Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge
ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla King akisisitiza jambo wakati wa
ziara ya Kamati ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mnara wa TTCL kwenye
kijiji cha Sanga Itinje kilichopo Kata ya Itinje wilaya ya Meatu mkoani
Simiyu. Kushoto kwa Mwenyekiti ni Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano
kwa Wote Eng. Peter Ulanga
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bwana John
Mongella akiongea kuhusu mchango wa mifumo ya mawasiliano katika
kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali mbele ya Kamati ya
Bunge ya Miundombinu na watendaji wa kampuni za simu wa mkoani Mwanza
(hawapo pichani) wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kukagua ujenzi wa
minara, ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini
mkoani Mwanza. Aliyeketi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu
Prof. Norman Sigalla King.
Meneja wa TTCL mkoa wa Shinyanga
Bwana Abdallah Lugage akitoa taarifa kwa Kamati ya Bunge ya Miundombinu
kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mnara wa kampuni hiyo kwenye kijiji cha
Sanga Intinje kilichopo kata ya Intinje wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.
Wa tatu kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo Prof. Norman Sigalla King.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya
Miundombinu, watendaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, wafanyakazi wa
TTCL na wanakijiji wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa ziara ya
Kamati hiyo ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mnara wa kampuni hiyo
kwenye kijiji cha Sanga Intinje kata ya Intinje iliyopo wilaya ya Meatu
mkoani Simiyu.
………………….
Serikali ya Awamu ya Tano ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli
imesisitiza kwa taasisi za Serikali, sekta binafsi na wananchi kwa
ujumla kulipa kodi kwa wakati ili nchi iweze kuongeza mapato yake kwa
lengo la kukuza uchumi, kujenga miundombinu ya barabara, reli, bandari,
mawasiliano, kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kuweza kuwatumika
wananchi.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Prof. Norman Sigalla wakati wa ziara
ya Kamati yake ya kukagua ujenzi wa minara, ufikishaji na upatikanaji
wa huduma za mawasiliano vijijini na kwenye maeneo yasiyo na mvuto wa
kibishara kwenye mikoa ya kanda ya ziwa ya Mwanza na Mara ambapo
Serikali imetoa ruzuku kwa makampuni ya simu za mkononi ili ziweze kutoa
huduma za mawasiliano kwa wananchi kupitia Mfuko wa Mawasiliao kwa Wote
(UCSAF) ulio chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Ameongeza kuwa Kamati yake
inasimamia sekta ya miundombinu yote nchini ikiwa ni pamoja na
miundombinu ya mawasiliano ambayo inategemewa na Serikali katika kukuza
uchumi na kuiwezesha nchi yetu kufikia uchumi wa kati na kuwa nchi ya
viwanda.
Prof. Norman Sigalla King amesema kuwa miundombinu na huduma za
mawasiliano ni moja ya nguzo kuu za ukuaji wa uchumi, inachochea
maendeleo ya taifa letu na kuiwezesha Serikali kuhudumia wananchi wake
kwa haraka, wakati, kwa ufanisi na kupunguza gharama za Serikali
kuwahudumia wananchi na kuokoa muda.
“Serikali imepeleka fedha nyingi
kwa ajili ya miundombinu mbalimbali ya nchi yetu kupitia Wizara hii
kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2017/2018 ili nchi iweze
kusonga mbele”, amesema Prof. Norman Sigalla King.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bwana
John Mongela ameieleza Kamati hiyo kuwa mifumo ya mawasiliano
imeiwezesha Serikali ya Mkoa wake kuongeza makusanyo ya mapato katika
Halmashauri za mkoa huo kutoka chini ya asilimia 46 kwa mwaka wa fedha
uliopita na kufikia asilimia 70 kwa mwaka huu wa fedha ambapo
Halmashauri hizo zinatumia zaidi ya asilimia 70 ya makusanyo hayo
kuendesha miradi ya maendeleo na kutekeleza majukumu mengine ya mkoa.
“Suala la mawasiliano duniani popote pale ni nyeti sana kwa kuwa
shughuli zote zinafanywa na mawasiliano kama vile miamala ya kifedha,
ulinzi na usalama wa raia na mali zake ambapo katika ngazi ya Mkoa
tumedhibiti kwa kiwango kikubwa ulinzi na usalama wa raia wetu na hali
ya mawasiliano kwenye mkoa wetu ni nzuri na tuna Mkongo wa Taifa wa
Mawasiliano,” amesema Mongella.
Ameongeza kuwa Mkoa huu ni mkoa wa pili
kwa ukubwa wa idadi ya watu na ni mkoa wa pili ambao unaongoza kwa
kuchangia kwa kiasi kikubwa mapato na ukuaji wa uchumi wa taifa letu.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Eng. Peter Ulanga amesema kuwa Mfuko
umetoa ruzuku kwa kampuni za simu za mkononi ili kufikisha huduma za
mawasiliano kwenye mikoa ya kanda ya ziwa na visiwa vyake takribani 36
vilivyopo kwenye kanda hii ili waweze kutumia mawasiliano kwa ajili ya
ulinzi na usalama na shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii.
Ameongeza
kuwa kupitia Halotel, UCSAF imepeleka mawasiliano kwenye vijiji 78
vilivyopo kanda ya ziwa na ziara hii inatusaidia kupata maoni ya wadau
na kukusanya changamoto ambazo zitasaidia kuboresha jukumu la UCSAF la
kufikisha huduma za mawasiliano vijijini na maeneo yasiyo na mvuto wa
kibiashara nchini nzima.
Mtaalamu wa miundombinu wa kampuni
ya simu ya Halotel wa Mkoa wa Mwanza na Simiyu Bwana Emmanuel Masanja
amesema kuwa kampuni yao inajenga minara kwa kukodisha au kupewa ardhi
na mamlaka za serikali za vijiji kwa ajili ya ujenzi wa minara hivyo
wanaishukuru Serikali kuwapatia ruzuku ya kufikisha mawasiliano
vijijini.
Ameongeza kuwa baadhi wa watu wanazuia maendeleo ya ujenzi wa
minara kwenye baadhi ya maeneo vijijini ambapo yanasababisha migogoro
ambayo inachukua muda mrefu kukamilishwa hivyo kuchelewesha ujenzi wa
minara na ufikishaji wa huduma za mawasiliano vijijini.
Bwana Masanja amesema kuwa kampuni
yao wanaiomba Serikali iwasaidie kusimamia upatikanaji wa ardhi kwa
ajili ya ujenzi wa minara ya mawasiliano kwenye ngazi ya Halmashauri
zote nchi nzima ili kuwawezesha wakandarasi kujenga minara kwa wakati
ili kuharakisha jitahada za Serikali ya Awamu ya Tano Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kufikisha huduma za mawasiliano kwenye vijiji
vyote nchi nzima na maeneo yasiyokuwa na mvuto wa kibiashara.
Aidha Mkurugenzi wa Kanda ya Ziwa
wa kampuni ya TIGO Bwana Ally Maswanya ameishukuru Serikali kwa
kuwapatia ruzuku ya kujenga minara na kufikisha huduma za mawasiliano
vijijini kwa kuwa kampuni zetu zinafanya biashara hivyo haikuwa rahisi
kwa kampuni za simu za mkononi kuwekeza bali UCSAF imetuwezesha
kusambaza mawasiliano vijijini.
Vile vile ameiomba Serikali kuwasaidia
kufikisha umeme kwenye minara kupitia Wakala wa Nishati ya Umeme
Vijijini (REA) kwa kuwa inawapa changamoto ya kuongeza gharama za
kuendesha minara hiyo na umeme wa jua hautoshelezi.
Ameongeza kuwa sisi kama kampuni
ya Halotel tunapata ushirikiano mkubwa kutoka ofisi za Wakuu wa Mikoa na
wilaya kwenye maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kujenga minara bali
changamoto ipo kwenye ngazi za Halmashauri za upatikanaji wa ardhi na
utatuzi wa migogoro ya ardhi na ukosefu wa ushirikiano wa kutosha kutoka
kwa mamlaka husika ili kufanikisha ufikishaji na upatikanaji wa huduma
za mawasiliano vijijini.
Mwenyekiti Prof. Sigalla amesema
kuwa nguzo za uchumi mojawapo ni miundombinu kwa maana ya barabara,
bandari, reli na mawasiliano na ndiyo maana serikali imepeleka fedha
nyingi kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/18.
Ametoa rai kwa
wananchi kuwa watoe ulinzi kwenye minara yote ya mawasiliano nchini kwa
kuwa Serikali inatumia kodi za wananchi kujenga minara. Ameongeza kuwa
wananchi watumie fursa ya mawasiliano kwa maendeleo na kujenga uchumi
wao na maendeleo ya taifa.
Pia ameyaomba makampuni ya simu yote nchini
ambayo yamepatiwa ardhi na serikali ya kijiji na kujenga minara irudishe
faida kwa wananchi wa eneo husika kwa kuwapatia fedha au huduma za
kijamii.
Amesisitiza kuwa kampuni za
mawasiliano zitumie fedha waliyopewa na Serikali kujenga minara na
kufikisha huduma za mawasiliano vijijini kwa wakati kwa kuwa
ucheleweshaji wa kutekeleza jukumu hilo unawanyima wananchi haki ya
kupata huduma za mawasiliano.
Pia ameongeza kuwa kwa namna yoyte ile
kampuni haziwezi kulipa gharama za ucheleweshaji wa kujenga minara hiyo
na upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi na Serikali kwa
ujumla.
“Maendeleo ni vita, ukipewa ruzuku na Serikali ya kujenga minara
na ukichelewesha ni hasara; hakikisheni mnakimbizana kukamilisha jukumu
hilo kwa wakati,” amesema Prof. Norman Sigalla King.
Aidha, ametoa rai kwa kampuni za
simu zinazopatiwa ardhi bure na Serikali za vijiji mbalimbali nchini
kote kutoa fedha kwa vijiji hivyo sehemu ya fedha wanazopata ili vijiji
viweze kunufaika na uwepo wa minara hiyo kwa kuwa kampuni zinafanya
biashara.
Ametanabaisha kuwa minara haina madhara kwa wananchi
ukilinganisha na usikilizaji wa simu za mkononi kwa muda mrefu zaidi ya
dakika tisa. Amewatahadhirisha wananchi kuwa wananchi wasikilize simu
kwa muda mfupi na isizidi dakika tisa.
“wananchi watumie vifaa vya
kusikiliza simu masikioni kwa wale ambao wanasikiliza simu kwa muda
mrefu na minara inayowekwa na UCSAF ni salama na tumieni simu kwa
maendeleo chanya,” amesema Prof. Norman Sigalla King.
Pia ameipongeza
Wizara kwa kazi kubwa inayofanya ya kujenga na kusimamia miundombinu
iliyopo kwenye sekta ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment