Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionyesha
michoro ya majengo ya Hospitali ya Uhuru inayotarajiwa kujengwa katika
kijiji cha Maduma wilayani Chamwino wakati alipokagua eneo hilo, Januari
18, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimshukuru Mzee, Meshack Njamasi, mmoja wa wananchi waliotoa maeneo yao bure kwa serikali ili yatumike kwa ujenzi wa Hospitali ya Uhuru katika kijiji cha Maduma wilayani Chamwino, Januari 18, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),
Selemani Jafo (kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge
(kulia) wakati alipokagua eneo itakapojengwa Hospitali ya Uhuru katika
kijiji cha Maduma wilayani Chamwino, Januari 18, 2019. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amekagua eneo la ujenzi wa hospitali ya Uhuru lenye ukubwa
wa ekari 109 lililoko katika wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.
Akizungumza
na wakazi wa kijiji cha Maduma wilayani humo leo mchana (Ijumaa, Januari 18,
2019), Waziri Mkuu amesema uamuzi wa Serikali ya kijiji hicho wa kutenga maeneo
ya maendeleo ni wa kupigiwa mfano na vijiji vya maeneo mengine.
“Uamuzi
wenu wa kutenga maeneo ya miradi ya maendeleo umekuwa na tija, ndiyo maana
Mheshimiwa Rais Magufuli aliposema ijengwe hospitali, hamkupata shida sababu
eneo tayari lilikuwepo. Ninawapongeza wazee waliojitolea maeneo yao ili
kuongeza kwenye eneo la hospitali,” amesema.
Wazee
waliotoa maeneo yao ni Mzee Meshack Njamasi (ekari 5.50), Mzee Jobu Malogo
(ekari 3.50) na Bw. Nehemia Mwikwi (ekari 4.50). Ekari 95.5 zilizobakia,
zimetolewa na Seriakli ya kijiji hicho.
Waziri
Mkuu aliwataka wakazi wa wilaya ya Chamwino wasibweteke bali wajipange na kila
mmoja ajipange kufanya kazi kama ambavyo Rais Magufuli amekuwa akihimiza.
“Ujenzi wa mji wa Serikali unaoendelea hivi sasa ni fursa kwenu. Na ujio wa
hospitali hii ni fursa nyingine kwa wana-Chamwino hasa kwa vile ujenzi wake utatumia
mfumo wa force account ambao unatoa fursa kwa wanajamii
kushiriki kazi za miradi ya eneo husika,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema ujenzi wa hospitali hiyo yenye hadhi ya wilaya ni utekelezaji wa
Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inayoelekeza wananchi wapatiwe huduma za
matibabu huko huko waliko. “Hadi sasa tumeshajenga vituo vya afya 350 ili
kusogeza huduma kwa wananchi na jumla ya hospitali za wilaya 67, zinajengwa
nchi nzima kwa mwaka huu,” amesema.
Mapema, akimkaribisha
Waziri Mkuu kuzungumza na wakazi wa vijiji jirani, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais (TAMISEMI), Bw. Selemani Jafo alisema eneo la ujenzi wa hospitali hiyo
liko umbali wa kilometa mbili kutoka barabara kuu ya Dar es Salaaam-Dodoma na
kilometa tatu kutoka Ikulu ya Chamwino.
Naye, Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine
aliwataka wakazi hao wachangamkie fursa hiyo kwa kusomba mawe, mchango, maji na
kwamba Kamati za usimamizi wa ujenzi zitapaswa kusimamiwa na wanakijiji.
Aliwataka
wakazi hao wasiishie kwenye lengo la kuwa na hospitali ya wilaya, bali walenge
kujenga hospitali yenye hadhi ya mkoa kwa kadri bajeti itakavyoruhusu.
Akitoa
taarifa kwa
Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Bilinith Mahenge alisema ujenzi wa
hospitali hiyo ni wa hadhi ya wilaya ikiwa na nyongeza ya huduma za wagonjwa wa
dharura na wagonjwa mahututi (Emergency Department and Critical Care Unit).
Alimshukru
Rais Magufuli kwa kutoa fedha za ujenzi wa hospitali hiyo sh. milioni 995.18
ambazo zilipaswa kutumika kwenye maadhimisho ya siku ya Uhuru, Desemba 9, mwaka
jana. “Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutuongezea kiasi kingine cha fedha cha
sh. bilioni 2.35 na kutufanya sasa tuwe na sh. bilioni 3.22 za ujenzi huo,”
alisema.
No comments:
Post a Comment