Na Mathias Canal, Singida
MASHINDANO ya Ikungi Elimu Cup 2017 yanataraji kufika ukomo kwa fainali Disemba 9, 2017 itakayozikutanisha timu za Mampando Fc na Matongo Fc ambazo ndizo zimepenya katika hatua ya makundi na Robo fainali katika mashindano ambayo yamekuwa na muitikio mkubwa na kuibua hamasa katika Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida.
Timu ya Matongo Fc imeingia hatua ya fainali kwa kuirarua Timu ya Ikungi Fc kwa goli 4 kwa 2 kupitia mikwaju ya penati baada ya timu hizo kutoshana nguvu kwa kutoka sare katika kipindi chote ndani ya dakika 90.
Timu ya Mampando Fc yenyewe iliwatumia vizuri washambulizi wake na hatimaye kuwavumisha nje ya mashindano timu ya Mwasutianga Fc kwa goli 3 kwa 1 kunako dakika 90 za mchezo.
Hata hivyo kabla ya mchezo wa fainali kutakuwa na mchezo wa awali ambao ni hatua ya kutafuta mshindi wa nafasi ya tatu bora ambapo mchezo huo utakuwa kati ya Ikungi Fc na Mwasutianga Fc Disemba 1, 2017 huku mechi ya kutafuta mshindi wa tano na wa sita ikiwa no kati ya Choda Fc na Maswea Fc.
Akizungumzia mashindano ya “IKUNGI ELIMU CUP 2017” wakati alipohojiwa na mtandao wa www.wazo-huru.blogspot.com Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida Mhe Miraji Jumanne Mtaturu alisema kuwa mashindano hayo yalianza kurindima Siku ya Jumamosi Agosti 19 mwaka huu ambapo mpaka yanafika ukomo yatakuwa yamewafikia zaidi ya wananchi 5000.
Mashindano hayo yalifunguliwa na Mgeni Rasmi-Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida na tangu awali timu mbalimbali kutoka Kata zote 28 na vijiji 101 katika Wilaya ya hiyo zimechuana vikali.
Mashindano ya "IKUNGI ELIMU CUP 2017" yakiongozwa na kauli mbiu ya “ Changia, Boresha Elimu Ikungi" yaliambatana na zoezi la ufyatuaji matofali ambapo kila Kata ilitakiwa kufyatua matofali 10,000 ikiwa ni sehemu ya kuhimiza utatuzi wa Changamoto mbalimbali Wilayani Ikungi ikiwemo Upungufu wa nyumba za walimu, Vyumba vya madarasa, Ofisi za walimu, Maabara, Thamani mbalimbali, Matundu ya vyoo vya walimu na wanafunzi.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu ambaye pia ni mlezi wa mfuko wa Elimu amewasihi wananchi na wadau kuchangia fedha au thamani zozote kadri wawezavyo ili kufanikisha kuboresha miundombinu ya elimu katika wilaya hiyo.
"Uzinduzi wa ufyatuaji matofali umeanzishwa kwa ajili ya majukumu muhimu kusaidia sekta ya Elimu ikiwa ni pamoja na kuendeleza ujenzi wa maabara uliokwama toka mwaka 2009" Alikaririwa Mhe Mtaturu
Kuanza kwa mashindano hayo ya “IKUNGI ELIMU CUP 2017” ni utekelezaji wa Wazo la kuanzisha Mfuko wa Elimu lilitokana na kikao cha wadau wa elimu kilichoitishwa na Mkuu huyo wa Wilaya mwezi Disemba, 2016 na kubaini changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ikiwemo kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi kuanzia elimu ya msingi mpaka Sekondari.
Mwisho
No comments:
Post a Comment