Tuesday, September 26, 2017

MHE KINGU AWAOMBEA MAJI WAKAZI WA JIMBONI KWA LISSU

Naibu waziri wa maji na Umwagiliaji Mhe Isack A. Kamwelwe akizungumza na watumishi wa Wilaya ya Ikungi mara baada ya kupita Ofisi za Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akielekea Manispaa ya Singida kwa ajili ya mapumziko, Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi Mhe Elibariki Kingu
Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi Mhe Elibariki Kingu (Kushoto) akimfatilia kwa makini Naibu waziri wa maji na Umwagiliaji Mhe Isack A. Kamwelwe wakati wa kikao cha pamoja na watumishi wa Wilaya ya Ikungi, Mwingine ni Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Ikungi Ndg Elieza

Na Mathias Canal, Singida

Pamoja na Changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili wananchi katika Jimbo la Singida Mashariki Wilayani Ikungi Mkoani Singida lakini uhaba wa upatikanaji wa huduma ya maji ni kikwaz kikubwa kwa wananchi kwani wanatumia umbali na muda mrefu kutafuta maji.



Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi Mhe Elibariki Kingu ametoa ombi hilo mbele ya Naibu waziri wa maji na Umwagiliaji Mhe Isack A. Kamwelwe wakati akizungumza na watumishi wa Wilaya ya Ikungi kwenye kikao kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu.

Mhe Kingu alisema kuwa Jimbo lake lina changamoto ya maji ambayo kwa kiasi kikubwa serikali inaendeleza juhudi za kuzitatua, huku akisema kuwa katika Jimbo jirani la Singida Mashariki linaloongozwa na Mhe Tundu Lissu hali ni mbaya zaidi katika upatikanaji wa miundombinu ya maji kwa wananchi wake.

Alisema kuwa hivi karibuni alipita katika jimbo hilo na kujionea adha inayowakumba wananchi jambo amablo lilimfanya kujipanga kuwaombea maji wananchi hao katika kipindi cha Bunge lijalo.

Alisema kuwa wananchi hao wamebaki wakiwa utadhani hawana muwakilishi wa Jimbo kwa kipindi cha miaka 10 jambo ambalo linafanya kuteseka na huduma za utafutaji maji kwa kutumia muda mwingi na umbali mrefu.

Aidha, Mhe kingu alisema kuwa pamoja na changamoto ya upatikanaji wa maji Katika Jimbo la Singida Mashariki lakini pia jimbo hilo linakumbwa na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu ambayo ni pamoja na uhaba wa vyumba vya madarasa, Nyumba za walimu, Maabara, Matundu ya vyoo na mabweni.

Hata hivyo alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu kwa kuanzisha mkakati wa pamoja wa kuanzisha Mfuko wa Elimu Ikungi utakaowashirikisha wananchi pamoja na wadau wa elimu kuchukua hatua madhubuti ili kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto na hatimaye kuwafanya wanafunzi waweze kuongeza ufaulu.

Naibu waziri wa maji na Umwagiliaji Mhe Isack A. Kamwelwe ameanza ziara ya kikazi ya siku nne Mkoani Singida ambapo atatembelea na kukagua Miradi ya Maji na vyanzo vya uboreshaji upatikanaji wa maji. 

MWISHO

No comments:

Post a Comment