Wednesday, October 3, 2018

Wadau wa Madini Kimataifa wameona umuhimu wa Tanzania kufanya mabadiliko – Nyongo


Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akimsikiliza Balozi wa Australia nchini Alison Charters alipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma ambapo wamejadiliana masuala mbalimbali kuhusu Sekta ya Madini. Wengine ni Mwenyekiti kutoka Tume ya Madini Prof. Idris Kikula na Wataalam kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini na Ubalozi huo.

Na Asteria Muhozya, Dodoma

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amesema wadau wa Sekta ya Madini Kimataifa hivi sasa wanaelewa umuhimu wa Tanzania kufanya mabadiliko katika Sekta husika yakiwemo ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 yaliyofanyika Mwaka 2017.

Naibu Waziri ameyasema hayo leo ofisini kwake jijini Dodoma alipokutana na Balozi wa Australia Nchini, Alison Charters ambaye amemtembelea Naibu Waziri Nyongo kwa lengo la kujadiliana masuala kadhaa katika sekta ya madini ikiwemo kupata mrejesho wa ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Madini kwa nchi za Afrika uliofanyika mwezi Agosti, 2018, nchini Australia, ambapo katika mkutano huo, Tanzania iliwakilishwa na Naibu Waziri Nyongo.

Naibu Waziri Nyongo amesema kuwa, awali wadau katika mkutano huo walikuwa na uelewa tofauti lakini mara baada ya kutoa wasilisho kuhusu mabadiliko hayo katika mkutano huo, waliona umuhimu wa Tanzania kufanya mabadiliko hayo kwa maendeleo ya nchi na sekta nzima.

“Mhe. Balozi nashukuru kwa nafasi hiyo isipokuwa nilitamani kupata nafasi zaidi ya kuelezea uzoefu wetu na mabadiliko katika sekta ya madini,” amesisitiza Naibu Waziri.

Ameongeza kuwa, wawekezaji wengi hawana tatizo na mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2017 yaliyofanywa isipokuwa changamoto ipo katika kipengele cha chanzo cha mtaji kutoka katika benki za ndani suala ambalo amesema wizara imelichukua na inaifanyia kazi.

Pia, Naibu waziri amemshukuru Balozi Charters kwa kumwezesha kukutana na wadau mbalimbali wa sekta ya madini wakati akiwa nchini humo, kwani, wadau hao wameonesha nia ya kuisaidia Tanzania katika masuala ya uongezaji thamani madini nchini na mafunzo kwa wataalam wa sekta.

“ Tulizungumza masuala mengi na umuhimu wa sisi kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini kufanyika hapa nchini. Tunasisitiza suala hili kwa kuwa hivi sasa tumezuia usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi”, amesema Naibu Waziri Nyongo.

Kwa upande wake, Balozi Charter amesema nchi hiyo itaona namna bora ya kufanya ili kuweza kuisaidia Tanzania kutoa mafunzo kwa wataalam wa sekta husika lengo likiwa ni kuwajengea uwezo ili waweze kusimamia sekta hiyo vizuri.

“Tunayo bajeti kidogo lakini tunaweza kufanya jambo kwa ajili ya wizara ya madini katika utoaji wa mafunzo. Ikiwezekana hata kuwaleta wataalam wetu kuja kutoa utaalam huo hapa nchini,” amesema Balozi.

Aidha, Balozi huyo ameeleza kuhusu fursa za masomo ambazo zimekuwa zikitolewa nchini Australia zikiwemo nafasi za  mafunzo ya muda mrefu na mfupi na hivyo kuwataka wataalam wa Tanzania  kuomba nafasi hizo pindi zinapojitokeza.

Pia, balozi huyo ametaka kujua majukumu ya Tume ya Madini mara baada ya tume hiyo kuanzishwa ambapo Mwenyekiti wa Tume hiyo ambaye naye amehudhuria kikao hicho, Profesa Idris Kikula amemweleza balozi huyo majukumu yanayosimamiwa na tume hiyo ikiwemo mikakati ya tume katika kutatua changamoto zilizopo katika sekta husika.

Akizungumzia mabadiliko katika sekta ya madini pamoja na masuala ya uwajibikaji kwa kampuni za madini kwa jamii, balozi Charter amesema suala hilo ni la msingi kwani hata katika nchi hiyo masuala hayo yalipewa kipaumbele na kushauri iwapo wizara inaweza kukutana na wadau kwa ajili ya kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu masuala hayo.

Mbali na mrejesho wa ushiriki wa Tanzania katika mkutano masuala ya madini kwa nchi za Afrika, kikao hicho pia kimejadili masuala ya leseni za madini, Uwajibikaji wa kampuni za madini katika jamii zinazozunguka migodi na kuhusu  kampuni za madini kutumia kampuni za wazawa kutoa huduma katika migodi.

No comments:

Post a Comment