Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akizungumza na watendaji wa
sekta ya ardhi katika halmashauri ya wialaya ya Rufiji mkoani Pwani wakati wa
ziara yake ya kukagua makusanyo ya kodi ya ardhi katika halmashauri za mkoa wa
pwani. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Juma Njwayo.
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akizungumza na watendaji wa
sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Kisarawe mkoa wa
Pwani wakati wa ziara yake ya kushtukiza katika halmashauri
hiyo kukagua makusanyo ya kodi ya ardhi katika halmashauri za mkoa wa pwani. Wa
pili kushoto ni Mkuu Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Joketi Mwengelo.
Na Munir Shemweta, RUFUJI
Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline
Mabula amekerwa na tabia ya wakurugenzi wa halmashauri nchini kuitengea fedha
kidogo idara ya ardhi katika halmashauri na hivyo kuifanya idara hiyo kushindwa
kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Akizungumza na watumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya
wilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani jana, Dk Mabula alisema wakurugenzi wengi katika
halmashauri nchini wamekuwa wakiifanya idara ya ardhi kwenye halmashauri hizo
kama mtoto yatima.
‘’Ukienda katika halmashauri nyingi idara ya ardhi imekuwa kama
mtoto yatima na ofisi zake haziridhishi kabisa ukilinganisha na zile ofisi za
idara nyingine kama vile afya na elimu’’ alisema Dk Mabula.
Kwa mujibu wa Dk Mabula, halmashauri nyingi alizotembelea bajeti
ya idara ya ardhi haizidi shilingi milioni nne ukiachilia mbali fedha za mapato
ya ndani ingawa wakati mwingine hazipatikani zote na kubainisha kuwa tatizo
linaloonekana ni wakurugenzi kutofahamu kama idara hiyo ina fedha
nyingi na kuweka wazi kuwa iwapo halmashauri zitaamua kuisimamia sekta hiyo
kikamilifu zitajikusanya mapato mengi ukilinganisha na sekta nyingine.
Hata hivyo, Dk Mabula alisema, katika ukusanyaji mapato ya
serikali nchini sekta ya ardhi inaweza ikawa sekta ya pili au ya tatu kwa
kuingiza mapato mengi Serikali ikiwa nyuma ya taasisi zinazoingiza mapato mengi
kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji
Mashaka Abdallah alimueleza Dk Mabula kuwa idara yake inakabiliwa na changamoto
kubwa ya ufinyu wa bajeti inayotengewa kwa ajili ya kutekeleza kazi za ardhi
pamoja na vitendea kazi kama Kompyuta, Printer, Shajala na usafiri.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, hali
ya ukosefu wa vitendea kazi inawakatisha tamaa watendaji wa sekta hiyo lakini
pia inachangia watendaji hao kutofanya kazi zao vizuri na wakati mwingine
kuwalazimu kutumia fedha zao za mfukoni kufanikisha kazi walizopangiwa.
Katika muendelezo wa ziara yake mkoa wa Pwani katika halmashauri
za wilaya za Rufiji, Kibiti, Mkuranga pamoja na Kisarawe Dk Mabula alikuta kila
halmashauri ikidai kiasi kikubwa cha fedha kwa wamiliki wa viwanja na mashamba
tofauti na kiwango ilichowekewa kukusanya kwa mwaka.
Mkuu wa Idara ya Ardhi katika Halamashauri ya wilaya ya Rufiji
Mashaka Abdallah alieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2018/2019 halmashauri yake
ilipangiwa kukusanya jumla ya shilingi milioni 15 na hadi kufikia tarehe 31
Desemba 2018 ilishakusanya shilingi milioni 16.7 ikiwa ni sawa na asilimia
111.6.
Akigeukia suala la ukusanyaji mapato kupitia sekta ya ardhi, Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema halmashauri nyingi
zimekuwa zikifanya makisio machache ya fedha za makusanyo inayopangiwa huku
zikiacha fedha nyingi kwa wadaiwa na kuwataka watendaji wake kuweka makadirio
kulingana na uhalisia wa madeni wanayodai.
Alitolea mfano wa halmashauri ya wilaya ya Rufiji kuwa pamoja na
kuwekewa kiwango cha kukusanya shilingi milioni 15 kwa mwaka na kukusanya
milioni 16.7 hadi kufikia desemba 2018 na kujivunia kuvuka lengo la
mapato lakini kumbukumbu zilizopo Wizara ya Ardhi zinaonesha halmashauri hiyo
inadai kiasi cha shilingi bilioni Moja.
Amewataka wakurugenzi wa halmashauri kuweka mkazo katika makusanyo
ya kodi ya ardhi na kubainisha kuwa wakurugenzi hao wangeweza kuzisaidia idara
za ardhi kupitia mapato yao ya ndani katika kuzipatia vifaa na ofisi lakini
wanashindwa kufanya hivyo na kusisitiza kuwa ni lazima idara hizo ziwezeshwe
ili zifanye kazi kwa ufanisi.
Alibainisha kuwa, hata baada ya sasa kuelezwa kuwa asilimia
thelathini ya mapato ya halmashauri ambayo yalikuwa yakirejea kwenye
halmashauri kuondolewa, wakurugenzi wamekata tama na kuziacha idara hizo bila
kuzisaidia lakini wakisahau kuwa mapato yanayopatikana kupitia sekta ya ardhi
ndiyo yanayorudi kusaidia shughuli za maendeleo.
Amewataka wakurugenzi wa halmashuri nchini kubadili tabia zao za
kuitenga idara ya ardhi na hivyo kuisadia kwa hali na mali kuhakikisha inafanya
kazi zake kwa ukamilifu na mwisho wa siku kuisadia kuingiza mapato serikalini.
No comments:
Post a Comment