Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan taarifa inavyoonyesha hali halisi ilivyo sasa
katika masuala yanayohusu uzazi salama wakati wa uzinduzi wa kampeni ya
"Jiongeze Tuwavushe Salama" jijini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Makamu
wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi vitendea kazi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) mara baada ya uzinduzi wa kampeni ya "Jiongeze Tuwavushe Salama" jijini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Sehemu ya Wageni kutoka Taasisi mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa kampeni ya "Jiongeze Tuwavushe Salama" ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.Uzinduzi huo ulifanyika katika Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.(Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo kwa kila Mkuu wa Mkoa aifanye afya ya uzazi na mtoto kuwa ajenda ya kudumu katika vikao vya ushauri vya Mkoa (RCC).
Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo leo wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya “Jiongeze Tuwavushe Salama” ya Kuongeza kasi ya Uwajibikaji Kupunguza Vifo Vitokanavyo na Uzazi na Watoto Wachanga.
“Ili kuhakikisha suala la kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto katika nchi yetu linapewa kipaumbele cha juu katika shughuli za Serikali za kila siku” alisema Makamu wa Rais
Tafiti zilizofanyika mwaka 2015/2016 zinaonyesha kuwa, kiwango cha vifo vitokanavyo na uzazi ni 556 kwa kila vizazi hai 100,000 ambayo ni sawa na vifo 11,000 kila mwaka ambayo ni sawa na wanawake 30 hufariki kila siku, kutokana na matatizo yatokanayo na uzazi na kwa uapnde wa watoto wachanga ni 25 kwa kila vizazi hai 1000 .
Makamu wa Rais amesema jamii ina jukumu zito la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga kwa kuhakikisha kuwa inajiwekea mpango mahsusi wa rufaa wakati wa dharura na utambuzi wa dalili hatarishi kwa mama na mtoto mchanga.
“Nitoe rai kwa wananchi, wanawake na wanaume na vijana kujitokeza kuchangia damu mara kwa mara kwa kuwa wakifanya hivi wanaokoa maisha ya mama mjamzito na watoto.” Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 80 ya damu salama inatumika kwa wakina mama wajawazito na watoto alisema Makamu wa Rais.
Kauli mbiu ya kampeni hii “Jiongeze: Tuwavushe Salama” inaaminika inaaminika italeta matokeo chanya katika kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto wachanga nchini.
Kwa Upande mwingine Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu alimshukuru Makamu wa Rais kwa kukubali kuwa mlezi wa kampeni hiyo ambayo itatekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja, pia alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa kipaumbele kwa afya ya Mtanzania.
No comments:
Post a Comment