Wednesday, October 3, 2018

"WAZIRI TIZEBA ANAFANYA KAZI KUBWA"-WAZIRI MKUU

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na mamia ya wakulima leo tarehe 3 Octoba 2018 katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati akimuwakilisha Rais, John Pombe magufuli katika Maadhimisho ya Miaka 25 ya Mtandao wa wakulima Tanzania (MVIWATA), (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Mamia ya wakulima wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza leo tarehe 3 Octoba 2018 katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati akimuwakilisha Rais, John Pombe magufuli katika Maadhimisho ya Miaka 25 ya Mtandao wa wakulima Tanzania (MVIWATA).
Mhandisi Dkt Charles Tizeba, Waziri wa kilimo akitoa salamu za wizara yake wakati akizungumza leo tarehe 3 Octoba 2018 katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro katika Maadhimisho ya Miaka 25 ya Mtandao wa wakulima Tanzania (MVIWATA).

Na Mathias Canal-WK, Morogoro

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb) amepongeza juhudi za kiutendaji zinazofanywa na Waziri wa Kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) kuisimamia Wizara yake ikiwa ni pamoja na usimamizi madhubuti wa kufuta Kodi na Tozo ambazo sio rafiki kwenye sekta ya kilimo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameyasema hayo leo tarehe 3 Octoba 2018 katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro akimuwakilisha Rais, John Pombe magufuli katika Maadhimisho ya Miaka 25 ya Mtandao wa wakulima Tanzania (MVIWATA),

Waziri Mkuu ameeleza kuwa Waziri Tizeba amefanya kazi kubwa kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima kote nchini hususani kero ya muda mrefu kuhusu tozo na kodi nyingi zilizokuwa zikiwasumbua wakulima kutokana na kutokuwa na tija badala yake kusalia na tozo na kodi muhimu pekee.

Waziri Mkuu alisema kuwa Waziri huyo  ametekeleza mambo mengi katika wizara yake katika mazao mbalimbali kwa kufuta tozo na Kodi zisizokuwa na tija kwa wakulima ambapo pia hivi karibuni alifuta tozo takribani 17 kwenye zao la kahawa.

Aidha, alimpongeza Waziri huyo kwa kufanya kazi kubwa yenye weledi mkubwa ya kueleza na kutoa ufafanuzi katika maeneo mengi muhimu ili kuwajengea uelewa wakulima juu ya kufutwa kodi hizo sambamba na kutoa ufafanuzi wa kutosha kwa wawakilishi wa wananchi kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu alimpongeza waziri wa kilimo kwa usimamizi na uratibu mzuri wa kilimo cha zao la Muhogo ambao umepata soko kubwa hivyo aliwataka wakulima kote nchini kuchangamkia kilimo cha Muhogo ili kuongeza tija ya kipato cha mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.

Kwa upande  wake mlezi wa Mtandao wa wakulima Tanzania (MVIWATA) Mzee Steven Mashishanga ambaye ni Mkuu wa Mkoa mstaafu akitoa neno la shukrani katika maadhimisho hayo mara baada ya hotuba ya mgeni rasmi, alipongeza ushirikiano unaaonyeshwa na Wizara ya kilimo kupitia waziri mwenye dhamana hiyo Dkt Charles Tizeba kwa Mtandao huo kwani jambo hilo limeongeza ufanisi na tija katika utendaji.

Aliongeza kuwa ushirikiano huo umeimarisha MVIWATA ambao umeongeza wanachama kufikia zaidi ya 300,000 huku ukiwa na wakulima takribani milioni mbili ambao wamenufaika na shughuli za MVIWATA ikiwemo uanzishaji na uimarishaji wa vyombo vya akiba na mikopo zaidi ya 120, mafunzo kwa wakulima kuhusu taaluma mbalimbali zaidi ya 115,000; kujenga na kuboresha miundombinu ya masoko 10 ikiwemo masoko ya Kibaigwa, Tawa, Kinole, Nyandira, Igurusi, Kasanga, Mkata, Igagala, Malolo na Matai.  

MWISHO

No comments:

Post a Comment