Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe.Angellah Kairuki akihutubia washiriki wa Kongamano la Tano al Wadau wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi lililofanyika katika Ukumbi wa Hazina Dodoma Februari 13, 2019 kwa lengo la Kuchambua na Kujadili sera ili kuboresha maeneo ya kisera ya kilimo lililoratibiwa na Jukwaa la Watafiti na Wachambuzi wa Sera za kilimo kwa kushirikisha wadau mbalimbali nchini.
Naibu Waziri Kilimo Mhe.Omari Mgumba akiwasilisha hotuba yake wakati wa kongamano hilo.
Sehemu ya wajumbe walioshiriki kongamano hilo wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe.Angellah Kairuki linaloendelea Jijini Dodoma kwa siku tatu kuanzia tarehe 13 hadi 15 Februari, 2019.
NA. MWANDISHI
WETU
Serikali
imedhamiria kuendelea kujenga mazingira wezeshi na endelevu katika Sekta ya
Kilimo kupitia sera imara na
zenye kutekelezeka.
Hayo
yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji
Mhe.Angellah Kairuki wakati akifungua Kongamano la Tano la Wadau wa Sekta ya
Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuhusu Sera Jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa tarehe 13Februari, 2019.
Waziri
alieleza kuwa, dhamira ya Serikali inaenda sambamba na mchango wa sekta ya
Kilimo katika uzalishaji pamoja na ukuaji wa uchumi nchini kwa kuzingatia namna
sekta hiyo inavyochangia katika maeneo mengi ikiwemo,utoaji wa ajira kwa
wananchi waliowengi.
“Ni mambo ambayo
yanajieleza yenyewe na kila mmoja wetu anayajua vizuri. Asilimia 65.5 ya
Watanzania wanategemea ajira na maisha yao kwenye kilimo, pia kinachangia
asilimia 95 ya mahitaji ya chakula nchini na asilimia 65 ya mali ghafi ya
viwanda vyetu,”alisema Kairuki
Aidha aliongezea kuwa,
asilimia 30 ya fedha za kigeni hutokana na mauzo ya nje ya mazao na bidhaa za
kilimo na huchangia asilimia 25 kwenye pato la Taifa.
Sambamba na hilo waziri
alieleza kuwa jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano tangu imeingia madarakani
imeendelea kutambua umuhimu wa kilimo katika kuongeza tija maeneo ya uzalishaji
na mna haja ya kuleta msukumo zaidi katika kukiendeleza.
Pamoja na jitihada za Serikali katika kuimarisha
sekta hiyo, Waziri alibainisha baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta hiyo
ikiwemo na sehemu kubwa ya kilimo kutegemea jembe la mkono, matumizi madogo ya
mbegu bora zinazotoa mazao mengi na kuhimili maradhi na athari za kimazingira,
matumizi ya maji ni kidogo mno pamoja na kilimo kutegemea mvua bila
kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji chenye uhakika.
“Tunategemea mno mvua ya Mwenyezi Mungu hatujatumia
vya kutosha maji aliyotuwekea juu ya ardhi na chini ya ardhi kwa kilimo katika
hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo nchini hekta milioni 29 zinafaa kwa
kilimo cha kumwagilia lakini ni asilimia 1 tu ya ardhi hiyo inamwagiliwa.
Tumejipa lengo la kuongeza kilimo kinachomwagiliwa nchini,”alisisitiza Kairuki
Kairuki alihamasha wakulima kuendelea kutumia mbolea
kutokana na Tanzania kutumia wastani wa kilo19 kwa hekta kiwango ambacho ni
kidogo kulinganisha kiwango cha takribani kilo 50 kwa hekta kinachotumiwa na
Jumuiya na Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kwa upande wake Naibu Waziri Kilimo, Mhe.Omari
Mgumba alieleza jitihada za serikali kuendelea kuhakiki madai ya madeni yenye
ukakasi ya Wakala wa pembejeo wanaosambaza mbegu na mbolea wanaoidai serikali
kiasi cha shilingi bilioni 35.
“kama mnavyofahamu mwaka ukipita wa fedha madeni
yanahamia Wizara ya Fedha kwa hatua zingine ikiwemo kuyachunguza na
kujiridhisha ambapo hadi sasa yamebainika kuwa na ukakasi katika takwimu na
tofauti ya taarifa na Serikali inaendelea kufuatilia hujuma zilizofanyika ili
kujiridhisha,”alisisitiza Mgumba.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Kilimo Chuo cha Kilimo
cha Sokoine ,Jackline Mkindi alipongeza uwepo wa kongamano hilo ambalo litatoa
fursa za kujadili na kueleza changamoto wanazokumbana nazo hususani upande wa
usambazaji wa Pembejeo nchini na madeni yaliyopo ambayo hadi sasa ni
sh.bilioni 39.9 ambazo zinapaswa kulipwa na serikali.
“Tunaimba Serikali ishushe bei na kuendelea kulipa
madai sahihi kwa wanao stahili pamoja na kutataua changamoto za wakulima
kutofikia gharama za pembejeo na kuwasaidia kujikamua katika uzalishaji kwa
kuwa na pembejeo bora na kwa wakati,”alisema Mkindi.
Kongamano limeandaliwa na Jukwaa la Uchambuzi wa
Sera za kilimo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Sekta binafsi na za umma
ili kuleta mageuzi katika sekta ya Kilimo na kuchangia katika ukuaji wa Viwanda
na kuhudhuriwa na takribani zaidi ya washiriki 300 nchini.
=MWISHO=
No comments:
Post a Comment