Saturday, August 4, 2018

MFANYABIASHARA AMZAWADIA RC MTAKA KUTAMBUA MCHANGO WAKE KWENYE MAENDELEO YA UCHUMI WA SIMIYU

Elizabeth Mlanda (kulia) mke wa Mfanyabiashara Clement Mlanda akimkabidhi Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka bahasha yenye fedha  kama shukrani yake kwa kutambua mchango wa Mkuu huyo wa Mkoa katika maendeleo ya Uchumi wa mkoa wa Simiyu

 Elizabeth Mlanda (kulia) mke wa Mfanyabiashara Clement Mlanda wa Mjini Bariadi akimkabidhi Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka  zawadi ya unga wa ngano, mafuta ya kula na sukari , Agosti 04,  2018,' Mjini Bariadi  ikiwa ni shukrani yake kwa kutambua mchango wa Mkuu huyo wa Mkoa katika maendeleo ya Uchumi wa mkoa wa Simiyu

Na Stella Kalinga, Simiyu

Bibi. Elizabeth Mlanda Mke wa Mfanyabiashara Mkubwa wa Mjini Bariadi mkoani Simiyu, Bw. Clement Mlanda Shigugulu ambaye anamiliki Hotel ya MS COMPLEX  amemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka  zawadi ya fedha taslimu (kiasi ambacho hakikutajwa),  kilo 50 za sukari, kilo 25 za unga wa ngano na lita 40 za mafuta ya kula, ikiwa ni shukrani kwake kwa namna uongozi wake ulivyochangia kuufungua mkoa wa Simiyu kiuchumi na kuwawezesha wafanyabiashara wa mkoa huo kufanya biashara katika nyakati mbalimbali.

Amesema kupitia uongozi wa Mhe. Mtaka kumekuwa na matukio makubwa  yanayochangia kuongezeka kwa mzunguko wa biashara mkoani Simiyu, ikiwemo Maonesho ya Kilimo na Sherehe za wakulima Nanenane ambayo yamewaleta watu kutoka sehemu mbalimbali hivyo kuwanufaiisha wafanyabiashara wa Simiyu hususani wamiliki wa hoteli na nyumba za kulala wageni.

" Jana nilienda Uwanja wa Nanenane nikakuta mambo mazuri, nilipokuja hotelini kwetu nako nikakuta watu wamejaa, nikamuuliza baba(mume wake) kuwa tutampa nini huyu Mkuu wa mkoa wetu kwa mambo mazuri anayotufanyia ya kutuletea maendeleo hivi na kutuletea heshima mkoa wetu mpya wa Simiyu " alisema.

"Nilimwambia mume wangu nitampa zawadi yoyote kumshukuru ili moyo wangu ufurahi, Nimemletea  mafuta ndoo mbili za lita 20, sukari kilo 50,unga wa ngano kilo 25, nampongeza sana na Mungu amzidishie aendelee na moyo huu wa kutuletea maendeleo Mkoa wetu mpya wa Simiyu" alisisitiza Bibi. Elizabeth.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amemshukuru Mfanyabiashara huyo kwa zawadi hizo na akaeleza kuwa itakuwa ni kumbukumbu katika maisha yake huku akifafanunua kuwa kazi anayoifanya ni wajibu wake katika kuwaletea wananchi. 

Ameongeza kuwa mikoa mingi imekuwa kiuchumi kutokana mchango wa viongozi waliopo, waliopita kwa kushirikiana na wananchi pamoja na wafanyabiashara.

"Maendeleo ndiyo nia ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kama ilivyokuwa kwa Marais, mawaziri waliopita, na kwa mkoa wa Simiyu mchango wangu unaendeleza kile walichofanya wakuu wenzangu wa mkoa walionitangulia, Marehemu Mabiti na baba yangu Elaston Mbwilo"'alisema.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment