Katibu Mkuu wa madini, Prof. Simon Msanjila
(kushoto) akieleza jambo katika kikao baina ya viongozi wa juu wa wizara na
viongozi wa mgodi wa North Mara kilichofanyika tarehe 17 Januari, 2019 ofisini
kwa Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia) jijini Dodoma.
Na Nuru Mwasampeta
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameutaka uongozi
wa mgodi wa North Mara kutii Mamlaka ya Serikali kwa kutekeleza maagizo
yanayotolewa na mamlaka za Serikali nchini.
Biteko alitoa kauli hiyo Jana tarehe 17 mwezi
Januari katika kikao kilichoanza kwa utulivu mkubwa lakini kadri dakika
zilivyokuwa zikisonga mbele kiligeuka kichungu na kuwapelekea wajumbe kutoka
mgodi wa North Mara na Bulyanhulu kuridhia kuanza kuwalipa fidia wananchi
wanaozunguka mgodi huo ambao wamekaa kwa muda mrefu pasipo kulipwa fidia zao.
Katika kikao hicho, Waziri wa Madini, Doto
Biteko, alianza kwa kuwahoji viongozi wa mgodi wa North Mara na Bulyankulu juu
ya changamoto kubwa iliyopo katika eneo
lao ambapo bila kusita walikiri wazi kuwa ni suala la malipo ya fidia ya ardhi
kwa wananchi wanaouzunguka mgodi huo.
Akizungumzia ukiukwaji katika kutekeleza
maagizo ya Serikali Waziri Biteko aliwaeleza wajumbe hao kuwa ili kuonesha
wanatii mamlaka ya Serikali walipaswa kuwa wamechukua hatua kadhaa katika
kuelekea kutatua changamoto hiyo.
Biteko alionesha kusikitishwa na mwitikio
unaooneshwa na wawekezaji hao ambao kutoka kikao cha mwisho kilipokaa na
kuafikiana kuanza kulipa fidia ya ardhi kwa wananchi wanaozunguka mgodi huo ni
miezi minne na hakuna chochote kilichofanyika.
“Hatuwezi kuwa tunakaa, tunafikia maamuzi
ninyi mnayapinga, ni nani yupo juu ya Serikali” Waziri Biteko alihoji. “Mnajua
suala la ardhi ni kubwa sana, mnajua ni maelekezo ya Rais, sasa Rais ameagiza
halafu hakitokei kitu! Mimi sielewi kabisa. Afadhali watu wangeanza kulipwa
unaweza sema sasa hatua za malipo zinafanyika lakini kuko kimya”aling’aka.
Akizungumzia chanzo cha mgogoro kuchukua muda
mrefu Biteko alisema ni tathmini iliyofanyika kwa mara ya pili kupelekea kiasi cha fidia mgodi unaopaswa
kuwalipa wananchi kuongezeka kutoka bilioni 1.6 hadi kufikia bilioni 12.
Akifafanua hilo mara baada ya kuzungumza na
mthaminishaji Mkuu wa Serikali (jina halikupatikana) kwa njia ya simu, Biteko
alisema ameelezwa kwamba tathmini inayofuatwa ni ile iliyofanyika kwa mara ya
pili maana hiyo ndiyo current na kukazia kuwa hawawezi kufuata ya awali
kutokana na kwamba muda wa kuwalipa fidia hizo ulipaswa kutokuzidi miezi sita
tangu tathmini kufanyika.
Ilielezwa kwamba, mara baada ya tathmini
kufanywa kwa ajili ya malipo ya fidia, haipaswi kuzidi miezi sita na baada tu
ya tathmini kufanyika; walipaswa kutoa tangazo ili kusimamisha uendelezaji wa
maeneo ili kutokuongeza uwekezaji utakaopelekea wananchi kulipwa zaidi.
Biteko alieleza kuwa wananchi wanaomiliki maeneo
hayo wakiendelea kufanya shughuli za maendeleo katika maeneo yao baada ya miezi
sita kutoka tathmini ilipofanyika ni dhahiri kuwa gharama ya kumlipa fidia
mwananchi huyo itaongezeka tu.
Aidha, Biteko aliwaeleza wajumbe hao kuwa
uongozi wa mgodi huo hawazifuati mamlaka husika katika kutatua changamoto hiyo
na kubainisha kuwa mgogoro huo hautatatuliwa na wizara ya Madini isipokuwa ni
watu wenye mamlaka na masuala ya ardhi.
Akijibu hoja ya mmoja kati ya wajumbe kutoka
North Mara aliyejaribu kueleza kuwa kiongozi mkuu wa masuala ya kisheria katika
mgodi huo anayeishi nchini Uingereza ni sharti aelezwe pindi maamuzi na maagizo
yeyote yanapopokelewa katika mgodi ili kufanya maamuzi yanayokidhi matakwa ya
mgodi. Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila alihoji endapo
north Mara ipo juu ya Serikali?
Prof. Msanjila aliendelea kwa kusema
haiwezekani mtu asiyekuwa na maamuzi katika mgodi kushiriki katika vikao
vinavyojadili na kutoa maamuzi halafu mtu asiyeshiriki katika vikao hivyo
akapinga maamuzi hayo.
“Yaani Waziri atoe maamuzi halafu mtu aliyeko
Uingereza ayapinge that is totally subbodination maamuzi ya mwisho yakishafanywa na Serikali hakuna
serikali nyingine au kampuni yoyote ile iyapinge! Maamuzi yanayotolewa Tanzania
hayawezi kwenda kujadiliwa London sio Sheria hiyo, ndio maana kampuni lazima
iwe imesajiliwa Brella, kwa hiyo mambo ya kusema mshauri yupo London, South
Africa No”. Alikazia Msanjila
“Don’t talk about London or South Africa tunapoongelea
masuala ya Tanzania tunaongea kwa sheria
za Tanzania we have nothing to do with London hiyo ni yao” alisisitiza.
Msanjila aliwakumbusha makubaliano
waliyoafikiana katika vikao vya nyuma kuwa yaliyowataka wajumbe wa vikao vya
maamuzi wasiokuwa na nguvu ya kufanya nakutekeleza makubaliano ya kikao
wasishiriki katika vikao hivyo ili kuepuka kupotezeana muda.
Huyu ni waziri, anamwakilisha Rais, hamuwezi
kwenda kuomba ushauri London kwa maagizo yaliyotolewa na waziri, hiyo si
sheria. Prof. Msanjila Alikazia.
Baada ya mahjiano makali na yaliyochukua muda
mrefu kikao kilifikia muafaka na ujumbe kutoka North Mara kukiri kuwa kutokana
ukweli kwamba baadhi ya wananchi waliofanyiwa tathmini malipo yao hayana shida
watakwenda na kuanza kufanya taratibu za malipo.
Walikiri kuwa mara baada ya kufika katika
vituo vyao vya kazi watakwenda kuendelea na taratibu za malipo ili kuonesha
uungwana na kuionesha Serikali na jamii kuwa wamechukua hatua kwa makubaliano
yaliyoafikiwa na viongozi wakuu wa nchi.
Aidha, walikiri kuwa wamejifunza kitu kutokana
na kikao hicho na kukiri wanaendelea kujifunza kwani wameona madhara makubwa
katika kuchelewesha malipo hayo na kuipelekea kampuni hasara kwa kulipa zaidi
ya mara mbile ya kile walichotakiwa kulipa awali.
Zaidi ya hapo, wamejifunza juu ya uhalisia wa
kisheria upande wa tathmini ya ardhi
kuwa huwa hai kwa kipindi cha miezi sita
na ikizidi hapo inafanyika tathmini nyingine lakini pia wamejifunza juu ya
taratibu na sheria za kusitisha shughuli za maendeleo kwa wananchi kwa
kutangaza kusimamisha shughuli za maendeleo katika maeneo yaliyofanyiwa
tathmini kwa kipindi cha miezi sita na pia kulipa fidia kwa wakati ili wananchi
wakajiendeleze katika maeneo mengine watakayohamia.
Aidha, Bi Jane Reuben- Lekashingo alisema kuwa
si lengo lao kupinga maamuzi ya serikali ila wanachelewa kutokana na taratibu
za kiutendaji wanaazopaswa kuzifuata ili
kukidhi matakwa na taratibu za kampuni
katika kutekeleza majukumu yao na kukiri kuwa sasa watasimamia sheria za nchi
na kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa katika vikao vya maamuzi.
No comments:
Post a Comment