Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa, akizungumza na
mmoja wa wafanyakazi mara baada ya kukagua uboreshaji wa mashine za
mfumo wa kielektroniki za kukatia tiketi eneo la Magogoni, jijini Dar es
Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa, akipata maelezo
kutoka kwa Mtaalamu wa mambo ya kiufundi kutoka kampuni ya Maxicom
Africa Bw. Peter Mungo, wakati akikagua uboreshaji wa mashine za mfumo
wa kielektroniki za kukatia tiketi eneo la Magogoni, jijini Dar es
Salaam.
Mtaalamu wa Vivuko Bernad Daud,
akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
(Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa, wakati akikagua hali ya
uendeshaji wa vivuko vinavyotoa huduma katika eneo la Magogoni na
Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa, akizungumza na
baadhi ya abiria wanaopata huduma za vivuko katika eneo la Magogoni na
Kigamboni, wakati alipofanya ziara yake kuona huduma zinavyotolewa na
vivuko hivyo, jijini Dar es Salaam.
Abiria wakiingia katika Kivuko cha
MV Kazi kinachoendelea kutoa huduma za usafiri kati ya Magogoni na
Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
………………
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa, amemtaka Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kuanza kufanya majaribio ya
uboreshaji wa mashine za mfumo wa kielektroniki za kukatia tiketi ili
kurahisisha zoezi hilo na kulinda mapato sahihi ya Serikali.
Akikagua huduma zinazotolewa na
vivuko katika maeneo ya Magogoni na Kigamboni jijini Dar es Salaam,
Naibu Waziri Kwandikwa amesisitiza kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha
wananchi wanapatiwa huduma ya usafiri kwa viwango vya kisasa na muda
mfupi.
“Hakikisheni mfumo huu unaanza
kujaribiwa mapema iwezekanavyo ili kama kuna upungufu utakaojitokeza
mkandarasi aushughulikie mara moja kabla ya kipindi cha uangalizi
hakijamalizika”, amesisitiza Mhe. Kwandikwa.
Ameongeza kuwa uboreshaji wa mfumo
wa kieletroniki wa kukatia tiketi utasaidia kudhibiti ukusanyaji wa
mapato na kutunza kumbukumbu sahihi za abiria wanaopata huduma katika
maeneo hayo.
Aidha Naibu Waziri Kwandikwa,
amewataka TEMESA kuongeza matangazo ya elimu kwa wananchi ya namna ya
kuchukua tahadhari wanapotumia vivuko hivyo ili kuongeza uelewa na
kuepusha ajali.
Kuhusu huduma zinazotolewa na
vivuko vya Mv. Magogoni, Mv. Kazi na Mv. Kigamboni, mtumiaji wa vivuko
hivyo Bw. Riziki Phillipo, amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali
kuhakikisha usafiri kati ya Magogoni na Kigamboni unakuwepo kwa uhakika
na wakati wote.
No comments:
Post a Comment