Sunday, July 22, 2018

Wananchi wa maeneo yenye madini watakiwa kuchangamkia fursa

Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko, viongozi mbalimbali wilayani Tunduru pamoja na wachimbaji wadogo wakiangalia moja ya eneo la machimbo ya Mbesa yanapopatikana madini ya almasi.

Na George Binagi-Ruvuma

Wananchi wanaoishi katika maeneo yenye rasilimali madini hapa nchini wametakiwa kuitumia vyema fursa hiyo kwa kuzalisha bidhaa mbalimbali ili kuwauzia wawekezaji katika maeneo hayo.

Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko aliyasema hayo Julai 20, 2018 wakati akizungumza na wananchi na wachimbaji wadogo wa madini ya shaba katika machimbo ya Mbesa yaliyopo Tunduru mkoani Ruvuma.

Akitolea mfano machimbo ya Mbesa, Biteko alisema wananchi wanapaswa kutumia vyema fursa za uwepo wa machimbo hayo na kuzalisha kwa wingi bidhaa za kilimo na ufugaji kwani uhakika wa soko utakuwepo kupitia wawekezaji.

Aidha, aliwataka wawekezaji katika sekta ya madini kuhakikisha wananunua bidhaa za chakula kutoka kwa wenyeji yalipo madini ili kukuza uchumi wao kupitia fursa ya madini katika maeneo yao.

“Kama mnataka kununu bidhaa mfano chakula, nyanya, mbogamboga na nyama, biashara yote hiyo lazima ifanywe na wenyeji na siyo kutoka mahali pengine”. Alisisitiza Mhe Biteko na kuongeza kuwa anataka kuona wananchi wa Mbesa wakiwemo akina mama na vijana wakilima na kufuga kwa wingi kwa sababu ya uhakika wa soko.

Pia aliwataka wananchi na mwekezaji kutoka kampuni ya Metalica Comodity Corperation (MCC), kushirikiana vyema ili kuondokana na migogoro isiyo ya lazima ambapo aliitaka kampuni hiyo kulipa fidia stahiki pale itakapohitajika na wanachi wawe tayari kuruhusu uwekezaji kufanyika katika maeneo yao.

Naye Mkurugenzi Mwenza wa kampuni ya Metalica Comodity Corperation (MCC), Ndg Benson Gabriel alisema kampuni hiyo imeanza utafiti wa madini ya shaba awamu ya pili katika machimbo ya Mbesa na utakapokamilika itaanza rasmi shughuli zake kwa kuzingatia sheria ikiwemo kulipa kodi zote za serikali pamoja na kuhakikisha wananchi wananufaika na madini hayo.

Awali wakazi wa Kijiji cha Mbesa walihoji namna watakavyonufaika na uwepo wa machimbo ya almasi katika eneo lao na kutaka kampuni ya Metalica Comodity Corperation (MCC) kuwapa kipaumbele cha ajira na shughuli mbalimbali pindi itakapoanza rasmi shughuli zake.
Naibu Waziri wa Madini Mhe.Doto Biteko akiangaliwa mawe ya almasi katika machimbo ya Mbesa wilayani Tunduru
Mawe yenye madini ya almasi
Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Biteko (wa pili kulia) akimsikiliza Mkurugenzi Mwenza wa kampuni ya MCC (kulia) inayotarajia kuanza uchimbaji madini katika machimbo hayo. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya Tunduru Mhe Juma Homera na kushoto ni Mkurugenzi Mwenza kampuni ya MCC, Benson Mwakilembe
Mkuu wa Wilaya Tunduru Mhe.Juma Homera akifafanua namna Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/20 ya Chama cha Mapinduzi CCM inavyosisitiza serikali kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali madini
Naibu Waziri wa Madini Mhe.Doto Biteko akiangalia eneo linalodaiwa kuwa na madini ya vito katika mto Muhuesi wilayani Tunduru. Serikali imezuia shughuli za uchimbaji katika eneo hilo kwa kuwa ni hifadhi ya mto
Naibu Waziri wa Madini Mhe.Doto Biteko (katikati) akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya Tunduru Mhe.Juma Homera (kulia) pamoja na Afisa Madini Mkazi wilayani Tunduru Abraham Nkya (kushoto) alipopita kuangalia eneo la mto Muhuesi wilayani Tunduru.

No comments:

Post a Comment