Saturday, August 4, 2018

WAPINZANI KUKIMBILIA CCM, NINI CHA AJABU?


Na Shabani Shabani

Tarehe 17 Desemba 2011 Chama Cha NCCR Mageuzi kupitia Halmashauri Kuu ya Chama hicho kilimvua uanachama wa NCCR Mageuzi Ndg.David Zacharia Kafulila aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, angepoteza ubunge na tungerudi kwenye uchaguzi na gharama zingekuwepo za uchaguzi, mahakama ndio iliokoa jahazi, wapinzani wa nchi hii walisema ni demokrasia.

Tarehe 10 septemba 2012 Kamati Kuu ya chadema ili wavua uanachama madiwani wawili katika jiji la Mwanza ambao ni Bwana Adamu  Chagulani wa Kata ya Igoma na Bwana Henry Matata wa Kata ya Kitangiri, sio kwa sababu walishindwa kuwahudumia wananchi ni kwa sababu ya migogoro yao wenyewe ndani ya Chadema, Kipindi hicho Chadema hawakuuliza gharama za kurudia uchaguzi wa marudio, wanachadema walishangilia na wapinzani wa nchi hii waliita ni demokrasia.

Tarehe 11 Mei 2015 Chadema waitangaza kumvua uanachama wa Chama hicho Bwana Zitto Zuberi Kabwe aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, baada ya wiki moja Bwana Zitto alijiuzulu  ubunge wa Jimbo, katika kipindi chochote  hadi ulipowadia uchaguzi Mkuu 2015 wananchi wa Kigoma Kaskazini hawakuwa na muwakilishi kwa sababu ya siasa zenye migogoro, chuki na uzandiki za wapinzani. Wapinzani waliita ni demokrasia.

Tarehe 30 Octoba 2017 Bwana Lazaro Samuel Nyarandu aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini kupitia CCM alitangaza kujivua uanachama wa CCM, kujiuzulu ubunge na siku chache baadae alijiunga na Chadema, Chadema walishangilia Sana waliwang'ong'a CCM kwa Kila neno, hawakusema demokrasia inaharibiwa walifurahia sana na wapinzani waliita ndio demokrasia.

Kimsingi naomba ni wafumbue macho ndugu zangu wananchi. Serikali ya Magufuli ndani ya miaka miwili  imejenga  vituo vya afya 208 nchi nzima uchaguzi wa marudio ulikuwepo na upo. Serikali ya Magufuli inajenga Reli ya Kiwango cha Kimataifa na sasa tuta la reli linakaribia ihumwe Dodoma uchaguzi wa marudio ulikuwepo na upo.

Serikali ya Magufuli imeendelea kusambaza umeme vijijini na sasa vijiji zaidi ya 12000 vimeunganishwa na umeme, uchaguzi wa marudio ulikuwepo na upo.

Hoja ni kuwa kila kitu kwenye Serikali kina bajeti yake, Serikali inaendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora za maji safi na salama, elimu, miundo mbinu ya usafiri na usafirishaji, afya na jambo la  utawala bora linalohusisha chaguzi za kidemokrasia ikiwemo chaguzi za marudio nalo lina bajeti yake , ruzuku za vyama vya siasa na taasisi zinazosimamia maadili ya viongozi wa umma, hii yote ni kuendelea kuimarisha demokrasia ya nchi yetu. Serikali ya Magufuli imejipanga kila kona.

Binafsi sioni sababu ya kelele zote za sasa za wapinzani,  hakuna jambo la ajabu, hakuna uvunjiifu wa sheria na wala hakuna matumizi mabaya ya kodi za wananchi ndio demokrasia.

Kama walivyoondoka awali ndivyo wanavyokuja CCM na zaidi. Wanaohamia CCM wamevutiwa, wamewiwa na wameguswa na  Mageuzi Makubwa ndani ya CCM, kuzidi kuimarika kwa CCM kama taasisi yenye muelekeo chanya na utendaji wa kihistoria wa  Rais John Pombe Joseph Magufuli, umewafanya waone hakuna haja ya kukaa nje ya historia ya mageuzi makubwa ya nchi yetu, nje ya CCM na nje ya  jahazi la uhakika. Ni hayo tu.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment