Tuesday, November 6, 2018

KAMPENI YA JUMANNE YA KUTOA KWA MWAKA 2018 IMEKUJA NA DONGE NONO KWA VIJANA

Foundation for Civil Society ni miongoni mwa mashirika yanayowezesha AZAKI mbalimbali hapa nchini kwa kuzipatia ruzuku, Na leo wamezindua rasmi kampeni yao ya Jumaanne ya kutoa (Giving Tuesday Campaign) ambayo uadhimisha kila mwaka na kwa mwaka huu wamekuja na mpango kabambe wa kuwawezesha vijana wanaofanya kazi za kijamii.
Washiriki wakifuatilia mkutano.

Akielezea Kampeni hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Bw. Francis Kiwanga alisema kuwa kampeni hiyo imekuwa ikifanyika duniani kote na mpaka sasa mataifa kumi yanaadhimisha siku hiyo Tanzania ikiwemo na kuyataja mataifa hayo ni India, China, Brazil, Mexico, Afrika ya kusini, Hispania, Rusia, na Jamhuri ya Czech pamoja na Romania.

Huku kauli mbiu kwa mwaka huu ikiwa ni  “Utoaji Wangu Hazina Yangu”

Aidha Mkurugenzi huyo alisema kuwa lengo la kampeni hii ni kuunga mkono na kuhamasisha utamaduni wa kujitolea hapa nchini, Na wameamua kulenga katika kundi kubwa ambalo ni vijana ili wawe na utamaduni huu wa kujitolea na kuweza kuifikia jamii yenye uhitaji kwa ukubwa zaidi.

Aliendelea kusema kuwa katika kampeni hiyo vitafanyika vitu vikubwa viwili cha kwanza ikiwa ni kampeni ndogo ya Kuchangia Damu itakayofanyika Novemba 24 katika Hospitali ya Muhimbili jengo jipya la Moi ghorofa ya nne kuanzia saa 3 kamili asubuhi mpaka saa 8 kamili mchana.

Na jambo la pili litakuwa ni kuchangia kwa ajili ya kituo cha New Hope Girls kilichopo Kimara jijini Dar es salaam, Hii ni asasi inayojihusisha na kuwalea watoto wa kike wanaoishi katika mazingira hatarishi wapatao 38 na mahitaji yao ni vitu vyenye thamani ya zaidi ya shilingi za kitanzania Million tisa (9000,000/=) ambapo inabidi michango hiyo iwasilishwe Novemba 27 ambayo ni Jumanne ya mwisho kwa mwezi Novemba.

Akizungumzia fursa hiyo Bw. Kiwanga alisema kuwa kwa vijana wenye umri kati ya miaka 18 mpaka 35 wanachotakiwa ni kuandaa stori au hadithi za kazi walizowahi kuzifanya katika kusaidia jamii eidha kwa kutoa Fedha, Muda, Kupaza sauti kwa ajili ya Wanyonge nk. Na kuviweka vitu hivyo kwa njia ya andiko lenye maneno yasiyozidi 200 au video isiyozidi dk 2 na kutuma kupitia barua pepe ifuatayo.

givingtuesday@thefoundation­-tz.org Huku mtumaji akianza na Jina kamili, Mahali anapoishi na Namba ya simu.

Kwa upande wa zawadi zitatoka kwa washindi watano wa kwanza huku mshindi wa kwanza akipatiwa Dola za Kimarekani 1500 na wapili atapata Dola 800, wa tatu Dola 700, wa nne Dola 600 na watano atapata 500 na mwisho wa kutuma ni tarehe 20 ya mwezi huu novemba.

Ikumbukwe kuwa Foundation for Civil Society ilianza kuadhimisha jumanne ya kutoa tangu mwaka 2016 ambapo waliweza kutoa vitu mbalimbali katika Shule ya msingi ya watoto wenye ulemavu ya Uhuru Mchanganyiko ikiwemo Magodoro, Mipira ya kuchezea na Mashine za kuandikia (Braille Machine) pamoja na kufanya ukarabati wa Vyoo ili viweze kutumiwa na watoto wenye wenye mahitaji maalum.

Na kwa mwaka 2017 waliadhimisha kwa kugharamia watoto wapatao 91 wenye Vichwa Vikubwa na Mgongo wazi kufanyiwa upasuaji na kutoa Bima za afya kwa watoto 101, Pamoja na kuhamasisha wananchi Kuchangia Damu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Kitengo cha Moi ambapo watu wapatao 40 walijitokeza kuchangia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society Francis Kiwanga akitoa ufafanuzi wa jambo mapema leo katika Uzinduzi wa Kampeni ya Jumanne ya Kutoa (Giving Tuesday Campaign) uliofanyika makao makuu ya shirika hilo Jijini Dar es salaam.

Meneja Biashara, Maendeleo na Ushirikiano wa FCS Martha Olotu akiendelea kutoa msisitizo kwa vijana kushiriki katika zoezi hili la jumanne ya kutoa.

Kijana Hussein Melele kutoka katika Taasisi ya Mulika Tanzania akiuliza maswali kuhusiana na kampeni ya Jumanne ya kutoa inayoendeshwa na Foundation for Civil Society.   

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Dorcus Masha ambaye pia ni muwakilishi wa Taasisi ya YUNA akiwasilisha maoni yake katika kampeni inayoendeshwa na FCS.

Meza kuu ikijibu maswali ya washiriki wa mkutano.

Mkutano ukiendelea 

No comments:

Post a Comment