Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
akihotubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Veta Jimbo
la Ulyankulu wilayani Kaliua Mkoani Tabora leo August 11.2017, ambapo
amewataka wananchi waliopewa uraia kuheshimu sheria za nchi vinginevyo
watachukuliwa hatua za kisheria.
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka wananchi wanaoishi kwenye makazi ya wakimbizi ya Ulyankulu
waache kujihusisha na matukio ya uhalifu.
Ametoa onyo hilo leo mchana
(Ijumaa, Agosti 11, 2017) wakati akiwahutubia mamia ya wakazi wa tarafa
ya Ulyankulu katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya
VETA, wilayani Kaliua mkoani Tabora.
Amesema matukio ya ujambazi,
mauaji na umiliki wa silaha yanayofanyika kwenye tarafa hiyo ni mengi
ikilinganishwa hali ilivyo kwenye maeneo mengine ya mkoa huo.
“Taarifa nilizonazo
zinaonyesha katika kipindi cha miaka miwili kumekuwa na matukio ya
mauaji 35, ujambazi matukio 12, umiliki wa silaha nao unatisha.
Yamekamatwa magobole 11, bunduki aina ya SMG saba na Mark Four mbili.”
“Tulikamata pia risasi 714 za
SMG zikiwa kwenye ndoo za mafuta na juu yake wamepaka mafuta ya mawese.
Pia risasi mbili za Mark Four zilikamatwa,” amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amewataka wakazi
hao ambao baadhi yao wamepewa uraia na wengine bado ni wakimbizi
waonyane wanapokutana kwenye vikao vyao kwa sababu matendo yao
yanaikwaza Serikali ambayo iliamua kuwapa hifadhi. “Ni vema mkikutana
kwenye vikao vyenu muelezane na kuonyana,” amesema Waziri Mkuu.
“Ninawasihi matukio haya
myadhibiti la sivyo mtaharibu nia njema iliyoleta uwepo wenu. Bunduki
na risasi zinakuja kufanya nini wakati nyie mko maeneo salama? Mauaji ya
nini? Kama kuna tatizo limekupata, muone mwenyekiti wa kijiji,
atakusaidia,” alisisitiza.
Alitumia fursa hiyo kuwaonya
baadhi yao ambao wamegeuka mawakala na wameanza kuwaleta ndugu zao bila
kufuata utaratibu. “Hatuzuii mtu kutembelewa na ndugu yake, lakini ni
lazima mfuate taratibu. Tunataka tudumishe amani iliyopo nchini lakini
pia tudumishe urafiki wa nchi zetu mbili za Burundi na Tanzania,”
aliongeza.
Mapema, Mbunge wa jimbo la
Ulyankulu, Bw. John Kadutu alimuomba Waziri Mkuu afuatilie suala la
upatikanaji wa maji kwenye tarafa hiyo, pia aliomba wasaidiwe ili kata
tatu za Kanindo, Igombenkulu na Milambo ziwezeshwe kufanya uchaguzi wa
Serikali za Mitaa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, AGOSTI 11, 2017.
No comments:
Post a Comment