Saturday, October 13, 2018

DKT TIZEBA AAGIZA WATAALAMU WA TUME YA UMWAGILIAJI KUZURU IRINGA KUKAGUA MFEREJI WA UMWAGILIAJI

Waziri wa Kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba akikagua mfereji wa maji wa Mkombozi na Mboliboli Tarafa ya Pawaga Mkoani Iringa kwa ajili ya umwagiliaji wa mashamba ya mpunga katika ziara ya kikazi ya kukagua hali ya upatikanaji wa mbolea katika mikoa ya Nyanda za juu kusini Jana tarehe 12 Octoba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal, WK)
Waziri wa Kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba akikagua mashamba ya mpunga alipotembelea Tarafa ya Pawaga Mkoani Iringa katika ziara ya kikazi ya kukagua hali ya upatikanaji wa mbolea katika mikoa ya Nyanda za juu kusini jana tarehe 12 Octoba 2018.
Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe Richard Kasesela akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Iringa kukagua hali ya upatikanaji wa mbolea kuelekea msimu wa kilimo wa mwaka 2018/2019.

Na Mathias Canal-WK, Iringa

Waziri wa Kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba amewaagiza wataalamu wa umwagiliaji kuzuru Tarafa ya Pawaga ili kutembelea na kukagua mfereji wa maji wa Mkombozi na Mboliboli Tarafa ya Pawaga ili kuanzisha skimu ya umwagiliaji.

Waziri Tizeba ametoa agizo hilo Jana tarehe 13 Octoba 2018 wakati alipotembela eneo la mashamba ya mpunga wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Iringa ya kukagua hali ya upatikanaji wa mbolea katika mikoa ya Nyanda za juu kusini.

Alisema kuwa mfereji huo unaohudumia wakulima wa mpunga katika vijiji vya mboliboli, Usolanga, Mbugani na Mkumbwani unapaswa kuwekewa mkakati wa haraka ili kujengwa skimu ya umwagiliaji kwa ajili ya mashamba ya wakulima yanayotajwa kuwa na ukubwa wa hekari 11,000.

"Kwa bahati nzuri Tume ya umwagiliaji sasa rasmi imehamishiwa kwangu haina hata siku tano nitawasimamia kweli kweli ili kuwa na matokeo makubwa na ya haraka kwenye kilimo ambacho ndicho mkombozi wa mkulima" Alikaririwa Dkt Tizeba

Aidha, aliwashauri wakulima katika Tarafa hiyo ya Pawaga kuingia katika kilimo cha pamoja ili pindi wanapovuna waweza kuuza kwa pamoja jambo litakalowafanya kuwa na maamuzi ya kupanga bei waitakayo ya Mazao.

Waziri Tizeba ameitaka Tume ya umwagiliaji kufanya uhakiki wa maeneo yote ya mashamba hayo ya wakulima kwa kuyapima kabla ya kuingia katika kilimo cha pamoja ikiwa ni pamoja na kuainisha gharama za ukamilifu wa mfereji huo wa Mkombozi na Mboliboli.

Alisema kuwa faida ya kulima kwa pamoja wakulima wanapata fursa ya kukopeshwa kirahisi na Mabenki kuliko kufanya kuomba mkopo kwa mkulima mmoja mmoja kwani masharti yake yanakuwa magumu zaidi. 

Kadhalika, Waziri Tizeba amemuagiza Mshauri wa Kilimo wa Mkoa wa Iringa Bi Grace Macha kuanisha uhitaji wa mbegu katika Mkoa huo ili taarifa zitolewe haraka kwa Wakala wa Taifa wa Mbegu (ASA) ili waweze kutoa mbegu punde msimu unapoanza.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment