Na Stella Kalinga, Simiyu
Katibu Tawala
Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amezindua rasmi mfumo wa ununuzi wa
dawa na vifaa tiba kupitia kwa mshitiri mmoja wa mkoa ujulikanao kama JAZIA,
uliobuniwa kuboresha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, vifaa vya maabara na
uchunguzi katika vituo vya kutolea huduma za afya vya Serikali ngazi ya Mkoa na
Halmashauri.
Akizindua
mfumo huo Novemba 05, 2018 Sagini amesema mfumo wa JAZIA si mbadala wa
Bohari ya Dawa (MSD) bali unalenga kuziba upungufu wa dawa, vifaa tiba, vifaa
vya maabara na uchunguzi katika Bohari ya Dawa (MSD).
“JAZIA ni
mfumo uliobuniwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na wataalam
washauri ili kuweza kuboresha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, vifaa vya
maabara na uchunguzi katika vituo vya kutolea huduma za afya vya Serikali ngazi
ya Mkoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, JAZIA si mbadala wa MSD bali ni
msaidizi wa MSD inapokuwa haina bidhaa husika.” alisema.
Aidha, Sagini
alibainisha kuwa mfumo huu utasaidia kupunguza gharama na bei ya upatikanaji wa
dawa kwani bei za dawa na vifaa tiba zitalingana na bei ya soko na sio matakwa
binafsi ya wazabuni.
Aliongeza
kuwa mfumo huo utapunguza urasimu uliokuwepo wa namna ya kununua dawa nje ya
MSD na hivyo kusaidia dawa kupatikana kwa muda mfupi huku akiwataka Waganga
wafawidhi wa vituo vyote vya kutolea huduma za afya kuagiza dawa na vifaa tiba
mapema wanapoona vinapungua kabla ya kusubiri vifaa hivyo na dawa kuisha
kabisa.
Kwa upande
wake Mratibu wa Mfumo wa JAZIA Mkoa wa Simiyu, Mfamasia Oscar Tenganamba
amesema mfumo huu ulifanyiwa majaribio katika mikoa ya Dodoma, Shinyanga na
Morogoro na kuonesha mafanikio makubwa na sasa hivi unatumika katika mikoa yote
Tanzania Bara.
Naye mmoja wa
wazabuni walioungana na kuwa mshitiri mmoja wa Mkoa katika dawa na Vifaa Tiba
(JAZIA) ambaye ni Mkurugenzi wa Operesheni kutoka Kampuni ya Total Health Lab
ya jijini Dar es salaam , Crispin Mtete amesema kampuni yake na Kampuni
ya Mufuruki Traders Company Ltd ya jijini Mwanza zitatoa huduma bora kwa
kuzingatia bei elekezi kama mkataba unavyoelekeza.
Mfumo wa
JAZIA utatumia mzabuni mmoja aliyechaguliwa kwa ushindani kujazia dawa na vifaa
tiba vinavyokosekana katika Bohari ya Dawa (MSD).
MWISHO
No comments:
Post a Comment