Friday, October 12, 2018

“UMUHIMU WA MBOLEA NI PALE INAPOMFIKIA MKULIMA SHAMBANI SIO KUWA GHALANI’ DKT TIZEBA

Waziri wa Kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba akizungumza na wanachama wa chama cha Tuungane wakulima Interpises katika kijiji cha Mbugani kilichopo kata ya Itunundu Mkoani Iringa katika ziara ya kikazi ya kukagua hali ya upatikanaji wa mbolea katika mikoa ya Nyanda za juu kusini leo tarehe 12 Octoba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-WK)
Waziri wa Kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba akikagua mfereji wa maji wa Mkombozi na Mboliboli Tarafa ya Pawaga Mkoani Iringa kwa ajili ya umwagiliaji wa mashamba ya mpunga katika ziara ya kikazi ya kukagua hali ya upatikanaji wa mbolea katika mikoa ya Nyanda za juu kusini leo tarehe 12 Octoba 2018.
Waziri wa Kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba akikagua mashamba ya mpunga alipotembelea Tarafa ya Pawaga Mkoani Iringa katika ziara ya kikazi ya kukagua hali ya upatikanaji wa mbolea katika mikoa ya Nyanda za juu kusini leo tarehe 12 Octoba 2018.
Waziri wa Kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba akikagua Ghala la kuhifadhi mpunga la Tuungane Wakulima Inteprises wakati akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Iringa kukagua hali ya upatikanaji wa mbolea katika mikoa ya Nyanda za juu kusini leo tarehe 12 Octoba 2018.
Waziri wa Kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba akikagua mashine ya kukoboa mpunga ya Chama cha Tuungane Wakulima Inteprises wakati akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Iringa kukagua hali ya upatikanaji wa mbolea katika mikoa ya Nyanda za juu kusini leo tarehe 12 Octoba 2018.

Na Mathias Canal-WK, Iringa

SERIKALI imesema itahakikisha mbolea inawafikia wakulima kwa wakati kabla ya kuanza msimu wa kilimo wa mwaka 2018/19 kwani umuhimu wa mbolea ni pale inapowafikia wakulima shambani sio kuhifadhiwa ghalani.

Katika msimu ujao Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa wakulima wanapata mbolea na pembejeo nyingine katika maeneo yao wakati wote wanapohitaji ili kuondoa adha ya muda mrefu ya mbolea kuchelewa kuwafikia wakulima kwa wakati.

Waziri wa Kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba ametoa kauli hiyo leo tarehe 12 Octoba 2018 wakati akizungumza na wanachama wa chama cha Tuungane wakulima Interpises akiwa katika ziara ya kikazi kata ya Itunundu Mkoani Iringa kukagua hali ya upatikanaji wa mbolea katika mikoa ya Nyanda za juu kusini.

Dkt. Tizeba amesema kuwa ili kuboresha usambazaji wa pembejeo kwa wakulima katika msimu wa mwaka 2017/2018 mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (Bulk Procurement system- BPS) umeongeza upatikanaji wa mbolea kwa wingi, bei nafuu na wakati.

Aidha, kwa kutumia utaratibu huo bei za mbolea aina ya DAP na UREA zimepungua kwa wastani wa asilimia 30.

Akifafanua zaidi, Dkt Tizeba alisema kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) inaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na pindi ukiukwaji wa bei elekezi unapobainika hatua stahiki zinachukuliwa kwa wahusika.

” Endapo kama kuna mtu atapandisha gharama za mbolea kwa kupandisha bei maradufu zaidi ya bei elekezi serikali itamchukulia hatua haraka za kisheria atakayebainika ” Alikaririwa Dkt Tizeba

Katika kuimarisha sekta ya kilimo serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuimarisha kilimo kwa kuwekeza katika pembejeo, mbolea na zana zinazoweza kuikuza sekta ya kilimo ili iweze kuchochea uchumi wa viwanda.

Kadhalika, Waziri Tizeba amewatoa hofu wakulima nchini kuwa kuna akiba ya mboleaya awali isiyopungua Tani 80,000 kwa ajili ya kupandia.

MWISHO

No comments:

Post a Comment