Trump amesema huenda hajakuwa akiweka ukali wa kutosha akiionya Korea Kaskazini awali
Rais wa Marekani Donald Trump
ameitahadharisha Korea Kaskazini kwamba inafaa kuwa na "wasiwasi sana"
iwapo itatenda lolote kwa Marekani.
Amesema utawala wa taifa hilo utakuwa
shida kubwa "ambayo ni mataifa machache sana yaliyowahi kukumbana nayo"
iwapo "hawatabadilika".
Amesema hayo saa chache baada ya Korea
Kaskazini kutangaza kwamba ina mpango wa kurusha makombora manne karibu
na kisiwa cha Marekani cha Guam.
Waziri wa ulinzi wa Marekani James
Mattis ametahadharisha kwamba mzozo wa kivita na Korea Kaskazini utakuwa
na "madhara makubwa" na akadokeza kwamba juhudi za kidiplomasia kwa
sasa zinaanza kuzaa matunda.
"Juhudi za Marekani zinaongozwa na diplomasia, zina msukumo wa kidiplomasia, na zinapata matokeo kidiplomasia," amesema.
Waziri mkuu wa Australia Malcolm
Turnbull amesema taifa lake liko tayari kushiriki katika vita dhidi ya
Korea Kaskazini iwapo nchi hiyo ya rasi ya Korea itatekeleza shambulio
dhidi ya Marekani.
"Iwapo kutakuwa na shambulio dhidi ya
Marekani, Mkataba wa Anzus utaanza kutekelezwa na Australia itajitokeza
kuisaidia Marekani," alisema kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio,
"vile vile ambavyo Marekani ingefika kutusaidia iwapo tutashambuliwa."
Hali ya wasiwasi imeanza kuongezeka wiki
za karibuni baada ya Korea Kaskazini kufanyia majaribio makombora
mawili ya kuruka kutoka bara moja hadi nyingine mwezi Julai.
Umoja wa Mataifa hivi majuzi uliongeza vikwazo dhidi ya Pyongyang kutokana na mpango wake wa silaha za nyuklia.
Akiongea Alhamisi Bedminster, New
Jersey, Bw Trump alidokeza kuwa huenda taarifa zake kuhusu Korea
Kaskazini hazijakuwa na ukali wa kutosha, licha ya kuionya Korea
Kaskazini wiki hii kwamba itanyeshewa na "moto na ghadhabu" kutoka kwa
Marekani.
Korea Kaskazini imepuuzilia mbali vitisho vya Marekani kama "upuuzi".
Bw Trump alishutumu serikali za awali za
Marekani akisema zilionyesha udhaifu sana zikikabiliana na Korea
Kaskazini na pia akashutumu mshirika wa karibu wa Korea Kaskazini,
akisema kwamba inafaa "kufanya juhudi zaidi."
Alisema: "Nawaambia, iwapo Korea
Kaskazini itafanya jambo lolote hata kwa kufikiria tu kuhusu
kumshambulia mtu tunayempenda au tunayewakilisha au washirika wetu au
sisi wenyewe inaweza kuwa na wasiwasi sana, sana."
"Nitawaambia ni kwa nini...ni kwa sabbau mambo yatawatendekea ambayo hawajawahi kufikirtia kwamba yanaweza kutokea."
Hata hivyo, aliongeza kwamba Marekani bado iko huru kushiriki katika mashauriano.
Aliongeza: "Nawaambia hivi, Korea
Kaskazini inafaa kujiweka sawa au wataona shida kubwa kiasi ambacho ni
nchi chache sana zilizowahi kushuhudia."
Marekani ina kambi ya jeshi la wanahewa la Andersen kisiwa cha Guam\
Korea Kaskazini ilisema Jumatano kwamba
inapanga kurusha makombora ya masafa wa wastani na ya masafa marefu
kuelekea kisiwa cha Guam, ambapo kuna kambi ya ndege za kivita za
kuangusha mabomu za Marekani.
Hata hivyo, kufikia sasa hakujakuwa na dalili zozote kwamba huenda kisiwa hicho cha Guam kikashambuliwa.
Kisiwa cha Guam na umuhimu wake
- Kisiwa cha Guam kina ukubwa wa kilomita mraba 541 (maili mraba 209) na kinapatikana bahari ya Pasifiki kati ya Ufilipino na Hawaii.
- Ni jimbo "lisilo na mpangilio wowote, na lisilojumuishwa kikamilifu" la Marekani, lenye wakazi karibu 163,000.
- Kambi za jeshi la Marekani hutumia karibu robo ya ardhi ya kisiwa hicho. Marekani ina wanajeshi 6,000 kisiwa hicho na kuna mipango ya kuwasafirisha maelfu wengine huko.
- Ni kituo muhimu katika shughuli za kijeshi za Marekani, ambapo huwezesha wanajeshi wa nchi hiyo kufika maeneo mengi muhimu Pasifiki, mfano eneo la bahari linalozozaniwa la South China Sea, rasi ya Korea na mlango wa bahari wa Taiwan.
Bw Trump alikuwa amewaambia wanahabari
Jumanne kwamba: "Korea Kaskazini wasidhubutu kutoa vitisho zaidi kwa
Marekani. Watajibiwa kwa moto na ghadhabu ambayo ulimwengu haujawahi
kushuhudia."
Seneta mkongwe wa Marekani John McCain hata hivyo alikuwa na shaka kuhusu tamko la Trump.
"Viongozi wengi wakuu ambao nimewahi
kuwaona, huwa hawatoi vitisho ikiwa hawako tayari kuvitekeleza na sina
uhakika kwamba Rais Trump yuko tayari kuchukua hatua," alisema Bw
McCain.
Korea Kaskazini ilikuwa imeghadhabishwa na vikwazo vipya ilivyowekewa na Umoja wa Mataifa siku ya Jumamosi.
Vikwazo hivyo vina lengo la kupunguza mapato kutoka kwa mauzo ya bidhaa nje ya Korea Kaskazini kwa theluthi moja.
KCNA imesema Korea Kaskazini, ambayo
imefanyia majaribio silaha za nyuklia mara tano, itajibu vikali na
kwamba "Marekani italipia" kwa kuchangia kutunga vikwazo hivyo.
CHanzo:BBC
No comments:
Post a Comment