Thursday, November 23, 2017

WAZIRI HARRISON MWAKYEMBE AZINDUA MICHUANO YA SHIMUTA IRINGA

 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe akiwa pamoja na mkuu wa mkoa wa Iringa bi Amina Masenza jukwaa kuu akiwahutubia wanamichezo waliojitokeza kushiriki michuano ya SHIMUTA

 Baadhi ya wanamichezo walikuwa wakifurahia jambo baada ya waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe kuzindua rasmi mashindano hayo


Michuano ya SHIMUTA inayohusisha wafanyakazi wa mashirika ya umma, kampuni za watu binafsi na taasisi zilizopo hapa nchini imezinduliwa rasmi mkoani Iringa huku washiriki wakiwataka waajiri kuwaruhusu wafanyakazi kushiriki katika michezo huku waziri mwenye dhamana ya michezo akitoa onyo kwa mamluki.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amezionya timu ambazo zinashiriki kwenye michuano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma na Kampuni Binafsi Nchini (SHIMUTA) kuacha kuchukua wachezaji ambao sio wafanyakazi  kwani kufanya hivyo kunapunguza ladha ya mashindano hayo.                                

Mwakyembe alisema kuwa michezo hujenga undugu na furaha baina ya wanamichezo hivyo kuwaingiza wachezaji ambao sio wafanyakazi kwenye mashindano hayo wataondoa maana halisi ya mashindano hayo jambo ambalo linaweza kuwafanya kushindwa kufikia malengo yao waliojiwekea. 

  “Mashindano haya ni ya wanamichezo wafanyakazi…kuna wale wanamichezo ambao sio wafanyakazi ambao wanajulikana kama mamluki au wavamizi kwamba hapa sio mahala pao nawasihi tuchezeshe wafanyakazi halisi ili mshindi apatikane kihalali na sio vyenginevyo….. kwa sababu ni hatari sana kumleta mwanamichezo ambaye sio mfanyakazi kwenye michezo hii anaweza kuvunjika mguu au akifa kwa mfano hatuombei itokee hiyo itakuwaje “Alisema Mwakyembe

Aidha Mwakyembe alizitaka timu hizo kuacha kuwatumia wachezaji wa aina hiyo kwani wana madhara makubwa hasa pale yanapokuwa yakijitokeza kwa kuzitaka timu zenye utamaduni huo kuhakikisha wanaondokana nao. 

Hata hivyo waziri Mwakyembe alionekana kukerekwa na baadhi ya menejimenti za Taasisi,Mashirika na makampuni mbalimbali kuwa na utashi wa kutokupenda michezo na wengine kwa kisingizio cha ukosefu wa fedha kuacha kufanya hivyo badala yake wamuunge mkono Rais Jakaya Kikwete katika jitihada zake za kuinua na kuendeleza michezo hapa nchini. 

Akizungumzia waamuzi wanaochezesha mashindano hayo, Mwakyembe aliwataka kuchezesha kwa haki bila upendeleo kwa kufuata sheria za mchezo husika ili mshindi aweze kupatikana kihalali kwa sababu wakienda kunyume chake wanaweza kusababisha tafrani na manung’uniko kwa baadhi ya timu shiriki. 

Hali kadhalika aliwataka kuhakikisha wanakuwa na nidhamu ya hali ya juu wakati wote wa mashindano ikiwemo kukubaliana na matokeo pindi watakapojikuta wamefungwa wakati wa mashindano hayo. 

Naye Mwenyekiti wa Shimuta, Khamis Mkanachi alisema kuwa kupungua kwa idadi ya timu shiriki kunatokana na baadhi ya mashirika kubinafsishwa hali ambayo imepelekea timu nyingi kushindwa kupata nafasi ya kupeleka washiriki wake lakini pamoja na kuwepo hali hiyo shirikisho hilo limendelea na jitihada za ziada kuhakikisha idadi ya timu hizo haipungui bali kuongezeka. 

Nao baadhi ya washiriki wameeleza sababu ya baadhi ya waajiri wasio na mapenzi na michezo kushindwa kutoa hamasa sehemu za kazi kwa kutokujua faida zitokanazo na michezo.

 Ni wajibu wa viongozi kuinua na kuendeleza michezo mahala pa kazi “ni kauli mbiu yenye lengo la kuhamasisha ushiriki wa michezo kwa watumishi kwa lengo la kukutanisha wafanyakazi wa idara tofauti na kubadilishana uzoefu wa kikazi lakini kubwa zaidi ni kujenga afya kwa kupitia michezo.

SHIMUTA ni Shirikisho la Michezo la mashirika ya Umma Taasisi, na kampuni binafsi hapa nchini, lililoanzishwa na serikali ili kuhimiza michezo mahala pa kazi.

No comments:

Post a Comment