Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia watoto wenye ulemavu wa
akili wakati alipotembelea Kituo cha watoto hao, cha Miyuji Cheshire House cha
jijini Dodoma, Septemba 2, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikabidhi zawadi ya keki kwa watoto wa Kituo cha Watoto Wenye Ulemavu wa Akili cha Miyuji Cheshire House jijini Dodoma, Septemba 2, 2018. Kushoto ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde, kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo hicho, Peter Mavunde na wapili kushoto ni mwakilishi wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma, Padri, Onesmo Wisi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia watoto wenye ulemavu wa akili wakati alipotembelea Kituo cha watoto hao, cha Miyuji Cheshire House cha jijini Dodoma, Septemba 2, 2018.
*Ataka uongozi wa Jiji la Dodoma
utembelee vituo vyote vya watoto wa aina hiyo
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ametoa msaada wa vyakula na mahitaji mengine kwa watoto
wenye ulemavu wa akili wenye thamani ya sh. 2,359,000.
Alikabidhi
msaada huo jana jioni (Jumanne, Oktoba 3, 2018) mbele ya uongozi wa kituo cha
Miyuji Cheshire Home kilichopo nje kidogo ya jiji la Dodoma wakiwemo wajumbe wa
Bodi, walimu na walezi.
Vifaa
hivyo ni mchele kilo 200, dengu (kg. 100), choroko (kg.30), mafuta ya kula
(lita 40), sabuni ya mche katoni moja, asali (lita 20). Vingine ni sukari (kg.
51), maji katoni sita, juisi katoni mbili, majani ya chai katoni moja, kahawa
na fedha taslimu sh. 226,000/-.
Akizungumza
mara baada ya kukagua majengo na miradi ya shamba la zabibu, ufugaji na bustani
ya kituo hicho, Waziri Mkuu alisema ameguswa sana na moyo wa kujituma
unaooneshwa na masista, walimu na walezi kwa watoto wanaolelewa kwenye kituo hicho.
“Kazi
ya kuwatunza hawa watoto ni kubwa sana inayohitaji upendo, moyo wa huruma na
uvumilivu. Mimi nimekaa nao kwa dakika chache tu, kazi nimeiona, kwa kweli
mnastahili pongezi sana,” amesema.
Alisema
amefurahi kusikia kwamba watoto 442 walipatiwa fursa ya kulelewa kwenye kituo
hicho na kusisitiza kwamba Serikali ya awamu ya tano imewaagiza watendaji wa
vijiji wahakikishe watoto wenye ulemavu wanapelekwa shule.
“Tumetoa
maelekezo kwa watendaji wa vijiji wafanye msako na kuwasisitiza wazazi wawatoe
nje watoto wao wenye ulemavu na kuwapeleka shule. Tumegundua kuwa hawa watoto
wakipelekwa shule wanafanya vizuri sana,” alisema.
Kuhusu
changamoto ya uhaba wa walimu na wataalamu kwenye kituo hicho, Waziri Mkuu
alisema jukumu la msingi la kusimamia masuala ya walemavu ni la Halmashauri.
Amewataka Afisa Elimu wa Jiji la Dodoma na Mkurugenzi wa Elimu (TAMISEMI)
watembelee vituo vyote vya mkoa huo vyenye watoto wenye mahitaji maalum na
kuainisha changamoto zinazowakabili na wazitafutie ufumbuzi.
“Afisa
Elimu wa Jiji na Mkurugenzi wa Elimu Maalum pale TAMISEMI wakae na kufanya
tathmini ya hali ilivyo ili walimu wenye taaluma hii waletwe hapa kujaza
mapengo yaliyopo,” alisema.
“Suala
la wataalamu wa physiotherapy na speech therapy itabidi
Naibu Waziri Mavunde afuatilie Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuona
watapatikanaje,” alisema.
Mapema, akitoa taarifa ya kituo hicho, Mkuu wa kituo
cha Miyuji Cheshire Home, Sista Bertha Ligoha alisema kituo hicho chenye uwezo
wa kutunza watoto 40, hivi sasa kina watoto 28 ambao kati yao 19 ni wa kiume na
tisa ni wa kike.
Alisema
kituo hicho kilichoanzishwa mwaka 1987, kimeshapokea watoto 442 ambao kati yao
165 ni wa kike na 477 ni wa kiume. Alisema hivi sasa kituo kina walimu wawili
tu (mmoja yupo na mwingine yuko masomoni) na kinahitaji walimu sita zaidi.
Aliishukuru
Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuwapatia vitanda 40 na pia wabunge na
Mawaziri ambao walichanga fedha na kuwanunulia magodoro 80.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya kituo hicho, Bw. Peter
Mavunde alisema wanakabiliwa na changamoto nyingine zikiwemo ukosefu wa vyanzo
vya uhakika vya mapato vya kuendeshea kituo hicho, upungufu wa walimu na
ukosefu wa gari la kupeleka watoto kwenye matibabu pindi wanapozidiwa.
“Tunakabiliwa
na changamoto kubwa ya kupata fedha za kuwalipa wahudumu na walezi. Tulipoingia
tulikuta wanalipwa sh.45,000 kwa mwezi, tukajipigapiga hadi wakaweza kulipwa
sh. 60,000 kwa mwezi. Tunatamani tufikishe kiwango cha sh. 100,000 lakini hali
ni ngumu kwetu,” alisema.
Alisema
wanahitaji pia vifaa vya mazoezi kwa watoto hao na kuongeza kuwa wana shida ya
kupata ulinzi wa eneo la kituo hicho kwa sababu makampuni ya ulinzi yanayataka
wawepo walinzi watatu katika eneo hilo na kila mmoja alipwe sh.180,000.
Hafla
hiyo fupi ilihudhuriwa na Naibu Waziri (OWM) Kazi, Ajira na Vijana, Bw. Anthony
Mavunde, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, Mwenyekiti wa Bodi ya
Kituo, Mzee Peter A. Mavunde, Mwakilishi wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki
la Dodoma, Paroko wa Kanisa Kuu Dodoma, Padre Onesmo Wisi, Wajumbe wa Bodi ya
Kituo na watendaji kutoka Jiji la Dodoma.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKU
S. L. P. 980,
41193 – DODOMA
JUMATANO, OKTOBA 3, 2018.
No comments:
Post a Comment