Wednesday, February 20, 2019

SERIKALI YAKERWA NA MAUAJI, UNYANG’ANYI MIPAKANI

*Yaviagiza vyombo vya ulinzi viongeze ulinzi na doria 

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuongeza ulinzi na doria katika maeneo ya mipaka kutokana na ongezeko la vitendo vya mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha na vitisho kwa wananchi.

Pia, Waziri Mkuu ameagiza wakimbizi wote watakaobainika kutoroka kwenye makambi wanayohifadhiwa na kuingia uraiani wakamatwe na wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria za Tanzania, kwani wanachokifanya ni ukiukwaji wa sheria.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana jioni (Jumanne, Februari 19, 2019) alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa wilayani Kibondo wakati akihitimisha ziara yake mkoani Kigoma.

Alisema maeneo yaliyo katika hali mbaya ni Kibondo, Buhigwe, Kasulu, Ngara, Biharamulo, Uvinza, Kakonko na Kigoma Vijijini, ambako wananchi hususani wafanyabiashara wameingiwa na hofu kutokana na vitendo hivyo.

Waziri Mkuu alisema pamoja na undugu waliokuwanao na nchi jirani, lakini kila nchi ina sheria na taratibu zake, hivyo ni lazima zifuatwe na ni marufuku kuingia katika nchi yoyote bila ya kufuata sheria na taratibu za nchi husika.

“Kulinda usalama wa nchi ni jukumu letu sote na si la vyombo vya ulinzi na usalama pekee, kila mmoja anapaswa kushiriki. Kwa upande wa majirani zetu wanaotaka kuja nchini ni lazima wafuate taratibu kwa kuomba vibali.”

Alisema watu wote wanaoingia bila ya kufuata sheria na taratibu ndio hao wanashiriki katika vitendo vya uhalifu yakiwemo mauaji ya raia wasiokuwa na hatia, unyang’ani wa kutumia silaha za kivita pamoja na utekaji wa watoto.

Waziri Mkuu alisema kuwa vyombo vya ulinzi na usalama viendelee kulinda mipaka yetu na watu wote watakaobainika wameingia nchini bila vibali wakamatwe na wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.

Aliongeza kuwa wakimbizi wanaohifadhiwa katika maeneo mbalimbali nchini hawaruhusiwi kutoka nje ya kambi hizo kwa sababu huduma zote wanazostahili zikiwemo za afya, elimu  na chakula zinapatikana kambini.

Pia, Waziri Mkuu aliitaka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iwasimamie vizuri watumishi wake wanaofanya kazi kwenye kambi hizo na kuchukua hatua kwa watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.

Mbali na agizo hilo kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, pia Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa wizara hiyo ufanye mazungumzo na Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) ili litekeleze majukumu yake bila kukiuka sheria za nchi.

Kadhalika, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaonya wananchi kuacha tabia ya kuwachukua raia wa nchi jirani na kuwaleta nchini kwa ajili ya kuja kufanya kazi za vibarua katika mashamba yao bila ya kuwa na vibali.

“Tabia ya kuwachukua watu kutoka nchi jirani kwa ajili ya kulima mashamba bila ya kuwaandikisha ni makosa kisheria. Anayetaka kupata vibarua kutoka huko aende kuomba vibali huku akieleza idadi ya anaowataka na siku watakazokaa.”

Waziri Mkuu alisema lengo la kufanya hivyo ni kulinda usalama kwa sababu wengine wanawafanyisha kazi na wakimaliza hawawalipi wanawatishia kuwashitaki kwa kuingia nchi bila ya kibali jambo linalochangia kuwepo kwa migogoro na visasi.

Pia, Waziri Mkuu alisema hata kama wakiwalipa hakuna anayefuatilia kama kweli baada ya kumaliza vibarua hivyo wanarudi makwao kwani wengi wao wanaendelea kubaki nchini huku baadhi wakijihusisha na vitendo vya kihalifu.

No comments:

Post a Comment