Serikali
kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mapema leo
Agosti 11, 2017, imetangaza matokeo ya washindi wa shindano la Afya na usafi wa
Mazingira kwa mwaka 2017, iliyokuwa na kauli mbiu ‘Nipo Tayari’.
Akitangaza
washindi hao mapema leo katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya, Jijini Dar es
Salaam Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy
Mwalimu amepongeza wadau mbalimbali kwa kuweza kufanikisha zoezi hilo zikiwemo
Halmashauri zote zilizoshiriki.
“Mashindano ya afya na
usafi wa mazingira kwa mwaka huu 2017 hapa nchini yaliweza kushirikisha
Halmashauri zote zaidi ya 185 huku, Halmashauri 73 zikishindanishwa Kitaifa
baada ya mchujo ngazi ya Mkoa.
Mchanganuo wa
Halmashauri hizi ni; Majiji Manne, Manispaa 21, Miji 21 na Halmashauri za
Wilaya 27. Kila mwaka, Wizara yetu imekuwa
ikiratibu mashindano haya Kitaifa nchini kote ikiwa na lengo la kuinua hali ya
afya na usafi wa mazingira katika ngazi ya Kaya na taasisi ili kulinda na
kuboresha afya ya jamii.” Amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri
Ummy Mwalimu amewatangaza washindi wa kwa upande wa Halmashauri za Majiji na
Manispaa ambapo Manispaa ya Moshi ikiibuka kidedea kwa kupata asilimia 78.5,
mshindi wa Pili, Jiji la Arusha, Asilimia 78.1 na mshindi wa tatu, Halmashauri
ya Manispaa ya Iringa, Asilimia 67.2.
Kwa upande Halmashauri za Miji, mshindi wa kwanza ameibuka
Halmashauri ya Mji wa Njombe huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Halmashauri ya
Mji wa Kahama na mshindi wa tatu ni Halmashauri ya Mji wa Tunduma.
Washindi
wa Halmashauri bora inayotekeleza kwa ufanisi Kampeni hiyo hususani katika
ujenzi na matumizi ya vyoo bora, mshindi wa kwanza ni Halmashauri ya Wilaya ya
Meru, kwa mshindi wa Pii imechukuliwa na Wilaya ya Njombe huku wa tatu ni
Halmashauri ya Wilaya ya Makete.
Waziri Ummy Mwalimu
amewatangaza washindi wa Kijiji bora kinachotekeleza kwa ufanisi hiyo ya usafi
ni Kijiji cha Kanikelele kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mshindi wa
pili, Kijiji cha Nambala kutoka Halmashauri ya wilaya ya Meru, na cha tatu ni
Kijiji cha Lyalalo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.
Aidha
Vijiji hivyo viliweza kupatikana baada ya kushirikisha jumla ya Vijiji na Mitaa
80 huku Kaya zake zikiwa zimefanikiwa kujenga na kutumia vyoo bora pamoja na
sehemu za kunawia mikono kwa maji na sabuni.
Washindi
wengine wa shindano hilo ni pamoja na Hospitali Bora kwa usafi ambapo Mshindi
wa kwanza ni Arusha Lutheran Medical Centre, mshindi wa pili, Hospitali ya
Rufaa ya Mtakatifu Fransisco na Ifakara – Morogoro na wa tatu, Hospitali ya
Rufaa Mount Meru.
Aidha,
Waziri Ummy Mwalimu amewatangaza washindi kwa upande wa Hoteli, ambapo Hyatt
Regency Dar es Salaam the Kilimanjaro, iliibuka mshindi wa kwanza huku wa pili
ikienda Mount Meru Hotel, Arusha na ya tatu ni Aden Palace Mwanza. “Wizara itatoa zawadi ya
gari la kubebea taka (trekta lenye tela) kwa Halmashauri ya Mji wa Njombe
ambayo imeibuka mshindi wa kwanza kundi la Miji.
Aidha
zawadi ya gari mpya aina ya Nissan itatolewa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Meru
ambayo ilishika nafasi ya kwanza katika utekelezaji wa Kampeni ya Taifa ya
Usafi wa Mazingira, na zawadi za pikipiki aina ya YAMAHA kwa washindi wote
waliosalia ili kutoa motisha kwa mabwana Afya wote.
Pia
zawadi nyingine zitakazotolewa kwa washiriki katika makundi yote ni pamoja
Vikombe na Vyeti maalum ambapo Wizara tutaandaa siku maalum kwa ajili ya
kukabidhi zawadi hizo na tunawapongeza kwa ushindi” alimalizia Waziri Ummy
Mwalimu.
Katika
kuongeza ufanisi wa mashindano hayo, Wizara iliunda kamati maalum ambayo iliratibu
na kusimamia zoezi zima la uhakiki wa Mashindano huku wajumbe wakitoka Taasisi
mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Rais– TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Baraza la Taifa la Usimamizi wa
Mazingira (NEMC), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi - Muhimbili, Chuo
Kikuu cha Ardhi, pamoja na wadau wa Maendeleo wanaojihusisha na shughuli za
Afya na usafi wa Mazingira hapa nchini huku wakizingatia vigezo hali bora ya
usafi wa mazingira kwa ujumla.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa Habari katika mkutano wa tukio hilo Jijini Dar es Salaam, la kutangaza washindi wa shindano la Afya na usafi wa Mazingira kwa mwaka 2017, iliyokuwa na kauli mbiu ‘Nipo Tayari’.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa Habari katika mkutano wa tukio hilo Jijini Dar es Salaam, la kutangaza washindi wa shindano la Afya na usafi wa Mazingira kwa mwaka 2017, iliyokuwa na kauli mbiu ‘Nipo Tayari’. Kulia kwake ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Usafi wa Mazingira, Theophil Likangaga.
Mratibu wa kampeni ya mashindano hayo ya Usafi wa Afya ya Mazingira, Bw. Anyitike Mwakitalima akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa tukio hilo. Anayemfuatia ni Waziri wa Afya, Mh. Ummy Mwalumu na kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Usafi wa Mazingira, Theophil Likangaga
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu akiwa na nembo ya kampeni ya NIPO TAYARI ambayo inahamasisha usafi wa mazingira hasa usafi wa kunawa mikono na matumizi sahihi ya vyoo.
Mwanahabari wa mtandao wa Michuzi Media, Chalila Chibuda akiwa na nembo ya NIPO TAYARI
Mwanahabari wa Tumaini TV akiwa na nembo ya NIPO TAYARI
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu akiwa pamoja na baadhi ya wadau wa Wizara ya Afya katika habari na nembo hiyo ya NIPO TAYARI
Mratibu wa kampeni ya mashindano hayo ya Usafi wa Afya ya Mazingira, Bw. Anyitike Mwakitalima akiwa na nembo ya NIPO TAYARI
No comments:
Post a Comment