Monday, September 11, 2017

DC MWANGA AWAKOROMEA MAAFISA MADINI WANAOINGIA BAGAMOYO KWA MASLAHI YA MATUMBO YAO

IMG_20170907_165126
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani ,alhaj Majid Mwanga ,aliyesimama mwenye koti jeusi akizungumza jambo na wananchi wa kijiji cha Kinzagu huko Lugoba,anaemfuatia kushoto ni mwenyekiti wa kijiji cha Kinzagu William Meleck na diwani wa kata ya Lugoba Rehema Mwene mwenye kilemba .(picha na Mwamvua Mwinyi )
IMG_20170907_173210
Mwekezaji wa kampuni ya Gulf.Conc.Khaled Mohammed ,akizungumza katika mkutano wa kijiji Kinzagu kata ya Lugoba (picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze

MKUU wa wilaya ya Bagamoyo,alhaj Majid Mwanga,amekemea tabia inayofanywa na baadhi ya maafisa wa madini wasio waadilifu ambao wanakandamiza sheria kwa maslahi ya matumbo yao na kuwanyima haki wananchi.

Aidha amesema kuanzia sasa,afisa madini anayeingia kwenye vijiji vilivyopo Chalinze na Bagamoyo, bila ya kupitia ofisi ya mkuu mkoa na wilaya hiyo ,mtendaji wa kijiji anapaswa amkamate na kufikishwa polisi.

Kutokana na kemeo hilo,amemuagiza katibu tawala wa wilaya kuwaandikia barua maafisa tarafa wote ,wapeleke taarifa za wawekezaji wenye leseni za mifukoni na wasioendeleza maeneo yao.

Alhaj Mwanga ,ameeleza pamoja na agizo hilo,serikali za vijiji zikae na zipeleke taarifa za wawekezaji waliokwapua ardhi za watu bila makubaliano na kupata ridhaa ya mkutano mkuu wa vijiji.

Aliyasema hayo katika mkutano wa kijiji cha Kinzagu,huko Lugoba /Chalinze,uliolenga kuzungumzia mgogoro baina ya mwekezaji Global co.ltd ,mwekezaji Gulf conc.na wananchi .

Alhaj Mwanga ,alisema atalala sambamba na maafisa madini wanaotengeneza migogoro kwa maslahi ya matumbo yao.

Mkuu huyo wa wilaya ,alieleza ni lazima maafisa hao wafuate sheria na kuheshimu mamlaka nyingine ,kwani kuna kila sababu ya kutambua ofisi ya mkuu wa mkoa,wilaya,kata na vijiji.

Hata hivyo alhaj Mwanga alifafanua kwamba,wawekezaji wenye leseni zilizoegeshwa kimagumashi itakuwa imekula kwao.

Alieleza hatua hiyo itasaidia kuondoa wimbi la wawekezaji walio na leseni ambazo hazijafuata sheri.

Anasema, kampuni ya Gulf ipo kwa mujibu wa sheria na wanaendelea na uzalishaji wa madini ya kokoto ambapo kutokana na athari ya vumbi ndani ya jamii alilazimika kuomba kuongeza eneo kwa ajili ya uzalishaji.

Anafafanua ,hatua mbalimbali zilifutwa kwa mujibu wa sheria ambapo kampuni hiyo ilifanya tathmini kwa ushirikiano na maafisa ardhi wa halmashauri ya chalinze .

“Baada ya zoezi hilo kukamilika nilifika hapa na tayari nilisaini barua niliyopaswa kusaini na kwasasa inasubiriwa mkuu wa mkoa aipitishe,”alisema alhaj Mwanga .

“Cha kushangaza baada ya uhakiki wa eneo linaloongezwa, inadaiwa alifika kamishna msaidizi wa madini Kanda ya Mashariki kijijini hapa na kusema eneo hilo ni la mwekezaji kampuni ya Global wenye leseni miaka 17 iliyopita “alisema .

Alhaj Mwanga alisema tamko hilo liliwachanganya wananchi na kampuni iliyokuwa na lengo la kulipa fidia wananchi .

“Afisa huyo wa madini asingekuja kuzuia zoezi hili watu tusingefika leo hii tena,kupoteza muda,gharama na kuacha mambo mengine ya kimaendeleo:,”Maafisa hawa hata hawajui na hawajabadilika kwenda na kasi ya Rais Magufuli ,bado wao wapo kwenye karne ya maslahi ya matumbo yao”alisisitiza .

Alhaj Mwanga aliwauliza watendaji wa chini wote na halmashauri juu ya taarifa za mwekezaji Global na hakuna aliye na taarifa zake hata ofisi ya wilaya hawaimtambui.

Nae mkazi wa Kinzagu,Mkombozi Mrisho alimuomba mkuu wa wilaya kusimamia haki yao kwa kamishna wa madini mkuu ili waweze kupata fidia na kuondoka katika eneo hilo ambalo ni hatarishi kwa afya zao.

“Mie nina umri zaidi ya miaka 17 aliyopewa leseni huyo Global lakini naapa hatumjui Global na hatujawahi kumuona tangu nizaliwe na kama kamishna huyo anamjua Global aseme alifanya tathmini mwaka gani “alisema Mrisho.

Mwakilishi wa kamishna wa madini Kanda ya Mashariki, aliyefika katika mkutano huo ,afisa madini kanda ya Mashariki-Dar es salaam ,Antony Ngalalumba,alisema kila mwekezaji lazima awe na leseni.

Alisema ,ni kweli wawekezaji wote wawili wanazo leseni, hivyo anabeba maagizo ya mkuu wa wilaya na malalamiko ya wananchi ambapo atayafikisha  kwa kamishna mkuu wa madini ili kupatiwa ufumbuzi.

Akizungumzia malalamiko ya maafisa madini kuingia vijijini bila kuonana na serikali ya vijiji ,alieleza afisa yoyote akitaka kufika ndani ya jamii lazima aione serikali ya kijiji kwa mujibu wa sheria ya madini 2010.

Ngalalumba ,alibainisha wawekezaji pia wanapaswa wawaone serikali ya kijiji badala ya kudharau serikali hizo kisheria .

Kwa upande wake ,diwani wa kata ya Lugoba,Rehema Mwene,alitaka maafisa madini kujenga ushirikiano na jamii na kuacha kukumbatia leseni za magumashi kwa maslahi yao.

Alisema mwekezaji Global tangu apewe leseni hiyo mwaka 2001 hajawahi kuendeleza eneo lake na hakufuata utaratibu.

Rehema ,aliiomba serikali ya awamu ya tano kuchukua hatua kwa watumishi wachache wanaokandamiza maslahi ya wananchi na kutumia raslimali za eneo husika vibaya.

Mtendaji wa kijiji cha Kinzagu Mauwa Mohammed.alisema kampuni ya Gulf ndio wanaitambua ambayo inaendelea na uzalishaji na kukaa nao kwenye mkutano wa kijiji kufanya makubaliano ya fidia.

Katika hatua nyingine,mwenyekiti wa kijiji cha Kinzagu ,William Meleck,alisema kitendo cha maafisa madini kuingilia zoezi la fidia ni kukwamisha maendeleo ya kijiji.

Alisema ,maafisa hao wanadharau serikali ya kijiji kwa kuingia kijijini pasipo ofisi ya kijiji kujua lolote huku wakidai taratibu zao sio lazima waripoti kwenye serikali za kijiji.

Mwekezaji wa kampuni ya Gulf.Conc.Khaled Mohammed ,alisema wakipata fursa hiyo wataendeleza ushirikiano wanaoufanya kijijini hapo.

Alisema kila siku wanazalisha awamu 50 za roli za kokoto na kuiingizia halmashauri ya Chalinze sh.milioni.tisa (9)kama ushuru kwa mwezi.

Hata hivyo Mohammed ,alieleza katika sekta ya afya tayari wamejenga nyumba ya mganga ya kuishi familia mbili na sekta ya elimu wanasomesha watoto wawili wa mazingira hatarishi elimu ya sekondari .

Kwa mujibu wa Mohammed ,mwaka 2001 walipata leseni ya uchimbaji madini ya kokoto Kinzagu kata ya Lugoba na wanatarajia kuongeza eneo kwa kulipa fidia wananchi waliofanyiwa tathmini zaidi ya Milioni.650 .

Katika mkutano huo ,uliadhimia kampuni ya Gulf.conc  iendelee na shughuli zake na kukamilisha zoezi la fidia huku likisubiriwa jibu kutoka kwa kamishna mkuu wa madini.

No comments:

Post a Comment