Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
akiongea na wananchi wa kitongoji cha Mwamnange kilichopo Wilaya ya
Kaliua leo Agosti 11 2017 .Wananchi hao walisimamisha msafara wake ili
kumuomba serekali iwasaidie kupata Umeme. Waziri Mkuu yupo Mkoani
Tabora kukagua shughuli za maendeleo
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeamua kufufua mazao matano ambayo yanaingiza kwa wingi fedha za kigeni nchini.
Amesema mbali ya korosho, Serikali imeamua kuboresha mazao ya tumbaku, chai, kahawa na pamba.
Ametoa kauli hiyo kwa nyakati
tofauti jana na leo wakati akiwahutubia wananchi kwenye maeneo
mbalimbali akiwa katika ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Tabora.
Alisema kuanzania sasa
serikali imepiga marufuku matumizi ya dola za Marekani kwenye ununuzi wa
zao la tumbaku kwa sababu mazao mengine makuu hapa nchini yananunuliwa
kwa fedha za Kitanzania.
“Ni kwa nini tumbaku inunuliwe
kwa dola za Marekani ilhali mazao mengine yananunuliwa kwa fedha za
Tanzania? Korosho, pamba, chai na kahawa wakulima wetu kote huko
wanalipwa kwa fedha za Tanzania, kwa nini tumbaku iwe tofauti?” alihoji.
Alisema wenye makampuni
wanaweza kukaa kwenye vikao vyao na kupanga bei zao kwa dola za Marekani
lakini pindi wanapoingia nchini, watalazimika kufanya malipo kwa
kutumia fedha ya Tanzania kwani mfumo malipo kupitia dola za Marekani
umekuwa ukiwaibia wakulima kwa muda mrefu.
Waziri Mkuu amewataka
watendaji na watumishi wa Halmashauri na wilaya za mkoa wa Tabora
wasimamie zao la tumbaku ili kuinua kilimo cha zao hilo na kuwanufaisha
wakulima.
“Maafisa kilimo na maafisa ushirika mnapaswa kulisimamia zao hili na siyo kuwaachia maafisa wa makampuni yanayonunua tumbaku.”
“Kwa muda mrefu mlizembea na
kuwaachia maafisa wa makampuni ya ununuzi ndiyo washughulike na
wakulima. Nataka mbadilike, kuweni karibu na wakulima na muwasaidie
kulima kisasa na kwa kutumia pembejeo,” alisema.
“Wasaidieni wakulima watoke
kwenye mfumo wa kukopa pembejeo, wahimizeni wajiwekee akiba ili msimu
ukianza wawe na fedha ya kununua pembejeo. Wakulima wanalaliwa sababu ya
mikopo ya pembejeo. Makato yanakuwa mengi kiasi kwamba mkulima
ahambulii chochote,” alisema.
Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake wilayani Kaliua ambako atazungumza na wananchi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, AGOSTI 11, 2017.
No comments:
Post a Comment