Rais Paul Kagame wa Rwanda
Mhe Dkt Charles Tizeba, Waziri wa kilimo Tanzania
Na Mathias Canal, Kigali-Rwanda
Viongozi wa nchi za Afrika waliokutana katika mji mkuu wa Rwanda,
Mjini Kigali wamekubaliana kuboresha hali ya sekta ya kilimo na kuongeza
kiwango cha usalama wa chakula barani humo ikiwemo kupambana na kadhia ya upotevu wa chakula jambo ambalo bado ni changamoto kubwa
inayohitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Viongozi hao wamefikia makubaliano hayo katika kongamano la saba
la Jukwaa la Mapinduzi ya Kijani ya kilimo na usalama wa chakula ambalo
lilianza siku ya Jumatano ya tarehe 5 mwezi huu wa Septemba 2018 mjini Kigali.
Rais Paul Kagame wa Rwanda akihutubia
washiriki wakati Wa kufunga kongamano la Mapinduzi ya kijani Barani Afrika (AGRF)
lililofanyika Mjini Kigali likiongozwa na kauli mbiu isemayo "Ongoza, Pima, Kua: Kuwezesha njia mpya za kubadilisha
wakulima wadogo kufanya kilimo biashara endelevu" amesema kuna ulazima wa kufanyika mageuzi na
harakati katika sekta ya kilimo kwa ajili ya kuboresha hali ya kiuchumi na
kijamii ya bara la Afrika.
Amefafanua kuwa kuinua
kiwango cha uzalishaji katika sekta ya kilimo, mbali na kuongeza usalama wa
chakula kutapunguza pia kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana na akina mama
wa Kiafrika.
Rais Paul Kagame wa
Rwanda ametilia mkazo sekta binafsi kuongeza kiwango cha uwekezaji na kueleza
kuwa kutengwa bajeti kwa ajili ya kuboresha ubora wa mbegu na kuimarisha sekta
ya kilimo kutaleta ustawi kwa maisha ya Waafrika.
Washiriki wa kongamano
la Jukwaa la Mapinduzi ya Kijani wameahidi pia kuchukua hatua za kisiasa na
kiuchumi zinazohitajika ikiwemo kudhamini bajeti kwa ajili ya utumiaji
teknolojia ya kisasa kwa lengo la kuleta mageuzi ya dhati katika sekta ya
kilimo na chakula na hatimaye kufanikisha Mapinduzi ya Kijani barani Afrika
Jukwaa la Mapinduzi ya Kijani (AGRF) limeandaa
kongamano kwa viongozi wa Afrika na kuendesha mpangilio wa kukuza
uwekezaji na sera ya kuongeza uzalishaji wa kilimo na ukuaji wa kipato kwa
wakulima wa Afrika.
Watu zaidi
ya 2000 wakiwemo wataalamu wa kilimo, viongozi wa serikali na maafisa
waandamizi kutoka nchi 40 walioshiriki katika mkutano huo wa siku tano
wameahidi kutumia fursa hiyo na kutoa dola milioni kadhaa za kimarekani katika
uwekezaji mpya kwa wakulima wa Afrika na biashara zinazohusiana na kilimo.
Waziri wa
kilimo nchini Tanzania Mhe Dkt Charles Tizeba (Mb) amesema mageuzi mapya
yanahitajika katika sekta ya kilimo ili kuhimiza Afrika kuondokana na umaskini
uliokithiri na kiwango cha chini cha uwekezaji.
Dkt Tizeba
amesisitiza kuwa nchi ya Tanzania, kama
zilivyo nchi zingine za Afrika, husumbuliwa na matatizo makubwa kadhaa ya
uhifadhi chakula ambayo hupelekea upotevu wa rasilimali uzalishaji kama
hazitashughulikiwa ipasavyo.
Aliyataja matatizo hayo kuwa ni pamoja na Teknolojia duni, hasa
katika uvunaji na uhifadhi wa chakula baada ya mavuno, Ujuzi hafifu wa mnyororo
wa matukio baada ya uvunaji, na Uhaba wa masoko na miundimbinu mibovu, kwani
wazalishaji na wanunuzi hawana mawasiliano mazuri kutokana na uhaba wa taarifa
na barabara zisizopitika katika misimu yote.
Aidha, matatizo mengine ni pamoja na Uhaba wa fedha katika
shughuli mbalimbali baada ya uvunaji, Ushiriki hafifu wa sekta binafsi katika
kuwekeza katika mchakato wa shughuli mbalimbali baada ya uvunaji, na katika
hatua ya uhifadhi, upotevu hutokana na magonjwa na wadudu ambao husababisha
upotevu katika ubora na kiasi.
Aliongeza kuwa upotevu wa chakula baada ya uvunaji umeendelea
kuwa tatizo kubwa siyo tu katika chakula lakini pia katika malighafi kwa
maendeleo ya viwanda huku akizitaja juhudi zilizofanywa na serekali ya Tanzania
kupunguza upotevu wa chakula ambazo ni pamoja na kushirikiana na wadau
mbalimbali wa maendelea, taasisi za kimataifa kama vile Bill and Melinda Gates
foundation, HELVETAS Swiss Inter Cooperation Agency, Rockefeller foundation,
AGRA, shirika la chakula duniani, mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo
yameboresha kwa kiasi kikubwa teknolojia ya uhifadhi kama vile mifuko ya
plastiki ya kuhifadhia nafaka ambayo imeonesha kuwa na mafanikio makubwa sana
kwa kuzuia wadudu waharibifu kupenya na kushambulia nafaka.
Pia Kuanzishwa kwa mfumo wa ubadilishanaji bidhaa Tanzania.
Kuweka mazao katika masoko yaonekanayo ili kurahisisha uuzaji na kupunguza
upoteaji wa bidhaa za kilimo. Chini ya mradi huu mazao yatatunzwa chini ya
mfumo vikundi vya wakulima na kuuzwa moja kwa moja katika mfumo wa
kubadilishana mazao.
Kongamano hilo limefikia ukomo hapo jana tarehe 8 Septemba
2018 baada ya kujadili maswala ya kilimo kwa siku nne mfululizo lilihudhuriwa
pia na viongozi wengine wa Afrika akiwemo Rais wa Ghana Mhe Nana Addo Dankwa
Akufo Addo, Makamu wa Rais wa Kenya Mhe William Ruto, Waziri Mkuu wa Gabon Mhe
Emmanuel Issoze-Ngondet sambamba na Waziri Mkuu mstaafu wa Uingereza Mhe Tony
Blair.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment