Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, akiwasha umeme katika Kata ya Kanyala wilayani Geita ambayo imepata umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza (REA III).
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, (katikati) akiwasha umeme katika Kijiji cha Lwezera wilayani Geita ambacho kimepata umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza (REA III).Kushoto kwake ni Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma na wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ( wa Tano kushoto) akikagua miundombinu ya umeme katika Kata ya Kanyala wilayani Geita ambayo imepata umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza (REA III).Wa Tatu kulia ni Mbunge wa Geita Mjini, Constantine Kanyau na Wa Tano kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Geita, Josephat Maganga.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard
Kalemani, ameeleza kuwa kasi ya usambazaji umeme vijijini inaendelea kuongezeka
ili kuweza kufikia lengo la Serikali la kusambazia umeme vijiji vyote ifikapo
mwaka 2021.
Dkt. Kalemani aliyasema hayo jana
akiwa katika ziara ya kukagua kazi ya usambazaji umeme katika Wilaya ya Geita
mkoani Geita ambapo aliambatana na viongozi mbalimbali wakiwemo Mkuu wa Wilaya
ya Geita, Josephat Maganga, Mbunge wa Geita Mjini, Constantine Kanyau, Mbunge
wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa
Nishati Vijijini, Mhandisi Amos Maganga.
“Kasi ya usambazaji umeme vijijini
kupitia mradi wa Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza inaongezeka, kwa mfano leo,
tunawasha umeme katika Vijiji 61 nchi nzima, na katika ziara yangu ya Siku Tatu
mkoani Geita nitawasha umeme katika Vijiji 12,” alisema Dkt Kalemani.
Katika siku ya kwanza ya ziara yake,
Dkt Kalemani alikagua miradi ya umeme wilayani Geita na kuwasha umeme katika
Kijiji cha Lwezera, Luhuha na mtaa wa Ibanda ulio katika Kata ya Kanyala. Pia
amewasha umeme katika Gereza la Butundwa ambalo linajishughulisha Kilimo na
Ufugaji.
Awali, Dkt Kalemani alifanya
mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel ambaye alimueleza
Waziri kuhusu mahitaji ya umeme katika Mkoa huo na kueleza kuwa
Mkoa umeshatenga eneo kwa ajili shughuli za Mnada wa madini na kuna
wawekezaji walioonesha nia ya kujenga mitambo ya kuchenjulia madini mkoani humo
hivyo ili kufanikisha suala hilo wanahitaji umeme wa uhakika.
Kuhusu suala hilo, Dkt Kalemani,
alieleza kuwa, Wizara inatambua lengo la Serikali la kuwa na viwanda
vya kutosha ili kuingia katika uchumi wa viwanda, hivyo Mkoa huo unachotakiwa
kufanya ni kuwasilisha mahitaji yake ya nishati ili yaweze kufanyiwa kazi.
Kwa upande wao, Mbunge wa Geita Mjini
na Geita Vijijini, kwa nyakati tofauti walieleza kuhusu masuala mbalimbali
yanayopaswa kufanyiwa kazi ikiwemo TANESCO kusogeza huduma karibu na wananchi
na kasi ya mkandarasi kuendelea kuongezeka, masuala ambayo Waziri wa Nishati
aliyaafiki na kutoa maelekezo kwa TANESCO na mkandarasi kampuni ya Whitecity
Guangdong JV.
No comments:
Post a Comment