Wednesday, February 13, 2019

Biteko ameitaka bodi ya STAMICO kuhakikisha inachangia pato la taifa kabla ya mwezi Juni, 2019


Waziri wa Madini, Doto Biteko akitoa maelekezo kwa mwenyekiti wa Bodi ya Stamico na Menejimenti ya shirika wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa shirika hilo.

Waziri wa Madini, Doto Biteko (Kulia) akimkabidhi Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Stamico  Mej. Gen (Mstaafu) ichael Isamuyo nyenzo ikiwa ni mwongozo katika kutekeleza majukumu ya bodi kwa shirika hilo.

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameitaka Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kuhakikisha kuwa sekta ya Madini kupitia shirika hilo inaongeza mchango wake kwa pato la taifa kwa kulipa mrabaha na kodi mbalimbali za serikali na kuongeza wigo wa ajira za watanzania kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi katika kuendesha shirika hilo.

Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo uliofanyika katika ukumbi wa ofisi za Stamico zilizopo maeneo ya Upanga jijini Dar es Salaam mnamo tarehe 12 February, 2019.

Biteko alisema anautambua wazi umuhimu wa Bodi hiyo katika kufanya maamuzi, kupitia Sheria na sera zinazohusiana na uendeshaji wa shirika hilo na ndio maana uundwaji wa bodi hiyo ulipewa kipaumbele mara tu baada ya yeye kuteuliwa kushika wadhifa huo wa Waziri wa Madini.

Ameendelea kwa kusema, uteuzi wao haukuwa rahisi na ulizingatia uwezo na uzoefu wa wajumbe katika kutekeleza majukumu ya Bodi pamoja na uzalendo walionao kwa taifa na kuwasihi kuhakikisha wanakuwa wasimamizi wazuri wa shirika hilo kwa manufaa ya Taifa.

Alisema, kigezo kikubwa kilichotumika katika uteuzi huo ni kuangalia ubunifu wa mtu mmoja mmoja, mahali anakofanyia kazi au alipofanyia kazi, “ninyi katika ofisi mlizopita mliacha mambo makubwa Imani yetu wizara ni kuwa mtatumia ubunifu huo katika kusimamia na kubadilisha taswira ya shirika letu”. Alisisitiza.

Alikiri kuwa Serikali imewaamini na kuwapa mamlaka ya kusimamia Shirika hilo tunaamini mnaweza ndio maana katika wengi mliteuliwa  ninyi.

Akibainisha majukumu ya Bodi hiyo, Biteko alisema ni pamoja na Kuisimamia Menejimenti ya Shirika katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku kwa mujibu wa Sheria.

Kusimamia sera ya Shirika na kuanzisha mifumo ya udhibiti katika utekelezaji wa Sera hizo, Kupitia na kuidhinisha miundo ya Maendeleo ya Watumishi wa Shirika, kupitia na kuidhinisha mishahara na marupurupu ya watumishi wa shirika pamoja na kuanzisha mfumo mzuri wa kutoa gawio kwa wana hisa wa Shirika.

Aidha, Biteko alilipongeza shirika kwa hatua nzuri waliyoifikia katika kutekeleza baadhi ya miradi ikiwa ni pamoja na uchimbwaji na uuzwaji wa makaa ya mawe wa Kabulo, kuanza uchenjuaji wa mabaki ya mchanga wa dhahabu katika eneo la mradi wa dhahabu wa Buhemba, kuzalisha na kuuza kokoto Ubena Zomozi, kuimarisha usimamizi wa miradi ya ubia ya TanzaniteOne na Buckreef na kampuni tanzu ya STAMIGOLD, na kuratibu shughuli za kuwaendeleza wachimbaji wadogo.

Biteko alikiri kuwa Serikali imechoshwa na kupata hasara kupitia katika shirika hilo, na kusema badala ya miradi inayoanzishwa katika shirika hilo kuzalisha faida inazalisha madeni na kuliingizia Taifa hasara ya mabilioni ya pesa.

Akitoa mfano wa watu wawili waliokwenda vitani, mmoja akiwa na moyo wa vita bila silaha na mwingine akiwa na silaha bila moyo wa kupigana Biteko alisema ni dhahiri yule mwenye moyo wa vita atashinda na kuitaka bodi hiyo kuiga mfano huo katika kutekeleza majukumu yake.

Aliendelea kusisitiza kuwa Serikali anaamini wajumbe wa bodi hiyo wanao moyo wa kupigana vita bila kubeba silaha na kuwasihi kuanzia hapohapokutekeleza majukumu yake, “anzeni hivyo mlivyo, ipeni Serikali sababu ya kuishawishi serikali kuleta pesa”. Alisisitiza.

Serikali ya awamu ya tano inafanya vitu vilivyoshindikana, Vilee vitu ambavyo watu wanasema haviwezekani ndivyo vinavyofanyika nasi tunaamini mmeteuliwa ili kurekebisha madhaifu ya Stamico yaliyoshindikana kwa muda mrefu, wakurekebisha na kulifanya shirika la Stamico kuwa bora ni ninyi bodi pamoja na  menejimenti ya shirika.

Aidha, ameitaka bodi hiyo kumtafuta popote pale mtu yeyote wanayedhani anaweza kulisaidia Shirika kuzalisha faida na vile vile amewataka kumpeleka mtu yeyote mwenye cheo chochote anayelirudisha shirika hilo nyuma ili atafutiwe kazi nyingine ya kufanya.

“Haiwezekani shirika kutoka kuundwa kwake mwaka 1972 halijawahi kutoa gawio, haiwezekani lipo kwa ajili ya nini? Lakini watu wakizunguka wanalipwa posho lakini mwenye mali hapati kitu”. Biteko aling’aka.

Aidha, Biteko aliwataka wanabodi hao kubadilisha wimbo wa lawama unaosbabaishwa na shirika hilo na kuimba wimbo wa sifa, amekiri kutaka matokeo na sio stori. Alisema kwa namna anavyowafahamu wajumbe hao wa bodi wakishindwa kulibadilisha shirika hilo kwa awamu hii yeye binafsi atakuwa wa kwanza kuomba shirika hilo lifutwe.

Aliwataka wajumbe hao wa bodi kuifanya Stamico kuwa eneo la mataifa mengine kujifunzia namna bora ya kuendesha mashirika ya umma ikiwa ni pamoja na kuwaacha kufanya maamuzi yao kama shirika.

Alimuhakikishia Mwenyekiti wa bodi hiyo kuifanyia kazi changamoto ya uhaba wa wafanyakazi unaolikabili shirika mara tu baada ya kuurekebisha muundo wa uongozi wa shirika hilo aliokiri kuwa na vyeo vingi kulioko uwezo na uzalishaji wa shirika.

Aliitaka bodi hiyo kuhakikisha inabadilisha fikra na taswira ya shirika kwa kubadilisha namna ya kufikiri kwa watendaji wake ili wafikiri kibiashara zaidi na si kimishahara.

Alisisitiza kuwa anataka aibu ya Stamico ya miaka mingi iondolewe sasa na kama sio sasa basi sasa hivi, na kuwataka kutoa taarifa wakati wowote wanapoona wanakwama katika kutekeleza majukumu yao.

Aidha, Biteko aliitaka bodi hiyo kwenda kufuatilia suala la hisa za kampuni ya Tanzania Gemstone Industries Ltd (TGI) iliyosajiliwa mnamo mwaka 1969 ikiwa ni kampuni Tanzu ya Stamico na kutoliingizia faida yeyote shirika licha ya uzalishaji kufanyika na kuwa na umiliki wa hisa za kampuni ya Mundarara Mining Ltd kwa asilimia 50.

Alihitimisha kwa kusisitiza kuwa wizara haitaingilia masuala ya shirika lakini jicho lake litakuwa Stamico kutokana na kwamba kushindwa kwa shirika ni kushindwa kwa wizara na kushindwa kwa wizara ni kushindwa kwa Waziri kitu ambacho hatakikubali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mej. Gen (Mstaafu) Michael Isamuyo alitoa shukrani zake kwa uteuzi uliofanywa wa kumpatia fursa ya kuwa Mwenyekiti wa bodi hiyo ambapo alieleza kuwa aliyeteuliwa mwezi Disemba Tarehe 6 na baadaye kuteuliwa kwa wajumbe wengine wa bodi ambao amekiri watafanya kazi kubwa kwa shirika na taifa.

Alikiri kuwa wajumbe wa bodi wametoka katika maeneo mbalimbali wakiwa na ujuzi na uzoefu tofauti tofauti ambao wakikaa pamoja katika kutekeleza majukumu watafanya kitu kikubwa na kusababisha mabadiliko makubwa kwenye Shirika kubwa la Taifa la madini.

Amekiri kuwa masuala yote waliyoagizwa watatekeleza kama walivyoelekezwa “Majukumu yetu tunayafahamu lakini haya majukumu ni muongozo tu, naamini tutatumia uwezo wetu, tutatumia akili zetu, uzoefu tulionao katika maeneo mbalimbali kuhakikisha kuwa tunatekeleza majukumu yetu kwa ufanisi kuhakikisha kwamba zile changamoto ambazo zipo na zitakazoendelea kujitokeza tunazigeuza kuwa fursa na tunazitatua”. Alisisitiza.

Amesema katika ameneo yote changamoto hazikosekani, lakini kufanya kazi kwa mazoea ndiko kunakorudisha nyuma mafanikio “huu mfumo wa kufanya kazi kwa mazoea bila ubunifu wowote utaturudisha nyuma alisema na haya ndiyo masuala uliyotushauri” amekiri kuwa bodi yake ina utashi huo na watahakikisha kuwa wanakuwa na ubunifu wa hali ya juu na kuifanya Stamico kujikwamua kutoka mahali walipo.

Akijibu hoja ya kuwa na moyo wa vita kabla ya kupata silaha, Isamuyo alisema yapo matatizo mengi kwa shirika ikiwa ni pamoja na suala la uhaba wa mitaji pamoja na wafanyakazi, na kuiri kuwa kutokana na moyo wa vita walionano changamoto hizo zitageuzwa na kuwa fursa.

Akitolea mfano ujenzi wa nyumba zenye vioo zilivyowafanya wezi kuichukulia ujenzi huwa kama fursa kwa kuwarahisishia kuingia  ndani ndani ya nyumba bila shida lakini pia hiyo kuwa ni fursa kwa wajenzi na wafanyabiashara kuzalisha kuzalisha nondo na kujengea ili kuwapa wezi kazi ya kufanya pindi wanapotaka kuvamia majengo ya watu kwa lengo la kuwaibia. Isamuyo ameahidi kugeuza changamoto za Stamico kuwa fursa na kulipeleka shirika mbele.

Amemuhakikishia Waziri wa Madini kuwa bodi hiyo haitashindwa kazi, “Hatutashindwa kwa sababu hamkushindwa kututeua, mlikuwa na majina mengi yenye sifa zinazofanana na zetu lakini hamkushindwa kututeua na kwa sababu ninyi hamkushindwa kututeua na sisi hatutashindwa kuhakikisha kwamba tunasonga mbele katika kutekeleza majukumu ya shirika” alisisitiza .

Amekiri kwamba kabla ya kuomba silaha ya mizinga sehemu yeyote tutahakikisha kwamba silaha ndogo zitafanya kazi na kuhakikisha adui anapigwa, amesema watumishi waliopo lazima wahakikishe kuwa wanafanya kazi na kuliletea shirika faida bila kutegemea mtu kutoka eneo lingine. Alisema waajiliwa wengine wakipatikana waje kuongeza nguvu lakini si kwa sababu waliopo wameshindwa kazi.

Kuhusu Mikataba isiyokuwa na tija, Isamuyo amewataka wanasheria kuhakikisha mikataba inayoingiwa sasa hivi inazalisha faida tofauti na ilivyokuwa awali.

Kuhusu agizo la kuhakikisha shirika linatoa gawio kwa serikali, Isamuyo amesema agizo hilo limetolewa kwa mwanajeshi, hilo ni agizo na litatekelezwa vizuri sana na kuahidi kufuatilia suala la kushughulikia hisa za kampuni ya Tanzania Gemstone Industries Ltd(TGI) ambayo ni kampni tanzu ya Stamico itashughulikiwa ipasavyo.

Ameiomba serikali kushughulikia changamoto za msingi na masuala mengine yanayopaswa kutatuliwa na wizara kufanyiwa maamuzi mapema ikiwa ni pamoja na suala la ajira mpya na kukiri kuwa shirika ni la kibiashara hivyo kila dakika inayopotea inazalisha hasara kwa shirika.

Uzinduzi wa Bodi hiyo ulishirikisha viongozi wote waandamizi wa wizara ikiwa ni pamoja na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo aliyewataka Bodi hiyo kwenda kufanya kazi na kuithibitisha Imani ya serikali kwao, Katibu Mkuu wa Wizara, Prof. Simon Msanjila pamoja na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Issa Nchasi.

No comments:

Post a Comment