utoshelevu cha asilimia 124. Niwahakikishie watanzania kwamba, tunacho chakula
cha kutosha nchini. Hata hivyo,
tuendelee kuweka akiba katika kaya zetu hadi tutakapovuna tena kwani inaonekana
kwamba huenda tusiwe na mavuno mazuri sana msimu huu kutokana na uhaba wa mvua
kwenye maeneo ya Kanda ya Ziwa, Kati na Kaskazini mwa nchi yetu. (Maelezo
ya kina yanapatikana uk.5 wa kitabu cha Hotuba ya bajeti).
3.2 Umwagiliaji
11. Mheshimiwa
Spika,
katika mwaka 2018/2019, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imekamilisha
mapitio ya Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002 ili kubaini
maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kwa kuzingatia Mipango Shirikishi
ya Maendeleo ya Rasilimali za Maji. Katika mpango huo, hekta 560,880 zimepangwa
kuendelezwa kwa lengo la kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 475,052
mwaka 2018/2019 hadi hekta 1,000,000 ifikapo mwaka 2035. (Maelezo ya kina yanapatikana
uk.6 wa kitabu cha Hotuba ya bajeti)
3.3 Maendeleo ya Ushirika
12. Mheshimiwa
Spika,
Wizara kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeendelea kuimarisha Sekta ya Ushirika
kwa kusimamia na kuhamasisha maendeleo yake. Vyama vya Ushirika vimeongezeka kutoka
vyama 10,990 Desemba 2017 hadi vyama 11,331 kufikia Desemba 2018. Vilevile, idadi
ya wanachama wa vyama vya ushirika imeongezeka kutoka 2,619,311 mwaka 2017 hadi
3,998,193 Februari, 2019 sawa na ongezeko la asilimia 53.
Hadi
Desemba 2018, mikopo yenye thamani ya Shilingi trilioni 1.3 imetolewa kwa
wanachama ikilinganishwa na Shilingi bilioni 902 iliyotolewa kufikia Desemba
2017.
Aidha, Akiba na Amana za wanachama katika
SACCOS zimefikia Shilingi bilioni 575 na hisa Shilingi bilioni 79. (Maelezo
ya kina yanapatikana uk.7 wa kitabu cha Hotuba ya bajeti)
4.0
UTEKELEZAJI WA MAENEO YA KIPAUMBELE KWA MWAKA 2018/2019
13.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2018/2019, Wizara imetekeleza
maeneo ya kipaumbele ya kuongeza tija kwa kuimarisha upatikanaji wa
pembejeo za kilimo, udhibiti wa visumbufu, matumizi ya zana bora za kilimo na
huduma za ugani; ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji; ujenzi wa miundombinu
ya kuhifadhi mazao ya kilimo na masoko; kufanya utafiti wa kilimo na kuzalisha
teknolojia kwa mazao ya mahindi, muhogo, ngano, michikichi, ufuta, alizeti,
pamba na mpunga.
14.
Mheshimiwa
Spika, maeneo mengine ya kipaumbele ni kuimarisha uzalishaji na
upatikanaji wa mbegu bora za mazao na kusambaza kwa wakulima; kuboresha maarifa
na ujuzi kwa watafiti; kuimarisha huduma za upimaji wa matabaka na ubora wa udongo
kuendana na mahitaji ya mazao ya kilimo ki-ikolojia; mafunzo na usambazaji
taarifa za kilimo na sayansi shirikishi; kusajili na kuandaa kanzidata ya
wakulima na kuimarisha ushirika. (masuala yote ya utekelezaji wa maeneo ya
kipaubele yapo kwa kina kwenye ukurasa 10-61
katika kitabu cha Hotuba ya bajeti)
15.
Mheshimiwa
Spika, ili kutekeleza vipaumbele hivyo, Shilingi bilioni 204.07 ziliidhinishwa na Bunge lako
Tukufu. Kati ya fedha hizo, Fungu 43 – Wizara ya Kilimo iliidhinishiwa Shilingi
bilioni 166.26 zikiwemo Shilingi bilioni
68.14 za matumizi ya kawaida na
Shilingi bilioni 98.12 za matumizi
ya maendeleo; Tume ya Taifa
ya Umwagiliaji - Fungu 05 iliidhinishiwa Shilingi bilioni 29.77 zikiwemo
Shilingi bilioni 3.95 za matumizi ya
kawaida na Shilingi bilioni 25.82
fedha za maendeleo; na Tume ya Maendeleo ya Ushirika - Fungu 24 iliidhinishiwa
Shilingi bilioni 8.05 zikiwa ni fedha
za matumizi ya kawaida.
4.1 Kuongeza Tija
katika Kilimo
Upatikanaji wa mbegu bora za mazao
16. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2018/2019, upatikanaji wa
mbegu bora umefikia tani 49,040.66. Kati ya kiasi hicho, tani 38,507.87
zimezalishwa hapa nchini, tani 8,361.46 zimeagizwa toka nje ya nchi na tani
2,171.33 ni bakaa ya msimu wa 2017/2018. Vilevile, miche 1,507 ya miwa, vipando 121,805
vya muhogo na vikonyo 520,000 vya viazi lishe vimezalishwa. Aidha, aina mpya 13
za mbegu bora zimeidhinishwa na zitaanza kuzalishwa msimu wa 2019/2020.
Upatikanaji na udhibiti wa ubora wa Mbolea
17. Mheshimiwa Spika, hadi Machi
2019, upatikanaji na usambazaji wa mbolea nchini ulikuwa tani 492,394
ikilinganishwa na mahitaji ya tani 514,138 katika msimu wa 2018/2019. Aidha, Wizara
kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imefanya
ukaguzi kwa wauzaji wa mbolea 1,350 na wafanyabiashara 496 wapya wa mbolea wamesajiliwa.
Upatikanaji
wa Viuatilifu na Udhibiti wa Visumbufu
18. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Wizara imenunua lita 296,000
na kilo 3,000 za viuatilifu vyenye thamani ya Shilingi bilioni tisa (9) kwa
ajili ya kukabiliana na milipuko ya visumbufu vya mazao. Hadi kufikia Machi 2019, ndege waharibifu wa nafaka
walidhibitiwa katika skimu za umwagiliaji za Kahe, Lekitatu na Misenyi kwa
mazao ya mpunga na mtama. Aidha, lita
119,000 kwa ajili ya kudhibiti Viwavijeshi Vamizi zimesambazwa katika Kanda ya
Ziwa, Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Magharibi, Kanda ya
Kaskazini na Kanda ya Mashariki na kutoa mafunzo kwa maafisa ugani na wakulima 350.
Zana
za Kilimo
19. Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha
kwamba wastani wa kitaifa wa matumizi ya zana bora za kilimo umeongezeka hadi
kufikia asilimia 20 kwa matrekta na asilimia 27 kwa wanyama kazi ikilinganishwa
na asilimia 14 ya matrekta na asilimia
24 ya wanyama kazi mwaka 2013. Kutokana na ongezeko hilo, matumizi ya jembe la
mkono yamepungua na kufikia asilimia 53 kwa mwaka 2018 ikilinganishwa na
asilimia 62 kwa mwaka 2013. Aidha, kupitia
Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) Wizara imendelea kutoa mikopo ya
pembejeo na zana za kilimo. Katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019, mikopo
33 yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.50
imetolewa.
4.2 Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Umwagiliaji
20. Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya
Maendeleo ya Umwagiliaji imeendelea kusimamia utekelezaji wa Mradi wa Skimu za Umwagiliaji za Wakulima Wadogo unaofadhiliwa
na Serikali ya Japan. Mradi umekarabati skimu za umwagiliaji 129 katika
Halmashauri 68 nchini pamoja na ununuzi wa mitambo ya ujenzi.
4.3 Utafiti
wa Kilimo na Uhaulishaji wa Teknolojia
21. Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2018/2019, Wizara kupitia TARI imegundua mbegu bora mpya aina nne (4) za
mahindi. Mbegu hizo zina uwezo wa kutoa mavuno kwa wastani wa tani 5.8 kwa
hekta kwenye mashamba ya wakulima katika ukanda wa chini na kati, zinahimili
ukame na zina ukinzani wa magonjwa ya majani ya mahindi na michirizi na ukungu.
Vilevile, kwa kushirikiana na kampuni binafsi, TARI imezalisha aina sita (6) ya
miche ya mbegu bora ya migomba na kugundua aina 62 za mbegu za mazao ya mikunde.
4.4 Maendeleo ya Mazao
22. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea
kuratibu utekelezaji wa mikakati ya maendeleo ya mazao mbalimbali kwa kuimarisha huduma za utafiti, upatikanaji
na utumiaji wa pembejeo na zana za kilimo, udhibiti wa visumbufu vya mazao,
huduma za ugani, uongezaji wa thamani na upatikanaji wa masoko. Aidha, Wizara
imeandaa mkakati wa miaka minne (2018/2019 – 2021/2022) wa kuendeleza zao la michikichi.
Mazao Makuu ya Asili ya Biashara
23. Mheshimiwa Spika, uzalishaji
wa mazao makuu ya biashara uliongezeka kutoka tani 901,641 msimu
wa 2016/2017 hadi tani 967,184 msimu wa 2017/2018 ikiwa ni ongezeko
la asilimia 7.2. Katika msimu wa
2018/2019, Wizara ililenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara hadi
kufikia tani 1,356,368 na hadi
kufikia Machi 2019, tani 667,631.77 sawa na asilimia 49.2 ya lengo zilikuwa zimezalishwa
na uzalishaji unaendelea.
24. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2017/2018,
uzalishaji wa mazao ya bustani ulikuwa tani milioni 5.33 na matarajio ya uzalishaji
kwa mwaka 2018/2019 ni tani milioni 5.96. Hadi Machi 2019, uzalishaji umefikia
tani milioni 4.36 sawa na asilimia 73.17 ya lengo na msimu wa uzalishaji
unaendelea.
4.5 Ujenzi wa Miundombinu ya Kuhifadhi Mazao ya Kilimo
na Masoko
Miundombinu
ya Kuhifadhi Mazao ya Kilimo
25. Mheshimiwa Spika, Wizara
kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) inaendelea kutekeleza
Mradi wa Kuongeza Uwezo wa Kuhifadhi Nafaka. Hadi
kufikia mwezi Machi 2019, asilimia 83 ya vifaa vilikuwa vimeingizwa nchini kwa ajili ya
ujenzi wa ghala katika vituo vya Makambako, Mbozi, Songea, Shinyanga na Dodoma.
Masoko ya Mazao ya Kilimo
26. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2018/2019, Wizara imeanzisha kitengo cha masoko ya mazao ya kilimo
ambacho kinahusika na kutafuta masoko ndani na nje ya nchi. Katika kutekeleza jukumu hilo, Wizara
imeingia makubaliano ya Itifaki ya Usafi baina ya Tanzania na Serikali ya China
kuwezesha kuuza muhogo nchini China ambapo hadi mwezi Machi 2019, kampuni tano
zimesajiliwa kwa ajili ya kuuza zao hilo nchini China.
Hifadhi na Usalama wa Chakula
27. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2018/2019, NFRA imenunua tani 46,236.035 za mahindi kwa ajili hifadhi na imeliuzia
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani tani 36,000 za mahindi zenye
thamani ya Shilingi bilioni 21. Aidha, Wizara
imeanza kutekeleza Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu katika mazao unaolenga kudhibiti
tatizo la sumukuvu katika mazao ya mahindi na karanga.
4.6 Huduma za Ushauri Kuhusu Utafiti, Mafunzo na
Usambazaji Taarifa za Kilimo na Sayansi Shirikishi
Huduma
za Ugani
28. Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2018/2019, Wizara imeandaa rasimu ya
Mwongozo wa Utoaji na usimamizi wa huduma za ugani utakaotumiwa na Sekta
ya Umma na Binafsi. Aidha, elimu kuhusu kanuni bora za uzalishaji wa mazao,
kuongeza thamani mazao ya kilimo, upatikanaji wa masoko, mitaji kwa ajili ya
kuwekeza kwenye kilimo, pembejeo na zana bora za kilimo imetolewa kupitia
maonesho na vyombo vya habari.
Vyuo na Vituo vya Mafunzo ya
Kilimo
29. Mheshimiwa Spika,
katika
mwaka 2018/2019, Wizara kupitia Vyuo vyake vya Kilimo imedahili na kufundisha wanafunzi 2,389
ambapo wanafunzi 2,051 wamefadhiliwa na Serikali na 338 wanajilipia wenyewe. Kati ya
wanafunzi waliodahiliwa, wanafunzi 1,537 ni ngazi ya Astashahada na 852
ni ngazi ya Stashahada. Jumla ya
wanafunzi 1,026 wakiwemo 263 wa Stashahada na 763 wa Astashahada watahitimu
masomo yao mwezi Juni, 2019.
4.7 Kuimarisha Ushirika
30. Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2018/2019, Tume ya Maendeleo ya Ushirika kupitia Shirika la Ukaguzi na
Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) limefanya ukaguzi wa nje kwa vyama vya
ushirika 2,297. Kati ya Vyama vilivyokaguliwa, asilimia 4.6 vilipata hati
inayoridhisha, asilimia 64.6 vilipata hati yenye shaka, asilimia 21.6 vilipata
hati isiyoridhisha na asilimia 9.2 vilipata hati mbaya. Hali hiyo ya Vyama vya
Ushirika siyo nzuri na hatuwezi kuifumbia macho. Natoa wito kwa Waheshimiwa
Wabunge katika maeneo yetu tuendelee kushirikiana na Halmashauri zetu
kuvisaidia vyama hivi ambavyo ni mkombozi wa mkulima.
4.8 Usajili wa Wakulima
31. Mheshimiwa
Spika,
Wizara imeanza usajili wakulima wote kwa mazao ambayo yanasimamiwa na Bodi. Mazao hayo ni, kahawa, korosho, miwa, pamba,
chai, mkonge, tumbaku na pareto. Hadi kufikia mwezi Machi 2019, wakulima
1,464,827 wametambuliwa na kusajiliwa katika maeneo mbalimbali nchini.
4.9 Masuala Mtambuka
32. Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2018/2019, Wizara imeendelea kuzingatia masuala mtambuka katika kutekeleza
majukumu yake. Masuala hayo ni pamoja na ushiriki wa vijana katika kilimo,
lishe, jinsia, hifadhi ya mazingira na VVU na UKIMWI.
5.0
MPANGO NA MAENEO YA KIPAUMBELE KWA MWAKA 2019/2020
5.1 Kuongeza Tija katika Kilimo
Upatikanaji wa mbegu bora za mazao
33. Mheshimiwa
Spika,
katika mwaka 2019/2020, Serikali kwa kushirikiana na Sekta
Binafsi, imejipanga kuzalisha jumla
ya tani 53,608.2 za mbegu mbalimbali. Wazalishaji hao ni pamoja na ASA, Vituo
vya Utafiti, Magereza na Sekta binafsi. Vilevile, ASA itazalisha vipando bora
vya mihogo pingili 7,000,000 na miche bora ya matunda 20,000. Ili
kufikia malengo hayo, miundombinu ya umwagiliaji itaboreshwa katika mashamba
yanayomilikiwa na ASA na eneo la uzalishaji wa mbegu litaongezwa hadi kufikia
hekta 811 katika mashamba mbalimbali.
Upatikanaji na udhibiti wa ubora wa Mbolea
34. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2019/2020, Wizara itasimamia
uagizaji na usambazaji wa tani 625,000 za mbolea zinazokadiriwa kutumika
nchini. Aidha, Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) itaongeza
mauzo ya mbolea kutoka tani 10,000 hadi tani 100,000. Vilevile, ghala moja (1)
lenye uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 za mbolea litakarabatiwa katika wilaya ya
Tabora pamoja na kuanza ujenzi wa kiwanda cha kuchanganya mbolea kwa uwiano (blending plant) katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Upatikanaji
wa Viuatilifu na Udhibiti wa Visumbufu
35. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020,
Wizara itanunua na kusambaza lita 300,000 na kilo 3,000 za viuatilifu kwa ajili
ya kukabiliana na milipuko ya visumbufu vya mazao. Aidha, Wizara itaendelea kuimarisha kituo cha
kudhibiti milipuko cha Kilimo Anga (Arusha) ili kutoa huduma bora. Vilevile,
Wizara itaendelea kuvijengea uwezo na kukarabati vituo 10 kati ya 36 vya
ukaguzi wa mazao mipakani.
Zana
za Kilimo
36. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2019/2020, Wizara itaanzisha kituo kimoja (1) cha zana za kilimo kwa
ajili ya kutoa huduma za kiufundi na mafunzo kwa watoa huduma binafsi wamiliki na watumiaji wa zana za kilimo kwa
lengo la kusogeza huduma karibu na wakulima katika Kanda ya Ziwa. Vilevile,
Wizara kupitia AGITF, imepanga kutoa mikopo 250 yenye thamani ya Shilingi
Bilioni 4.12.
5.2 Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Umwagiliaji
37. Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2019/2020, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itafanya tathmini ya
miradi ya umwagiliaji ambayo ujenzi wake haujakamilika ili miradi hiyo iweze
kukamilishwa kwa awamu.
Aidha, kupitia
Mradi wa Kuendeleza Skimu za Wamwagiliaji Wadogo, Wizara itakamilisha ujenzi wa
skimu 16 za umwagiliaji katika maeneo mbalimbali.
5.3 Utafiti wa Kilimo na Uhaulishaji wa Teknolojia
38. Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2019/2020, Wizara kupitia TARI imepanga kutafiti, kugundua na kusambaza aina 15
za mbegu bora za mazao ya nafaka, mizizi, mbegu za mafuta, mikunde, migomba na
mazao ya bustani. Vilevile, Wizara itasafisha aina tisa (9) za mbegu ya mpunga
na kuzalisha tani 10 za mbegu za awali katika Kituo cha Utafiti cha KATRINI. Aidha,
kupitia kituo cha TARI Naliendele, Serikali itajenga kinu cha kubangua korosho
chenye uwezo wa kubangua tani 1,800 kwa mwaka na kusindika tani 1,000 za mvinyo
na sharubati (juice).
5.4 Maendeleo ya Mazao
39. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2019/2020, Wizara
imepanga kuongeza uzalishaji wa mazao ya kipaumbele kwa kuendelea kuratibu
utekelezaji wa mikakati ya maendeleo ya
mazao hayo ikiwemo kuimarisha utafiti, upatikanaji na utumiaji wa
pembejeo na zana za kilimo, udhibiti wa visumbufu, huduma za ugani, kuongeza
maeneo ya uzalishaji, uongezaji wa thamani na upatikanaji wa masoko.
Zao
la Korosho
40. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2019/2020, Wizara
kupitia Bodi ya Korosho itaendelea kutekeleza programu ya kuzalisha miche bora milioni
10 ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
Aidha, Bodi kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango
itahakiki na kulipa vikundi vya wazalisha miche ya mikorosho kwa msimu wa
2017/2018 ambao hawajalipwa katika mikoa saba (7). Vilevile, Wizara itaratibu
upatikanaji na usambazaji wa tani 30,000 na lita 500,000 za salfa kwa ajili ya
kudhibiti visumbufu vya zao la korosho.
Zao
la Miwa na Uzalishaji wa Sukari
41. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia Bodi ya Sukari
itaratibu uzalishaji wa tani 403,786 za
sukari kwa kuongeza eneo la uzalishaji wa kilimo cha miwa kutoka hekta 52,000
hadi hekta 97,000. Wizara, kwa
kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Kituo cha
Uwekezaji Tanzania (TIC) itawezesha upatikanaji wa ardhi ya uwekezaji wa miradi
mipya ya sukari katika Wilaya za Kasulu, Kibondo, Rufiji, Geita, Kilombero,
Karagwe, Pangani, Bagamoyo na Morogoro.
Zao
la Kahawa
42. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia Bodi ya kahawa
itaongeza uzalishaji wa kahawa kutoka tani 65,000 hadi tani 80,000. Aidha Bodi
imepanga kuzalisha na kusambaza miche milioni 10 ya kahawa
katika Wilaya 42.
Zao
la Mkonge
43. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia Bodi ya Mkonge
imepanga kuongeza uzalishaji wa mkonge kutoka tani 38,506 hadi tani 113,506 kwa
kuongeza eneo la uzalishaji kutoka hekta 42,426.11 hadi 114,915.08, kusimamia
uendeshaji wa mfumo wa kilimo cha wakulima wadogo cha mkataba na kuimarisha
vyama vya ushirika na masoko ya mkonge.
Zao la Pamba
44. Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2019/2020, Wizara kupitia Bodi ya Pamba imepanga kuongeza uzalishaji wa pamba
kutoka tani 222,000 hadi tani 700,000 na tija kutoka tani 300 hadi tani 600 kwa
ekari. Aidha, upatikanaji wa mbegu za pamba utaongezeka kutoka tani 22,000 hadi
40,000 na upatikanaji wa viuatilifu utaongezeka kutoka lita milioni 7 hadi milioni
10.
Zao
la Tumbaku
45. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia Bodi ya Tumbaku
imepanga kuongeza uzalishaji kutoka tani 55,000 hadi tani 60,000; kuimarisha
vituo 1,972 vya kufungia na kuchambulia tumbaku; itaimarisha mfumo wa
upatikanaji wa pembejeo za zao la tumbaku kwa kuwaunganisha watoa huduma wa
pembejeo na Vyama vya Ushirika ili ziwafikie kwa wakati.
Zao la Chai
46. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia Bodi ya Chai
imepanga kuongeza uzalishaji wa chai kavu kutoka tani 34,000 hadi tani 40,000
ambazo ni sawa na tani 182,000 za majani mabichi ya chai. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PSSSF) itafufua
kiwanda cha chai cha Mponde ili kuimarisha upatikanaji wa soko la majani
mabichi ya chai kwa wakulima na kuongeza ajira.
5.5 Miundombinu ya Hifadhi na Uongezaji
Thamani Mazao ya Kilimo
47. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2019/2020, Wizara kupitia NFRA itakamilisha awamu ya kwanza ya Mradi wa
Kuongeza Uwezo wa Kuhifadhi ambapo ujenzi wa maghala matano (5) yenye uwezo wa
kuhifadhi tani 60,000 na vihenge nane
(8) vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 190,000 za nafaka utakamilika na hivyo
kuongeza uwezo wake wa kuhifadhi nafaka kutoka tani 251,000 hadi tani 501,000.
5.6 Vituo vya Utafiti huduma za
Ugani na Mafunzo
Kuimarisha
Vituo vya Utafiti
48. Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2019/2020, Wizara itakarabati ofisi na kuvipatia vifaa muhimu vituo vya
utafiti vya Ukiliguru, Ilonga na Tumbi. Aidha,
miundombinu ya umwagiliaji ya vituo vya utafiti vya Ilonga,
Naliendele, Ukiliguru na miundombinu ya uhifadhi wa mbegu katika vituo vya
Uyole, Ilonga na Seliani itaboreshwa.
Huduma za
Ugani
49. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2019/2020, Wizara
kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI na Sekta binafsi itakamilisha Mwongozo wa
Utoaji na Usimamizi wa Huduma za Ugani Kilimo ili kuendana na mahitaji ya sasa
ya utoaji wa huduma za ugani nchini.
Vyuo na Vituo vya Mafunzo ya Kilimo
50. Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2019/2020, Wizara
itadahili wanafunzi 2,500 ngazi ya Astashahada na Stashahada kwa ufadhili wa
Serikali. Vilevile, itakarabati miundombinu ikiwa ni pamoja na madarasa sita
(6), ofisi 12, mabweni 12, maktaba sita (6) na mabwalo ya chakula sita (6)
katika vyuo vya mafunzo ya kilimo vya Mtwara, Igurusi, HORTI Tengeru, Tumbi,
Mlingano na Maruku.
5.7 Kuimarisha Ushirika
51. Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2019/2020, Tume ya Maendeleo ya Ushirika itaimarisha udhibiti na usimamizi wa
vyama vya ushirika; itahamasisha wanachama wa Vyama vya Ushirika vya Mazao
kuanzisha SACCOS 1,500 kwenye maeneo yao; na itahuisha Sera ya Maendeleo ya Ushirika
ya mwaka 2002 na kuipitia upya sheria za ushirika.
5.8 Uratibu, Takwimu, Ufuatiliaji na Tathmini
52. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka
2019/2020, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Wizara ya Mifugo
na Uvuvi, Wizara ya Viwanda na Biashara, Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya
Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar itafanya Sensa ya kilimo.
5.9 Masuala Mtambuka
53. Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2019/2020, Wizara itaendelea kuzingatia masuala mtambuka yakiwemo ushiriki wa
vijana katika kilimo, lishe, jinsia, VVU na UKIMWI na mazingira katika
utekelezaji wa majukumu yake.
5.10
Maeneo Maalum ya Maboresho
katika Kilimo
54. Mheshimiwa Spika, naomba
nizungumzie maeneo machache ya kimkakati ambayo kama Wizara tumeona ni muhimu
kuyafanyia maboresho ili kuimarisha usimamizi wa kilimo na kuwapatia wakulima
huduma kwa urahisi zaidi. Maeneo hayo ni kama ifuatavyo:
Mapitio ya Sera na Sheria
55. Mheshimiwa Spika, Wizara imeanza na
itaendelea kuipitia Sera ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2013 na sheria mbalimbali
kwa lengo la kubaini maeneo ambayo yatapaswa kuhuishwa ili kwenda na hali
halisi ya sasa na mwelekeo wa Serikali wa kubadili kilimo chetu kuwa kilimo cha
kibiashara. Mtazamo wa Wizara ni kuwa na
Sheria moja itakayosimamia rasilimaliwatu, matumizi bora ya pembejeo, ardhi ya
kilimo na maeneo mengine muhimu.
Bima
ya Mazao
56. Mheshimiwa
Spika,
Wizara kwa kushirikiana na wadau imeanza mchakato wa kuanzisha Bima ya Mazao
hapa nchini ili kumwezesha mkulima kulipwa fidia pale anapopata hasara. Maandalizi
yanaendelea kufanyika ili katika mwaka 2019/2020 tuwe angalau na aina mbili za
mifumo ya Bima ya mazao inayoweza kutumika hapa nchini. Hata hivyo, ili
utaratibu huu uwezekane, kutahitajika takwimu sahihi za hali ya hewa pamoja na
uzingatiaji wa kanuni bora za Kilimo.
Usajili
wa wakulima
57. Mheshimiwa
Spika,
katika mwaka 2019/2020, Wizara itaimarisha kanzidata ya wakulima na kuendelea
na usajili wa wakulima wa mazao mchanganyiko kwa kushirikiana kwa karibu sana
na Vyama vya Ushirika na Taasisi nyingine kilele za wakulima kama vile Tanganyika Farmers Association (TFA).
Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge tusaidiane kuhamasisha wakulima katika maeneo
yetu ili watakapofikiwa na zoezi la uandikishaji watoe ushirikiano na waelewe
kwamba zoezi hili ni la kuwasaidia kupata huduma bora za Kilimo.
Masoko
ya Mazao ya Kilimo
58. Mheshimiwa
Spika, Wizara
imeamua kuimarisha utafutaji wa masoko ya mazao ya kilimo ndani na nje ya nchi.
Katika mwaka 2019/2020, Wizara itakiimarisha kitengo cha masoko kwa kukijengea
uwezo wa kufanya uchambuzi na utafutaji wa masoko ndani na nje ya nchi.
Aidha, elimu itaendelea kutolewa kwa wakulima
ili wazalishe kulingana na mahitaji ya soko. Vilevile, tutaendelea kufanya kazi
kwa karibu na taasisi nyingine zinazohusika na masoko nchini ikiwemo TANTRADE
na Soko la Bidhaa (TMX).
Mfumo wa upatikanaji wa Pembejeo za
Kilimo
59. Mheshimiwa
Spika,
Wizara imeanza zoezi la kupitia kwa kina mifumo iliyopo ya uzalishaji, uagizaji
na usambazaji wa mbegu, mbolea na viuatilifu. Mifumo iliyopo kwa sasa
inatofautiana kwani kuna baadhi ya Bodi za Mazao zinazojihusisha na
uagizaji na usambazaji wa pembejeo,
wakati mwingine Vyama vya Ushirika vinaagiza na kusambaza pembejeo kwa
wanachama wao, wakulima pia hununua pembejeo moja kwa moja kutoka kwa
wafanyabiashara na pia mbolea kwa sasa inaagizwa kwa mfumo wa pamoja (Bulk
Procurement).
60. Mheshimiwa
Spika, kutokana
na umuhimu wa pembejeo za kilimo na tofuati ya mifumo hiyo, tumeamua kuipitia
yote ili kuona mfumo bora unaoweza kutumika kuhakikisha pembejeo zenye ubora
zinapatikana na kusambazwa kwa wakulima kwa wakati. Malengo yetu ni kukamilisha
mapitio hayo na kupata majawabu ya mfumo bora ifikapo Juni 2019, ili mwaka
2019/2020 tuwe na mfumo madhubuti utakaokuwa na tija kwetu sote. Nina uhakika
kwamba, mfumo mzuri wa upatikanaji na usambazaji wa pembejeo utawezesha uwepo
wa pembejeo bora kwa bei nafuu na hivyo kuongeza matumizi kwa wakulima wetu.
61. Mheshimiwa
Spika, maelezo ya
kina ya hotuba yangu hususan mpango na maeneo ya kipaumbele kwa mwaka 2019/2020
yanapatikana ukurasa wa 61 hadi 91 katika kitabu cha hotuba cha Wizara ya
Kilimo kwa mwaka 2019/2020 kilichowasilishwa Bungeni.
6.0
SHUKRANI
62. Mheshimiwa
Spika,
kabla sijamaliza hotuba yangu naomba nitoe shukrani za dhati kwa watu, taasisi,
makundi na wadau mbalimbali ambao tunashirikiana kuendeleza kilimo. Kwanza, nawashukuru
sana, Naibu Mawaziri wa Kilimo, Mhe. Omary Tebweta Mgumba (Mb.) na Mhe.
Innocent Lugha Bashungwa (Mb.) kwa ushirikiano wanaonipatia katika kutekeleza
majukumu yangu. Napenda pia, kuwashukuru Katibu Mkuu, Mhandisi Mathew John Mtigumwe;
Naibu Katibu Mkuu, Prof. Siza D. Tumbo; Wakurugenzi wa Idara na Wakuu wa
Vitengo; Taasisi na Asasi zilizo chini ya Wizara; watumishi wote wa Wizara; na
wadau wa Sekta ya Kilimo kwa juhudi, ushirikiano na ushauri uliowezesha
kutekelezwa kwa majukumu ya Wizara kwa mwaka 2018/2019 pamoja na kuandaa Hotuba
hii. Ni matarajio yangu kwamba, nitaendelea kupata ushirikiano wao katika mwaka
2019/2020.
63. Mheshimiwa
Spika,
naomba nitumie fursa hii kuzishukuru Nchi na Mashirika mbalimbali ya Kimataifa
ambayo yamesaidia Wizara katika juhudi za kuendeleza kilimo. Nachukua fursa hii
kutaja baadhi yao kama ifuatavyo: Serikali za Japan, Marekani, Uingereza,
Ireland, Malaysia, China, Indonesia, Korea ya Kusini, India, Misri, Israel,
Ubelgiji, Ujerumani, Finland, Norway, Brazil, Uholanzi, Vietnam, Canada na Poland. Ninayashukuru pia Mashirika na Taasisi za
Kimataifa zifuatazo: Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, AU, IFAD,
DFID, UNDP, FAO, JICA, EU, UNICEF, WFP, CIMMYT, ICRISAT, ASARECA, USAID, KOICA,
ICRAF, IITA, IRRI, ILRI na CABI. Nyingine ni CFC, AVRDC, AGRA, CIP, CIAT/PABRA,
UNEP, WARDA, Shirika la Kudhibiti Nzige wa Jangwani na HELVETAS. Wadau wengine ni Shirika la Kudhibiti Nzige
Wekundu, Bill and Melinda Gates
Foundation, Gatsby Trust, Rockfeller
Foundation, Aga Khan Foundation, Unilever na Asasi zisizo za kiserikali
nyingi ambazo hatuwezi kuzitaja zote hapa.
64. Mheshimiwa
Spika, natoa shukrani
za pekee kwa wananchi wa Jimbo langu la Vwawa kwa ushirikiano wanaoendelea
kunipa katika kipindi chote cha kuwawakilisha hapa Bungeni. Aidha, napenda
kuwahimiza kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo ya jimbo letu na Taifa
kwa ujumla. Kwa umuhimu wa kipekee ninatoa shukrani za dhati, kwa wakulima wa
nchi hii kwa kazi kubwa wanayofanya katika uzalishaji wa mazao ya chakula na
biashara.
7.0
MAOMBI YA FEDHA MWAKA 2019/2020
65. Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2019/2020, Wizara inaomba idhini ya kukusanya maduhuli ya Shilingi 3,472,515,000 yatokanayo na vyanzo mbalimbali vya mapato.
66. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka
2019/2020, Wizara ya Kilimo inaomba kutumia jumla ya Shilingi 253,856,943,970 kupitia Fungu 43, Fungu 05 na
Fungu 24 kama ifuatavyo;
FUNGU 43 – Wizara ya Kilimo
67. Mheshimiwa Spika, jumla ya Shilingi 208,044,783,140 zinaombwa. Kati ya fedha hizo, Shilingi 143,577,036,140 ni kwa ajili ya
kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo Shilingi 82,000,000,000 ni fedha za ndani na Shilingi 61,577,036,140 ni fedha za nje. Aidha, Shilingi 64,467,747,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambapo Shilingi 13,214,159,060 ni kwa ajili ya mishahara ya Wizara, Shilingi 29,621,801,490 ni kwa ajili ya
mishahara ya Bodi na Taasisi, Shilingi
11,453,309,490 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo kwa Wizara na Shilingi 10,178,476,510 ni kwa
ajili ya matumizi mengineyo kwa Bodi na Taasisi.
FUNGU 05 – Tume ya Umwagiliaji
68. Mheshimiwa Spika, jumla ya Shilingi 37,485,090,830 zinaombwa. Kati
ya fedha hizo, Shilingi 32,501,462,613
ni kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo ambapo Shilingi 3,000,000,000 ni fedha za ndani na
Shilingi 29,501,462,613
ni fedha za nje.
Aidha, Shilingi 4,983,628,217 zinaombwa kwa ajili ya
matumizi ya kawaida ambapo Shilingi 4,098,444,217 ni kwa ajili ya
mishahara ya watumishi wa Tume na Shilingi
885,184,000 ni kwa ajili ya matumizi
mengineyo.
FUNGU
24 – TUME YA USHIRIKA
69. Mheshimiwa Spika, jumla ya Shilingi 8,327,070,000 zinaombwa kwa
ajili ya matumizi ya kawaida ambapo Shilingi 6,127,370,000 kwa ajili ya mishahara na Shilingi 2,199,700,000 kwa ajili ya matumizi
mengineyo.
Maelezo ya sehemu ya maombi ya fedha mwaka 2019/2020 kwa fungu 43, 65 na
fungu 24 yanapatikana ukurasa wa 93 hadi 95 katika kitabu cha hotuba ya bajeti
ya Wizara ya Kilimo.
HITIMISHO
70. Mheshimiwa
Spika,
Pamoja na hotuba hii, vipo viambatisho vinavyotoa ufafanuzi wa baadhi ya
maeneo. Hotuba hii pia inapatikana
katika tovuti ya Wizara ya Kilimo, www.kilimo.go.tz. Ninaomba kuhitimisha kwa kukushukuru wewe
binafsi na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza.
71. Mheshimiwa
Spika,
NAOMBA
KUTOA HOJA
No comments:
Post a Comment