Sunday, August 5, 2018

DKT TIZEBA AAGIZA WAKAGUZI WA VIUATILIFU KULINDA MASLAHI YA TAIFA

Mgeni rasmi-Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akizungumza wakati wa mkutano wa ufunguzi wa mafunzo ya wakaguzi wa viuatilifu kwenye hafla iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha kilimo (SUA) Mkoani Morogoro leo Tarehe 5 Agosti 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akisisitiza ufanisi kazini wakati akizungumza kwenye mkutano wa ufunguzi wa mafunzo ya wakaguzi wa viuatilifu kwenye hafla iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha kilimo (SUA) Mkoani Morogoro leo Tarehe 5 Agosti 2018.
Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu katika Ukanda wa Kitropiki (Tropical Pesticide Research Institute - TPRI) Dkt Margaret Mollel akitoa taarifa ya mafunzo ya wakaguzi wa viuatilifu mbele ya mgeni rasmi Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba kwenye hafla iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha kilimo (SUA) Mkoani Morogoro leo Tarehe 5 Agosti 2018.

Na Mathias Canal, WK-Morogoro

Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba leo tarehe 5 Agosti 2018 amefungua rasmi mafunzo ya wakaguzi wa viuatilifu yaani mimea na mazao katika hafla iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha kilimo (SUA) Mkoani Morogoro ambapo asilimia 99 ya washiriki wanatoka katika vituo vya ukaguzi wa mazao mipakani vikiwemo vya nchi kavu, bandarini na viwanja vya ndege.

Katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu katika Ukanda wa Kitropiki (Tropical Pesticide Research Institute - TPRI), Waziri Dkt Tizeba ameagiza washiriki hao Kulinda maslahi ya wakulima, walaji na Taifa kwa ujumla dhidi ya wafanyabiashara wachache wa viuatilifu wanaotaka kutajirika kwa kutuletea viuatilifu vilivyo chini ya kiwango.

Waziri huyo anayeshughulikia sekta ya kilimo nchini ameyasema hayo kwa msisitizo mkubwa huku akiwataka kutekeleza wajibu wao wa ukaguzi wa viatilifu kwa umakini, uaminifu na uadilifu mkubwa kwa kutumia Sheria na Kanuni zilizopo.

Amesisitiza kuwa wataalamu hao wanapaswa kuitetea maslahi ya nchi pale inapohitajika kwa kutumia kwa umakini mkubwa kwa utashi wa Sheria na Kanuni zinazotakiwa ikiwa ni pamoja na taratibu nyingine za kisheria katika kuhusisha watumishi wengine wa Serikali kama waendesha mashtaka wa Serikali na askari.

Pia, aliwataka Wakaguzi kutoka Makao Makuu ya Wizara na Taasisi ya TPRI kuangalia namna ya kuunganisha shughuli zinazofanywa kati ya Kitengo cha afya ya mimea (PHS) na TPRI katika kuwasimamia na kuwaongoza wakaguzi kutoka katika vituo vyetu vya mipakani ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi na uadilifu kwa kuwapatia vitendea kazi pale fursa zinapopatikana kwa kuzingatia mahitaji.

Katika hatua nyingine Waziri Tizeba ameelekeza uongozi wa TPRI pamoja na PHS kuhakikisha katika mafunzo hayo wanawapatia taarifa muhimu za orodha ya viuatilifu vilivyosajiliwa kote nchini ili kurahisisha utendaji timilifu katika kutekeleza majukumu yao.

Amewasisitiza watumishi hao kushirikiana na watumishi wengine wa Serikali kutoka taasisi mbalimbali walio katika vituo vya ukaguzi mipakani ili kuongeza ufanisi wa kazi na kuwahudumia wadau kwa wakati kama ilivyoelekezwa katika mafunzo hayo.

Aidha, ameipongeza TPRI kwa juhudi wanazochukua za kuongeza idadi ya wakaguzi wa viuatilifu kupitia mafunzo ambapo ameeleza kuwa mafunzo hayo yatawezesha wakulima kuweza kudhibiti visumbufu vya mazao kwa kutumia viuatilifu sahihi na hivyo kulinda afya za walaji, viumbe wengine na mazingira, na kuiwezesha Tanzania kukidhi matakwa ya mikataba ya kimataifa ya udhibiti wa viuatilifu na visumbufu vya mimea na mazao.

Sambamba na hayo aliongeza kuwa kwa kutambua changamoto ya tija ndogo katika uzalishaji, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 Ibara ya 22 inayosimamiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Dkt John Pombe Joseph Magufuli, inaielekeza Serikali kufanya kilimo chenye tija kwa kuzingatia matumizi sahihi ya teknolojia (zikiwemo za udhibiti wa visumbufu vya mazao) ili kuongeza malighafi za viwanda vya kuongeza thamani ya mazao na ajira.

Alisema, Mpango wa kuendeleza sekta ya kilimo ASDP II umeainisha umuhimu wa matumizi ya Udhibiti Husishi wa Visumbufu vya Mazao (Integrated Pest Management - IPM) vikiwemo viuatilifu katika kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya kilimo.

“Hivyo, ni matumaini yangu kuwa usimamizi na udhibiti wa uingizaji na matumizi sahihi ya viuatilifu itawezesha kufikiwa kwa malengo ya nchi ya kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya kilimo na kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda” Alikaririwa Mhe Dkt Tizeba

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu katika Ukanda wa Kitropiki (Tropical Pesticide Research Institute - TPRI)  ambaye pia ni makamu Mkuu wa Chuo kikuu cha Kilimo (SUA) Prof Raphael Chibunda amemshukuru Waziri huyo wa kilimo kwa kufungua mafunzo hayo ya siku 14 ambapo alisema kuhusu changamoto ya wakaguzi wa viutilifu na visumbufu vya mimea ni Chuo hicho cha kilimo kuanzisha Shahada ya Usimamizi wa kinga ya mimea (Plant Protection Management).

MWISHO.

No comments:

Post a Comment