Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith
Mahenge amezitaka Halmashauri za Wilaya, Mji na Manispaa Mkoani Dodoma
kuhakikisha zinatenga asilimia kumi (10%) ya makusanyo yao ya ndani kwa ajili
ya vijana, wanawake na Walemavu kuanzisha miradi ya viwanda vidogo na vya kati.
Lengo ni kuitikia kampeni ya Serikali
inayoitaka Mikoa kuanzisha viwanda kama ilivyozinduliwa hivi karibuni na Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mheshimiwa Seleman Jafo.
Akizungumzia hilo, ameonya tabia ya
baadhi ya Halmashauri kutotoa asilimia kumi (10%) ya makusanyo yake ya ndani au
kutoa kiasi kidogo kwa ajili ya vijana, wanawake na walemavu na kuwa utaratibu
unaotumika sasa wa Halmashauri kukopesha fedha hizo wakati mwingine sio muafaka
sana badala yake Halmashauri zitumie fedha hizo kuwafungulia vijana, wanawake
na walemavu viwanda vidogovidogo na kuwakabidhi waendeleze uzalishaji na
kuviendesha.
Dkt. Mahenge amebainisha hayo wakati
wa mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea Wilaya za Mkoa wa Dodoma
kujitambulisha na kukagua miradi ya maendeleo ambapo amesema kuwa viwanda
vinavyoweza kuanzishwa ni vya uchakataji wa nafaka, usindikaji mazao na
utengenezaji vyakula vya Mifugo.
Amesema kuwa asilimia kumi hiyo
ikitumika na kusimamiwa vizuri inaweza kutekeleza kampeni ya kuanzisha viwanda
ambapo vijana na wanawake wanaweza kufaidika kuanzia ngazi za chini kama
vijijini kwa kupata ajira kipato na halmashauri kupata ushuru.
Aidha, ameongeza kuwa mbali na
uanzishaji viwanda miradi mingine Halmashauri inayoweza kuwaanzishia vijana,
wanawake na walemavu ni pamoja na ufugaji samaki kwa kuwachimbia mabwawa.
Ametaja miradi mingine mbali na
viwanda kuwa Halmashauri zinaweza kuchimba visima na kujenga miundombinu ya
umwagiliaji ili vijana, wanawake na walemavu waendeshe kilimo cha umwagiliaji
kuzalisha mazao mbalimbali ambayo yanaweza kuwa malighafi kwenye viwanda
vinavyoanzishwa.
“Sisi ni Viongozi, maana ya kuwa
viongozi ni pamoja na kuwasaidia wananchi kuweza kufanya maamuzi yenye manufaa
kwao na uanzishwaji wa viwanda utawanufaisha wananchi wengi na Mkoa kwa ujumla”
alimalizia Dkt. Mahenge.
No comments:
Post a Comment