Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula leo amezindua kiwanda kidogo cha uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo nguo, sabuni, mapambo na keki kilichopo shule ya sekondari ya wasichana Bwiru kilichoanzishwa kwa ushirikiano na taasisi isiyo ya Serikali ya Kivulini inayotetea haki za mwanamke na mapambano ya unyanyasaji wa kijinsia
Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo Mhe Dkt Angeline Mabula mbali na kuwapongeza kwa kuitekeleza kwa vitendo dhana ya Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli ya kuwa na nchi ya viwanda ameziasa shule nyengine zilizopo ndani ya Jimbo lake kuiga mfano huo wa kuwa na viwanda vidogo vidogo vitakavyosaidia kupunguza tatizo la ajira na kuwafanya wanafunzi kuwa na shughuli za kufanya mara baada ya kumaliza shule hivyo kutojiingiza katika mambo yasiyofaa kwa jamii kwa kisingizio cha kukosa shughuli za kufanya huku akikemea mimba za utotoni kwa wanafunzi hao
‘… Niwapongeze kwa kuitafsiri kwa vitendo dhana ya Serikali ya awamu ya Tano ya kuwa na nchi ya viwanda nyie mmeanza hivyo nitoe wito kwa shule nyengine kuiga kutoka kwenu hii itasaidia kupunguza tatizo la ajira na mtaacha kujikita katika mambo yasiyofaa ikiwemo kujiingiza katika mapenzi kabla ya muda na mmemsikia Mhe Rais na mimi namuunga mkono hatutakubali mama mwenye mtoto kurudi shuleni …’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Angeline Mabula amechangia milioni moja kama jitihada za kuunga mkono uanzishwaji wa kiwanda kwaajili ya ununuzi wa malighafi pamoja na kutoa matofali ya ujenzi wa jengo la kiwanda hicho
Akimkaribisha mgeni rasmi mstahiki meya wa manispaa ya Ilemela Mhe Renatus Mulunga amewahakikishia wanafunzi hao kuwa manispaa yake itakuwa bega kwa bega nao katika kuhakikisha ustawi na ukuaji wa kiwanda hicho katika kuiletea maendeleo jamii yake na mwanafunzi mmoja mmoja watakaofanya kazi katika kiwanda hicho
Kwa upande wake afisa elimu wa manispaa ya Ilemela na mwakilishi wa mkurugenzi wa manispaa hiyo Mwalimu Juma Kasandiko amezitaka shule za manispaa ya Ilemela kuhakikisha zinashona nguo zake katika kiwanda hicho ili kurahisisha upatikanaji wa soko la kudumu kwa kiwanda hicho sambamba na kupunguza gharama kwa wazazi
Akihitimisha ufunguzi huo mkuu wa shule ya wasichana Bwiru Mwalimu Meckitrida Shija amezitaja changamoto mbalimbali zinazokikabili kiwanda hicho ikiwemo kukosekana kwa eneo la kudumu la kiwanda sambamba na mtaji mdogo katika uzalishaji kunakochangia kukosekana kwa malighafi
Uzinduzi huo ulihusisha ununuzi wa bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho pamoja na kuhudhuriwa na maafisa elimu wa wilaya jirani za Bunda, Misungwi, wataalamu kutoka taasisi ya Kivulini, na baadhi ya madiwani wa manispaa ya Ilemela
' Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga '
Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela
27.11.2017
No comments:
Post a Comment