WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekipiga
marufuku Chuo Kikuu Ardhi kukodi makampuni ya kufanya kazi mbalimbali kwa niaba
yake.
Amesema kitendo hicho
kinaharibu kazi na sifa ya chuo hicho kwa kuwa baadhi ya makampuni wanayoyapa
kazi hayakidhi vigezo.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Novemba 23,
2017) kwenye ufunguzi wa sherehe za maadhimisho ya miaka 10 ya Chuo Kikuu
Ardhi.
“Kama kuna umuhimu wa
kufanya kazi na kampuni ni bora muanzishe kampuni ya kwenu itakayofanya kazi
vizuri ili kujiepusha na matatizo.”
Pia Waziri Mkuu amekiagiza
chuo hicho kufanya tafiti zenye kuleta majibu ya maswali na changamoto
mbalimbali zinazolikabili Taifa na Dunia.
Ametaja baadhi ya changamoto
hizo kuwa ni mabadiliko ya tabia nchi, ujenzi holela, uharibifu wa mazingira na
majanga ya asili kama mafuriko.
Amesema Serikali inaamini
kuwa matokeo ya kazi zinazofanywa na chuo hicho zikiwemo tafiti ni chachu ya
maendeleo ya taasisi za elimu ya juu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Dira
ya Maendeleo ya Taifa imeweka mkazo wa kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa
kupato cha kati ifikapo 2025, hivyo wanahitajika wataalamu wa kutosha na wenye
weledi.
“Hivyo Chuo Kikuu cha Ardhi
kama taasisi ya Serikali inawajibu mkubwa wa kutayarisha wataalamu mbalimbali
wa sekta za ujenzi, ukadiriaji majenzi na uhandisi wa mazingira.
Pia Waziri Mkuu amewataka
watumie fursa hiyo ya kuadhimisha miaka 10 ya chuo hicho kujitafakari na kuona
ni kwa namna gani wanaweza kuwekeza zaidi ili kuongeza tija ya uwepo wa taasisi
hiyo kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
“Wekeni mikakati madhibuti
itakayowezesha chuo kupiga hatua kubwa zaidi katika kipindi cha miaka 10 ijayo.
Siku zote mjikite katika kutafuta kuwa na ubora zaidi ya wakati uliopita.”
Awali, Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema Serikali inakkitegemea
chuo hicho katika kufanikisha ajenda yake ya uchumi wa viwanda kwa kuwa kinatoa
wataalamu wengi.
Maadhimisho hayo
yalihudhuriwa na Mkuu wa chuo hicho ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa David
Msuya, Mwenyekiti wa Baraza la chuo Bibi Tabitha Siwale, Makamu Mkuu wa chuo
Profesa Evaristo Liwa pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, wanafunzi na
watumishi wa chuo hicho.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, NOVEMBA 23, 2017.
No comments:
Post a Comment