Sunday, July 22, 2018

Wafanyabishara watakiwa kuongeza thamani ya madini kabla ya kuyasafirisha

Naibu Waziri wa Madini Mhe.Doto Biteko akizungumza katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya Tunduru mkoani Ruvuma kabla ya kuanza ziara yake wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya Tunduru Mhe.Juma Homera akitoa taarifa ya upatikanaji madini wilayani humu kwa Naibu Waziri wa Madini Mhe.Doto Biteko.

Na George Binagi-BMG

Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko amewataka wafanyabiashara wa madini nchini kufunga mashine za kukatia madini katika mkoa husika wanaonunua madini kama sheria inavyoelekeza.

Mhe Biteko alitoa kauli hiyo Julai 19, 2018 wakati akizungumza na wafanyabiashara wa madini ya vito katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.

Aidha Mhe Biteko alisikitishwa na hatua ya baadhi ya wafanyabiashara wanaonunua madini ya vito ikiwemo Ruby na Gem Stone wilayani Tunduru kutokuwa na mashine za kukatia madini hayo wilayani humo na badala yake mashine hizo ziko Jijini Dar es salaam.

Alisema sheria ya uwazi na uwajibikaji katika sekta ya uziduaji, kifungu cha 49 inamtaka mfanyabishara wa madini anayetoka nje ya nchi kufungua mashine zisizopungua 30 katika eneo husika analonunulia madini na ikiwa ni mfanyabishara mzawa sharti afunge mashine zisizopungua tano.

Mhe Biteko aliongeza kwamba sheria ya madini ya mwaka 2010 kifungu cha 73 inatamka wazi kwamba kila mmiliki wa leseni ya madini (dealer) lazima ayaongeze thamani madini yake kabla ya kuyasafirisha jambo ambalo linaonekana kukiukwa na wafanyabiashara wengi nchini.

Kutokana na hali hiyo, aliwaagiza wafanyabiashara wote nchini kuhakikisha wanatimiza masharti hayo kwa mujibu wa sheria ndani ya siku 30 baada ya kupewa leseni ambapo alibainisha kwamba wote walioomba leseni za kufanya biashara ya madini wataanza kupewa leseni hizo kabla ya mwezi huu kuisha.

Katika hatua nyingine Mhe Biteko aliwataka watanzania wanaoingia ubia na wawekezaji kutoka nje ya nchi kuhakikisha wanaingia makubaliano yanayowanufaisha kwa mujibu wa sheria badala ya kuingia makubaliano yasiyo na tija kwao ambapo sheria ya madini inatamka wazi kwamba mwananchi mzawa atakayeingia ubia na mwekezaji kutoka nje ya nchi anapaswa kupata hisa zisizopungua asilimia 25.

Akisisitiza kuhusu hilo, Biteko alionyesha kukerwa na hatua ya mmoja wa wazee wilayani Tunduru kuingia ubia na wafanyabiashara wa madini ya vito (Gem Stone) kutoka nchini Sirilanka huku akiwa hakujui hisa zake katika makubaliano hayo na hivyo kuonya juu ya makubaliano (mikataba) ya aina hiyo ambayo yanawanyonya wananchi jambo ambalo serikali haiwezi kulivumilia liendelee.

No comments:

Post a Comment