Waziri wa Madini Angellah Kairuki akiangalia ramani ya jengo la Kituo cha Umahiri Chunya litakavyokuwa mara baada ya kukamilika kwake. Jengo hilo linajengwa na Mkandarasi SUMAJKT.
Sehemu ya jengo la Kituo cha Umahiri Chunya likiwa katika maendeleo ya ujenzi wake.
Sehemu ya viongozi wa Wilaya, viongozi wa Ofisi za Madini Mbeya na Chunya pamoja na wadau wa madini wilayani humo wakimsikiliza Waziri wa Madini Angellah Kairuki (hayupo pichani).
Waziri wa Madini Angellah Kairuki akisikiliza jambo kutoka kwa Mkandarasi SUMAJKT alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Umahiri Chunya. Wengine ni Wataalam kutoka Ofisi za Madini Mbeya na Chunya, wataalam kutoka Wizara ya Madini, na uongozi wa Wilaya ya Chunya.
Na
Asteria Muhozya, Chunya
Waziri wa Madini Angellah Kairuki amewataka Maafisa Madini nchini
kuhakikisha wanafanya kaguzi za mara kwa mara katika maeneo ya wachimbji wadogo
ikiwemo kutoa elimu ya uchimbaji, masuala ya afya na usalama kazini ili
kuongeza tija katika shughuli hizo.
Waziri Kairuki aliyasema hayo Novemba 27, wakati akikagua
maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Umahiri Chunya kinachojengwa na Mkandarasi
kampuni ya SUMAJKT.
Alisema, wachimbaji wadogo wanatakiwa kulelelewa ili watoke katika
uchimbaji mdogo wa madini kwenda uchimbaji wa Kati na hatimaye kuwa wachimbaji wakubwa, na kueleza kuwa, ili kufikia azma
hiyo elimu ya mara kwa mara kwa
wachimbaji ni muhimu ikatolewa kwani itawezesha serikali kupata mapato
kutokana na kufuata uchimbaji sahihi.
Pia, aliwataka Maafisa hao kuhakikisha kuwa wanatatua migogoro
katika maeneo yao kwani suala hilo litawezesha uzalishaji zaidi na kupelekea
serikali kunufaika na shughuli hizo, ikiwemo ongezeko la ajira na ustawi wa
jamii.
Vilevile, Waziri Kairuki alieleza kuwa, pamoja na kwamba katika
Mwaka wa Fedha 2018/19 wizara yake imepangiwa kukusanya shilingi bilioni 310,
lakini kama anataka makusanyo hayo yafikie shilingi bilioni 500 na kuongeza
kwamba, Maafisa madini watapimwa kutokana na ukusanyo huo wa maduhuli.
“ Sisi tumepangiwa kukusanya shilingi bilioni 310. Lakini na mimi
nataka makusanyo hayo yafikie shilingi bilioni 500 na nitawapima maafisa madini
kwa ukusanyaji wa maduhuli,” alisema Waziri Kairuki.
Katika hatua nyingine, amezitaka Halmashauri zote nchini
kuhakikisha kwamba zinashaurina na Wizara ya madini katika masuala yote
yanayohusu kodi za madini kabla ya kuyatolea maamuzi kwa kuwa, isipofanyika hivyo inachangia taasisi za serikali kukinzana
katika utoaji wa maamuzi.
Alisema, wizara inaandaa utaratibu wa kukutana na Mwanasheria Mkuu
wa Serikali na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais, TAMISEMI ili kulijadili suala la
kodi katika sekta ya madini.
Akizungumzia umuhimu wa Kituo cha Umahiri, alisema kuwa, kitawezesha
wachimbaji kujua taratibu zinazotakiwa katika
utekelezaji wa majukumu yao katika sekta ya madini na kwamba, wizara
inaangalia uwekezano wa kuwa na vituo hivyo katika kila mikoa ikiwemo ofisi za
kisasa na vituo vya mafunzo ili kuwezesha
kuwepo na tija zaidi katika sekta ya madini.
“ Tumeanza na vituo vya mahiri lakini upo umuhimu wa maafisa wetu
kuwa na nyumba za kuishi lakini pia kuhakikisha
kwamba maafisa wetu hawakai katika eneo moja kwa kipindi kirefu,” alisema.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Wilaya ya Chunya Athumani
Kwariko alimweleza Waziri Kairuki kuwa, leseni nyingi wilayani humo hazifanyiwi
kazi kutokana na wamiliki wake kukosa mitaji na uwepo wa migogoro. Hata hivyo amesema kuwa, tayari ofisi hiyo
imewasiliana na wamiliki hao ili kuhakikisha kwamba
wanaziendeleza leseni hizo.
Akizungumzia madini yanayopatikana
wilayani humo hiyo aliyataja kuwa ni pamoja na
ya dhdhabu, chuma, bati, ulanga, chokaa na kokoto na mchanga.
Naye, Mwenyekiti wa Chama Cha Wachimbaji Mkoa wa Mbeya Leonard
Manyesha akielezea umuhimu wa kituo hicho alisema kwamba kitawawezesha kupata maelekezo ya kitaalam kuhusu uchimbaji
na hivyo kuwawezesha kupata mazao bora ya dhahabu na yenye tija.
Aidha, alipongeza kwa hatua ya serkali ya kutaka kuhamasisha Mikoa
kutenga maeneo kwa ajili ya uanzishaji wa masoko ya madini na kueleza kuwa,
uwepo wa masoko hayo utasaidia tatizo la wachimbaji kuficha mapato kuisha.
No comments:
Post a Comment