Saturday, August 12, 2017

WANANCHI KATA YA MABILIONI WILAYANI SAME WATUMIA MAJI YENYE CHEMBECHEMBE ZA KINYESI CHA BINADAMU

Mkuu wa wilaya ya Same,Rosemarry Sitaki akizungumza katika mkutano na wananchi katika kata ya Mabilioni wilayani Same.
Baadhi ya wananchi katika kata ya Mabilioni wilayani Same wakimsikiliza mkuu wa wilaya alipozunumza nao katika mkutano uliofanyika katika ofisi ya kata.
Afisa Elimu wa Kata ya Mabilioni wilayani Same,Richard Sekibojo akimkabidhi taarifa ya kata hiyo Mkuu wa wilaya ya Same,Rosemarry Sitaki wakati wa mkutano uliofanyika katika ofisi za kata hiyo.
Baadhi ya wananchi wa kata ya Mabilioni waliohudhuria mkutano huo.
Mkuu wa wilaya ya Same ,Rosemarry Sitaki akifuatilia maelezo ya kero mbalimbali yaliyokuwa yakitolewa na wananchi katika mkutano huo.kushoto kwake ni Diwani wa kata ya Mabilioni,
Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii ,Kanda ya Kaskazini
 
WANANCHI katika Kata ya Mabilioni wilayani Same wako katika hatari ya kupata ugonjwa wa kipindupindu kutokana na kutumia maji ya mto Ruvu yaliyopimwa na kugundulika kuwa na chembe chembe za Kinyesi cha Binadamu.
Wakazi 5109 wanaounda kaya 1158 wamekuwa wakitumia maji ya Mto Ruvu unaopita katika vijiji vitatu viliyoko kaika kaa hiyo vya Chekereni,Mabilioni na Ruvu Mbuyuni  kwa ajili ya Kunywa,Kupikia ,Kufulia ,kuogea pamoja na Kilimo .
Afisa Elimu wa kata ya Mabilioni ,Richard Sekibojo aliyasema hayo wakati akitoa taarifa ya kata hiyo kwa Mkuu wa wilaya ya Same, Rosemarry Sitaki alipofanya ziara katika kata hiyo na kufanya mkutano na wananchi wa kata ya Mabilioni.
“Mh Mkuu wa wilaya kata ya Mabilioni haina maji safi ya kunywa,kwani wananchi wanatumia maji ya Mto Ruvu kwa matumizi yote ya nyumbani pamoja na Kilimo  na maji hayo yalipimwa yakaonekana kuwa yana chembechembe za kinyesi cha binadamu zinazosababiha ugonjwa wa kipindupindu”alisema Sekibojo.
Akijibu malalamiko hayo Mkuu wa wilaya ya Same,Rosemarry Sitaki alisema uko mradi mkubwa sana wa maji wa serikali toka wizara ya Maji ,ambao unatoa maji Bwawa la Nyumba ya Mungu  kupitia wilaya ya Mwanga,Same hadi Korogwe mkoani Tanga .
“Kuhusu suala la maji ,nilikuwa naambiwa hapa kuwa kila visima vikichimbwa maji yanakuwa na chumvi nyingi sana na kwamba hayawezi kutumika kama maji ya kunywa na yale ya mtoni ndio kama tulivyosikia kuwa hayana sifa za kiafya na kutumika na binadamu.”alisema Sitaki.
Mradi huu mkubwa ndio utakuwa suluhu ya haya matatizo ,mradi tayari umeanza kujengwa kwenye chanzo ukiwa katika hatua za mwisho kukamilika na katika wilaya ya Same mkandarasi amekwisha patikana na ameanza kuchimba matenki .
Alisema kulingana na ukubwa wake,mradi huo utachukua hadi miaka mitatu kukamilika kwake na kwamba utagharimu zaidi ya Sh. Bilioni 142 ukifadhiliwa na serikali kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa na mashirika ya misaada ya kimataifa kutoka nchi za Falme za Kiarabu.
Kwa mujibu wa serikali mkoa wa Kilimanjaro,mradi huo utawaepusha idadi kubwa ya wananchi kwenye Wilaya hizo kuondokana na hatarini kuugua magonjwa ya mlipuko kama Kipindupindu na Kuhara kutokana na kunywa maji yasiyo safi na salama.
Hadi kukamilika kwake mradi huo utanufaisha zaidi ya wananchi 247,500 wa vijiji 28 vya Wilaya za Mwanga na Same kwa upande wa mkoa wa Kilimanjaro ambao kwa sasa upatikanaji wa maji vijijini ni asilimia 79 na mijini mkoa wa Kilimanjaro unakimbilia asilimia 98.
Mradi huo unajengwa kwa ufadhili wa Benki ya Kiarabu inayosimamia Maendeleo ya Nchi za Afrika (Badea), Mfuko wa Ofd unaojumuisha nchi zinazozalisha mafuta (Opec) na Mfuko wa Maendeleo wa Kimataifa wa Saud na Mfuko wa Misaada wa Kuwait.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment