Monday, July 23, 2018

Wananchi wa kata ya Kinampanda Iramba watoa neno kwa Mwigulu Nchemba

Mbunge wa jimbo la Iramba magharibi mkoa wa Singida Dkt Mwigulu Nchemba akiongea na wananchi wa kata ya Kinampanda kutoa taarifa ya ulipofikia ujenzi wa kituo cha afya ambacho kilikua ni moja ya ahadi zake akiomba ridhaa ya kuongoza jimbo hilo leo.
 Mbunge wa jimbo la Iramba magharibi mkoa wa Singida Dkt Mwigulu Nchemba akikagua ujenzi wa kituo cha Afya  cha kata ya kinampanda kinachojengwa kwa nguvu za wananchi wakishirikiana na mbunge pamoja na serikali kuu, kituo hicho ni cha kwanza  tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika


MBUNGE wa Iramba Magharibi, Dkt Mwigulu Nchemba amesema atahakikisha ujenzi wa kituo cha afya unaoendelea katika Kata ya  Kinampanda kilichopo Wilaya ya Iramba mkoani Singida, unakamilika kwa wakati ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara katani hapo,, Dkt Mwigulu alisema ilikuwa aibu kwa eneo kongwe kama Kinampanda kuliko na taasisisi kongwe kama Chuo cha Ualimu Kinampanda na Sekondari kongwe ya Tumaini  kutokuwa na kituo cha afya huku huduma zikiwa zinapatikana mbali.

Alisema kila wilaya ilipewa fedha za  mradi mmoja wa kituo cha Afya lakini   aliamua  kufanya kampeni maalum ya ujenzi wa kituo hicho cha afya cha Kinampanda uwe na  ramani ya hospitali ya Wilaya sambamba na kituo cha Ndago kilichokuwa na sifa.

"Pongezi kwa serikali kwa msaada wa fedha za ujenzi wa kituo cha afya na jitihada za wananchi wetu kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati. Niliwaomba twende mbio mbio kwa kujenga majengo ya huduma za kawaida ili kufikia masharti ya fedha tulizopewa," alisema Dkt Mwigulu.

Alifafanua kuwa ujenzi huo umefikia katika kupaua ambapo anachangia mabati 200, mbao  na saruji ya kumalizia lengo . Awali Dkt alichangia siment mifuko 500 na nondo miambili ili kuunga mkono juhudi za  wananchi waliopo katika kata ya Kinampanda na wale watakaotumia kituo hicho kupata huduma za afya na kuokoa maisha ya watanzania wengi.

Dkt Mwigulu alitembelea katika kituo hicho ili kuangalia maendeleo  ya ujenzi huo unafadhiliwa na Ofisi ya Mbunge wa jimbo akishirikiana na wananchi ambao wanachangia ujenzi huo.

Naye, Mwenyekiti wa Kijijini cha Kinampanda, Samwel Mhenga alisema tangu uhuru kata ya Kinampanda  hakijawahi kuwa na Kituo cha afya,  lakini historia inaandikwa kwa Mbunge huyo kuona haja ya kujenga  kituo cha afya cha kisasa.

Mhenga alisema kutokana na changamoto za huduma za afya, walikuwa wakiwapeleka wagonjwa hasa wakina mama wajawazito kwenda katika hospitali za Hydum, Ikungi, Singida mjini na Nkinga Tabora kwa ajili ya kujifungua. 

Alisisitiza kuwa kupitia kituo hicho cha afya,  kitasaidia kurahisisha utoaji wa huduma za afya kupunguza vifo vya  wakina mama na watoto.

"Mbunge wetu anayejali afya zetu amesaidia kupata kituo cha afya ili kupunguza changamoto ndio maana nawaambia Nchemba huyu, Nchemba huyu amekuwa akifanya kazi chini ya uwepo wa Mungu. Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, 2020 ni tiki tu," alisema Mhenga.

Mwisho

No comments:

Post a Comment