Na Asteria Muhozya, Mbinga
Maafisa Madini nchini wametakiwa
kutobagua migodi midogo kwa kuelekeza nguvu kwenye migodi mikubwa tu
huku wakisisitizwa kutatua migogoro kwenye maeneo yao ya kazi na
kuelezwa kuwa, watakaobainika wakibagua
migodi hiyo na kutotatua migogoro wataondolewa
kwenye nafasi zao.
Hayo yalibainishwa Januari 17 na
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakati
akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini aina ya Sapphire wakati
wa ziara yake katika kijiji cha
Masuguru, Wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma.
Naibu Waziri Nyongo alifanya ziara hiyo
ikilenga kukagua shughuli za uchimbaji madini wilayani humo pamoja na
kusikiliza kero za wachimbaji katika migodi hiyo, ambapo wachimbaji waliwasilisha kero za kutaka
kutengewa maeneo kwa ajili ya shughuli za uchimbaji, bei elekezi za madini ikiwemo kuunganishwa na huduma ya umeme kwenye migodi yao.
Akizungumza kijijini hapo, alimtaka
Afisa Madini mkoa wa Ruvuma hukakikisha anaishughulikia kero hiyo na kuitatua mara moja na kuongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya
Muungano anataka wachimbaji nchini wachimbe madini, hivyo, maafisa madini kote nchini wahakikishe wanashughulikia kero
katika maeneo yao ya kazi ikiwemo kusuluhisha migogoro.
“Sisi ni matajiri, tumebarikiwa
madini ya vito. Wachimbaji chimbeni lakini mchimbe katika maeneo yaliyoruhusiwa
kuchimbwa”.alisisitiza.
Alisema kuwa, kama mgogoro ni mkubwa
wapo viongozi wa vyama vya wachimbaji wahakikishe kuwa wanafikisha migororo hiyo na kusema “tuleteeni
na sisi lakini usipoishughulikia
migogoro hiyo tutakuondoa.
Aliongeza kwamba, serikali inalenga
katika kuwatoa wachimbaji wadogo kutoka katika uchimbaji mdogo kwenda uchimbaji
wa kati na hatimaye mkubwa na ndiyo
sababu inaendelea na ujenzi wa vituo vya umahiri katika maeneo mbalimbali nchini ikilenga
katika kutoa elimu ya uchimbaji bora, uchenjuaji bora, biashara ya madini na
ujasiliamali ili kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogo wanakua.
Aliongeza kuwa, elimu
ya ujasiliamali ni muhimu kwa wachimbaji wadogo kwa kuwa itawaandaa kuwa
na uchimbaji endelevu na wenye tija.
Akijibu ombi la ruzuku, aliwataka wachimbaji wadogo kujiunga katika
vikundi vidogo vidogo ili iwe rahisi kwa
wachimbaji hao kufikiwa ikiwemo kupatiwa
huduma za leseni, elimu, vifaa, kuwamilikisha, kuwapatia mikopo na kuwafuatilia jambo ambalo litapelekea wafanye kazi kwa
urahisi na kwa kulipa kodi za serikali na wao kubaki na kipato kitakachowezesha maisha bora.
Alisema uwepo wa mazingira mazuri
migodini utasaidia vijana kufanya kazi na hivyo kuwa na taifa lenye watu
wanaofanya kazi. Aliwataka maafisa
madini wote kuhakikisha wanashughulikia migogoro ya wachimbaji wadogo na
kueleza kwamba, endapo serikali itakuta migogogoro ya wachimbaji wadogo katika maeneo yao wataondolewa.
Aliongeza kwamba, wizara imejipanga
na tayari kuna baadhi ya maeneo yametengwa kwa ajili ya wachimbaji na kuwasisisitiza kuhakikisha wanauza madini wanayoyachimba katika maeneo rasmi.
Akizungumzia suala la broker,
aliwataka kuhakikisha wanakuwa na leseni ya kufanya shughuli hizo ikiwemo vifaa
vya kupimia madini na kuwataka kulipa kodi. Pia, aliwatahadharisha wachimbaji
wanaoshirikiana na broker wasiokuwa na
leseni kuacha kwani kwa kufanya hivyo
ni kwamba kwamba wote wanaliibia taifa.”
Maafisa madini hakikisheni mnawajua ma broker wote na wawe na leseni na walipe kodi, “
alisisitiza Nyongo.
Akijibu ombi la ruzuku lililowasilishwa kwake, alisema fedha za ruzuku zilizokuwa zikitolewa
awali hazikuwafikia walengwa wote na kueleza kuwa, wapo waliopata ruzuku hizo
lakini hawakuwa wachimbaji na kuongeza kwamba, hivi sasa wizara inaangalia namna
bora ya kuwasaidia wachimbaji.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkoa wa
Ruvuma Abraham Nkya alisema kuwa, mkoa huo tayari umetenga
maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kwamba watashirikiana na wachimbaji
hao ili suala hilo liweze kuwasilishwa
Tume ya Madini kwa ajili ya hatua zaidi.
Awali , kiongozi wa wachimbaji aliwasilisha ombi kwa Naibu Waziri la wachimbaji kupatiwa ruzuku. Alisema mkoa huo umebarikiwa madini ya
ujenzi, nishati, viwanda huku eneo la
Masuguru likibariwa madini ya Sapphire. Alisema eneo hilo liliombwa kwa ajjili
ya uchimbaji mdogo lakini mpaka sasa
bado halijatengwa.
Pia, alisema ipo changamoto ya
kukosekana elimu kwa watendaji vijijini ambao wamesababisha mgizo mkubwa wa
kodi kwa wachimbaji.
No comments:
Post a Comment