Wednesday, November 28, 2018

MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA BALOZI WA PALESTINA PAMOJA NA BALOZI WA JAPAN JIJINI DAR ES SALAAM

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi wa Palestina nchini Mhe. Hamdi Mansour AbuAli (kushoto) aliyefika ofisini kwa Makamu wa Rais kujitambulisha, Ikulu jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Balozi wa Palestina nchini Mhe. Hamdi Mansour AbuAli (kushoto) aliyefika ofisini kwa Makamu wa Rais kujitambulisha, Ikulu jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Rais) 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuonyesha viungo vya chai kutoka Zanzibar Balozi wa Japan nchini Mhe. Shinichi Goto (kushoto) wakati wa kumkabidhi kama zawadi, Mheshimiwa Balozi wa Japan alifika ofisini kwa Makamu wa Rais kujitambulisha, Ikulu jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Rais) 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Hamdi Abuali, Balozi wa Palestina; Mhe. Shinichi Goto, Mhe. Balozi wa Japan na Bwana Abdulmajid Nsekela, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB.
Makamu wa Rais alianza kuonana na Mhe. Hamdi Abuali, Balozi wa Palestina , hapa nchini aliyekuja kwa lengo la kujitambulisha.
“Katika mazungumzo yetu alinielezea kuhusu hali ya kisiasa ya Palestina na uchaguzi mkuu unaotegemea kufanyika mwishoni mwa mwaka huu” alisema Makamu wa Rais.
Balozi huyo pia alimueleza Makamu wa Rais  jinsi anavyo furahishwa na utendaji kazi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwenye kujenga Tanzania mpya yenye kuendeshwa na uchumi wa viwanda.
Makamu wa Rais alipata nafasi ya kufanya mazungumzo na Balozi wa Japan nchini Tanzania ambaye alikuja kwa lengo la kujitambulisha.
Balozi huyo aliwasilisha salamu za Mhe. Shinzo Abe, Waziri Mkuu wa Japan na kueleza utayari wa Japan kuendelea kutusaidia katika kukuza uchumi.  
Makamu wa Rais ameipongeza Japan kwa kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa Maonesho ya Kibiashara ya ‘World Expo’ kwa mwaka 2025.
Pia Makamu wa Rais alitumia fursa hiyo kumshukuru Balozi wa Japan kwa mradi wao unaolenga kuboresha maisha ya watu wa hali ya chini kwenye sekta ya Elimu na Afya.
Vilevile Makamu wa Rais alimueleza Balozi huyo kuwa ili ushirikiano wetu uzidi kukua basi ni vyema kuhakikisha kuwa tunaendelea kubadilishana uzoefu ikiwemo kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wa pande zote mbili wanatembeleana na kunufaika na fursa zilizopo baina yetu.
Mwisho, Makamu wa Rais alikutana na kuzungumza Bwana Abdulmajid Mussa Nsekela, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB aliyefika ofisini kwa Makamu wa Rais kujitambulisha.
Pamoja na mambo mengine Mkurugenzi huyo alimueleza Makamu wa Rais shughuli mbalimbali za kibenki wanazotoa kwa Jamii na Serikali wakiwa na lengo la kuhakikisha huduma hizi hazitoki nje ya lengo la uanzishwaji wa Benki hii ambalo ni kuwezesha vikundi mbalimbali.

No comments:

Post a Comment